BABELI MKUU MAMA WA MAKAHABA
Jina la Bwana YESU Mfalme wa Wafalme na Mkuu wa Uzima libarikiwe daima.
Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.
Siku ya leo tutajifunza kwa ufupi kuhusu siri ya uasi iliyojificha ndani ya kanisa, na tunapozungumzia siri ya uasi tunalenga ile roho ya mpinga kristo ambayo inatenda kazi tangu kanisa la kwanza hata sasa.
1Wathesalonike 2:7 ” Maana ile SIRI YA KUASI hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.”
Sasa hii siri ya kuasi (mpinga kristo), kama tunavyosoma hapo.. hata sasa inatenda kazi ndani ya kanisa, lakini ni kwa siri ndio yule mwanamke aliyempanda yule mnyama ambaye katika kipaji cha uso wake ana jina limeandikwa kwa siri BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. Tusome..
Ufunuo wa Yohana 17:1 Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;
2 ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.
3 Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.
5 Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.”
Sasa kuna maswali hapo ya kujiuliza kuhusu huyu mwanamke.
Swali la kwanza, kwanini ni Babeli Mkuu?
Hii inamaanisha kuwa kulikuwa na Babeli nyingine zilipita lakini sio KUU, Babeli ile iliyotengeneza mnara ilikuwa ni Babeli lakini sio kuu!..Babeli ya Nebkadneza ilikuwa ni Babeli lakini si kuu!…Hivyo hiyo Yohana aliooneshwa ndio kuu!!
Na swali lingine ni kwanini ni MAMA WA MAKAHABA?,
Hii inamaanisha anao watoto (mabinti) ambao nao ni makahaba, na yeye mwenyewe anafanya ukahaba..
Sasa kumbuka mwanamke kibiblia anawakilisha kanisa (Waefeso 5:31-32, 2Wakorintho 11:2, Ufunuo 21:9) Na kama yeye ni kanisa ni wazi kuwa waototo wake nao watakuwa ni makanisa na wote wanafanya ukahaba…..Kanisa linalofanya ukahaba kibiblia ni kanisa linaloabudu sanamu, na kuacha sheria za Mungu…Na mwisho inamalizia NA MACHUKIZO YA NCHI…Na sio machukizo ya Mbingu…maaana yake anafanya machukizo akiwa hapa hapa duniani! machukizo ni jambo lolote linalomchukiza Mungu.
Kwahiyo ile siri ya kuasi (mpinga Kristo), inatenda kazi yake kwa siri kupitia uvuli wa kanisa lake la uongo alilolianzisha, ndio yule mwanamke na mpaka sasa amezaa zaidi ya mabinti 4000 ndio wale makahaba au yale makanisa mengine madogo.. kumbuka mama yao ni kahaba mkuu (Dhehebu kubwa), hivyo watoto wake ndio madhehebu mengine yaliyosalia.
Na huko ndiko mpinga Kristo anatengeneza ile sanamu yake ambayo atakuja kuisimamisha siku za mwisho katika utawala wake baada ya kanisa la kweli kunyakuliwa.
Ndugu mpaka sasa sanamu ya mnyama (mpinga Kristo) tayari imetengenezwa ni kusimamishwa tu, ndio huo mfumo wa kuyaunganisha madhehebu yote pamoja (World Council of Churches) ambapo mpinga Kristo atakuja kuyatengenezea katiba moja, kila dhehebu litasajiliwa katika huo mfumo na iwapo mtu atakataa kusajiliwa, hatoweza kufanya ibada, wala kufanya chochote kwani wakati huo kila kitu kitasajiliwa, na hiyo ndio chapa ya mnyama jinsi itakavyofanya kazi, pasipo kuipokea hiyo huwezi kuishi kwa wakati huo.
Kumbuka wakati huo hauko mbali, kumekaribia sana.. hivyo huu sio wakati wa kuendelea kushikilia dini na udhehebu, huu ni wakati wa kumtafuta Mungu kweli.
Ikiwa na maana kama bado hujatubu kwa kumaniasha kabisa kuacha dhambi, ni wakati sasa wa kumaniasha kutubu kwasababu muda ulio bakia ni mfupi.
Hivyo ndugu, hebu itazame mwisho wako itakuwa wapi? Je! hiyo njia unayopita ni njia sahihi kulingana na biblia?
Biblia inasema Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. tena inasema..
“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.
Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo7:13-14)
Angalia ni njia gani umechagua kupita, je ni ile pana au ile nyembamba ambayo wengi hawataki?
Njia nyembamba ni ile inayosema msiipende dunia wala mambo yaliyomo duniani lakini ile njia pana inasema duniani kuna usalama (inahubiri tu mafanikio ya hapa duniani na kumfaraji mtu mwenye dhambi aendelee kuishi hivyo),
Lakini ile nyembamba inasema watu watendao mambo ya jinsi hiyo..uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, ulevi n.k hawataridhi ufalme wa Mungu na kwamba wasipotubu sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kiberiti sawa sawa na Ufunuo 21:8.
Vilevile ile njia pana inahubiri kwamba mwanamke kuvaa suruali, nguo fupi, na zinazoonyesha maungo yake ni sawa tu maana Mungu anaangalia moyo.. Lakini ile njia nyembamba inasema Mungu anaangalia moyo na mwili (2Wakorintho7:1) hivyo mwanamke kuvaa suruali ni machukizo kwa Mungu (kumbukumbu 22:5).. mwanamke wa kikirsto anapaswa avae kwa kujistiri maana yeye ni nuru ya ulimwengu. (Mathayo5:16)
Njia pana inasema mwanamke kujipamba ni urembo na ni kumpendeza mumewe.. Lakini njia nyembamba inasema kujipamba kwenu kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, KUSUKA NYWELE; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. (1Petro3:3-5),
Kwa maana hiyo kuvaa hereni, mikufu, vipini, nywele za bandia, kucha za bandia, kuweka rangi mdomoni/lipustick na kujipodoa/make up ni machukizo kwa Mungu maana miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu (1Wakorintho6:9)
Njia pana inahubiri ubatizo wa maji na Roho Mtakatifu hauna umuhimu..ukishapokea Roho imetosha, lakini njia sahihi inasema mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuona ufalme wa Mungu (Yohana 3:5) na kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji mengi na ni kwa jina la Yesu Kristo, na kuzaliwa kwa Roho ni kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Na vyote vina umuhimu.
Swali! Je! Umechagua kupita njia ipi?
Maamuzi ni yako, Mungu ametuwekea njia ya uzima na mauti mbele kwamba sisi tuchague.
Ila anatusihii tuchague ile ya uzima ambayo ni nyembamba.
Hivyo usiangalie kiongozi wa dini yako au dhehebu lako, au ndugu yako, au mzazi, hebu amua kujikana nafsi na kuchukua msalaba wako na kupita kwenye ile njia iendayo uzimani ambao wengi hawapendi… kumbuka ni wachache waionao, fanya hivyo ili uokoe nafsi na roho yako.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.