MADHARA YA ULEVI
(Sehemu ya pili)
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu katika mwendelezo wa somo letu sehemu ya pili.
Leo kwa neema za Mungu tutajifunza madhara ya ulevi ndani ya kanisa.
Tunaposema ulevi ndani ya kanisa..hatulengi ule ulevi wa nje/mwilini kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza bali tunalenga ulevi wa rohoni.
Upo ulevi wa rohoni ambayo adui ibilisi ameingiza katikati ya waaminio, na kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza moja ya madhara ya ulevi ni mtu kupoteza ufahamu..Sasa kutokana na divai/kilevi ambayo shetani ameingiza ndani ya kanisa..imesababisha wakristo wengi kupoteza fahamu zao na mwisho wakabaki kuwa UCHI ROHONI na kibaya zaidi hawajitambui kuwa wapo uchi (madhara ya ulevi)
Hebu tuangalie hiyo divai/kilevi ambayo shetani aliingiza ndani ya kanisa na kuwalewesha waumini.
Ufunuo wa Yohana 17:1 “Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;
2 ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi WAMELEVYWA KWA MVINYO YA UASHERATI WAKE.
3 Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.”
Umeona hapo, huyu kahaba jinsi alivyoilevya kanisa na dunia yote kwa MVINYO YA UASHERATI WAKE, huu ndio ulevi ambao tunauzungumzia katika somo hili.
Mvinyo unaozungumziwa hapo, sio pombe.. Bali ni mafundisho ya uongo ambayo yanampelekea mwamini kuacha njia ya kweli (Yesu Kristo) na kutumikia ulimwengu na kuupenda..na huo ndio Uzinzi na ulevi wa rohoni ambayo ni hatari sana.
Kama biblia inavyosema..
Hosea 4:11 Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.”
Mafundisho yote yasiyomfanya mtu kuwa mtakatifu bali inamfanya mtu kuwa vuguvugu na kuupenda ulimwengu hiyo ni mvinyo kutoka kwa yule kahaba…na mwisho wa kunywa hiyo mvinyo ni kupoteza ufahamu na kushindwa kujitambua kabisa..na hiyo ndio ajenda ya ibilisi katika nyakati hizi za mwisho.
Biblia inasema kanisa la Laudikia ambalo ndilo kanisa la mwisho ni kanisa lililo vuguvugu na ambalo linajiona kuwa tajiri kumbe ni maskini, ni kipofu na UCHI.
Ni kwasababu gani halijioni kuwa ni maskini, na kipofu na uchi? ni kwasababu limepoteza fahamu baada ya kulevywa na ule mvinyo wa yule kahaba. (Madhara ya ulevi)
Ufunuo wa Yohana 3:14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika;
Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na UCHI.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”
Umeona madhara ya ulevi ndani ya kanisa.
Hebu jipime, je! ufahamu wako upo sawa kweli?
Ikiwa unapenda tu kuhubiriwa mafanikio ya hapa duniani na huku roho yako haina usalama, basi yawezekana fahamu yako imeondolewa kupitia hayo mafundisho, na ndio maana huoni kuwa upo UCHI kama vile Nuhu baada ya kulewa hakujitambua tena kuwa yupo uchi.
Ikiwa leo unatembea uchi barabarani, unavaa vimini, suruali, nguo za kubana na kuchora mwili wako, na huku huoni upo uchi, basi tambua kuwa ufahamu wako umeondolewa na hayo mafundisho kutoka kwa yule kahaba mkuu.
Sio ajabu leo hii watu hawatambui majira na nyakati hizi kuwa ni za hatari sana.. ni kwasababu wameleweshwa na mvinyo hawajitambui tena!
Ni kwanini wanashindwa kuelewa maandiko kuhusu ubatizo sahihi, nafasi ya mwanamke ndani ya kanisa, wanawake kufunika vichwa, mavazi yampasayo mwanumume na mwanamke, ibada ya sanamu, sabato halisi, n.k, jibu rahisi ni lile lile…wameondolewa fahamu zao kupitia ule mvinyo.
Hivyo ndugu: Angalia aina ya mafundisho unayofundishwa mahali ulipo; je! yanakufanya kuwa mtakatifu au yanakupeleka kuupenda huu ulimwengu ambao unaenda kufika mwisho karibuni.
Jihadhari na mafundisho ya uongo! na yale yanayokufanya tu uone vitu vya kidunia na vile vinavyokuja huoni maana yatakuondolea ufahamu na mwisho utajikuta upo uchi pasipo kutambua kuwa uko hivyo. (Hizi ni siku za mwisho unyakuo wa kanisa upo karibu)
Mpende Bwana kwa moyo wako wote na roho yako yote na Bwana atakuongoza katika njia yake.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.