MADHARA YA ULEVI

Biblia kwa kina No Comments

MADHARA YA ULEVI

(Sehemu ya kwanza)

Shalom: Jina Tukufu la Bwana Yesu libarikiwe milele.

Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Je! Unafahamu madhara  ya ulevi kibiblia? Mbali na zile zinazojulikana na wataalamu wa afya, leo tutaangalia madhara ya ulevi hasa katika biblia ni zipi…karibu ufuatane nami katika somo hili naamini utajifunza kitu na kama wewe ni mlevi, basi leo utaacha ulevi kabisa na utawahubiria wengine waache ulevi.

Kwanza kabla hatujaangalia madhara ya ulevi ni zipi, ni vizuri ufahamu kuwa tunapozungumzia ULEVI hatulengi tu ulevi wa pombe basi, bali tunalenga ulevi wa mambo yote mabaya… ambayo yanaweza kuleta madhara kimwili na kiroho pia.

Watu wengi ni walevi siyo kwa sababu wanapenda ulevi. Ukikutana na walevi, baadhi yao utakuta wanasema “Natamani sana kuacha ulevi ila sasa kila nikijaribu kuacha nashindwa.” Watu wanaosema hivyo ujue tayari wameshakuwa watumwa wa ulevi na kwamba mara nyingi au mara kadhaa wamejaribu kuacha tabia hiyo lakini wameshindwa kuacha.

Kuwa mtumwa wa ulevi ni jambo linaloumiza sana. Nina ndugu zangu amabo ni walevi haswa, kwa hiyo ninapozungumzia kuhusu ulevi najua kwa sababu nimeishi na walevi.

Ulevi siyo tu kunywa pombe sana. Ulevi upo wa aina nyingi ingawa watu wengi wakisikia neno ulevi, wazo linalowajia kichwani ni unywaji wa pombe. Ni kawaida watu kuwa na mtazamo wa kuwa mlevi ni yule anayekunywa pombe tu kwa sababu ni mazingira na utamaduni ndiyo unafanya wawe hivyo. Siyo kosa lao na hatuwezi kuwalaumu.

Ulevi wa kufanya tendo la ndoa ni ulevi kama ulivyo ulevi mwingine wa kunywa pombe. Ni ulevi kama ulivyo ulevi mwingine kwa sababu watu hawa wote wameshindwa kudhibiti akili zao kwenye utumiaji wa vitu hivyo. Kadhalika mtu anayevuta sigara ni mlevi kama alivyo mlevi wa mapenzi na mlevi wa pombe.

Watumiaji wa madawa ya kulevya kama heroin, cocaine na bangi ni walevi sawa na walevi wengine na wote wameshindwa kudhibiti ulevi wao. Pia kuna ulevi mkubwa wa ulaji wa vyakula na unywaji wa vinywaji laini ambao watu wengi huwa hawahesabu kama ni moja ya ulevi.

Kuna ulevi wa kutumia mitandao ya kijamii au intaneti. Kuna vitu ambavyo huwezi kufanya mpaka ufanye kitu fulani. Mfano mtu hawezi kulala mpaka aingie mtandaoni kuperuzi. Wote huu ni ulevi.

Ulevi nini? Ulevi ni tabia au hali ya mtu kushindwa kukaa kwa kipindi cha muda fulani bila kutumia kitu fulani na asipotumia kitu hicho, matokeo yake ni kujisikia vibaya mpaka atumie kitu hicho. Ile hali ya kujisikia vibaya huondoka kwake kwa muda.

Kuna watu hawawezi kukaa na kumaliza wiki, mwezi na hata miezi bila kufanya kitu fulani. Huu ndiyo ulevi wenyewe ninaozungumzia hapa wengine hawawezi kukaa na kumaliza masaa, siku, wiki, mwezi na miezi bila kuvuta sigara huku wakijua au kwa kutokujua sigara wanayovuta inaenda kuharibu sehemu ya mapafu/mwili.

Kadhalika kuna watu hawawezi kukaa na kumaliza wiki hata mwezi bila kutumia vyakula kama chipsi, na vinywaji kama soda na juisi. Huu wote ni moja ya ulevi na yeyote asiyweza kukaa kwa kipindi cha muda fulani bila kutumia vitu hivi na vinginevyo ni mlevi kama walivyo walevi wengine. Wote wameshindwa kuendesha akili zao wanavyo taka wao ziende badala yake akili zao zinawaendesha wao zinavyotaka waende.

Hebu tuangalie kwa ufupi madhara ya ulevi kibiblia.

1:Ulevi huondoa ufahamu

Hosea 4:11 “Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.”

Hiyo ni dhara la kwanza linalompata mtu mlevi. Sasa utajiuliza ni kwa namna gani ulevi unaondoa ufahamu wa mtu?

Tukirudi kwenye ile habari ya Nuhu ambaye tunamsoma katika Mwanzo 9..biblia inasema baada ya Nuhu Kutoka katika safina alianza kuwa mkulima wa mizabibu, akanywa divai, akalewa, akawa UCHI katika hema yake. (akapoteza ufahamu)

Mwanzo 9:20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu;

21 akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.

22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.

23 Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.

24 Nuhu AKALEVUKA KATIKA ULEVI wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea.”

Umeona hapo, Nuhu baada ya kulewa, alipoteza fahamu zote..hadi akawa ajitambui kuwa yupo uchi..mpaka baadaye alipokuja kulevuka katika ulevi wake yaani kurudiwa na fahamu tena ndipo akajua kumbe alikuwa uchi.

Hayo ndio madhara ya ulevi, unapolewa aidha kwa divai/pombe, au kilevi kingine mbali na pombe, unapoteza ufahamu wako, na hatimaye unabaki uchi.

Na kubaki uchi sio tu kuacha mwili wazi, bali pia kubaki tupu katika maisha ya kawaida ni uchi. Walevi wengi ni vigumu kupata mafanikio, sio kwasababu hawana fedha bali wanaziwekeza kwenye ulevi badala wawekeze kwenye miradi mbali mbali.

Ndio hapo utakuta mtu yupo radhi auze hata kiwanja ili apate tu fedha ya kwenda kulewa, wanafunzi wengi wameshindwa kumaliza masomo yao kwasababu wametumia ada kwenye kamari, kubeti, kufurahia anasa na starehe n.k, sasa kwa hali hiyo kwanini usibaki uchi!. Hayo ndio madhara ya ulevi.

Unapokesha kutazama filamu, kucheza magemu, kuperuzi mitandaoni, unajipunguzia ufahamu wako, na mwishowe unabaki uchi..huo muda ungepaswa ufanye ama utafakari mambo yanayojenga maisha yako.

Vilevile unapokunywa pombe, unapotumia madawa ya kulevya kama sigara, bangi n.k unapoteza fahamu yako kabisa, kumbukumbu zako zinapotea na hatimaye unaweza kupoteza akili kabisa, hata wataalamu wa afya wanadhibitisha hilo…we fikiria mtu amelewa mpaka anabaki uchi hajitambui tena!. Ufahamu wake umeondoka kabisa.

2: Dhara la pili ambalo ndilo kubwa kabisa linalomtokea mtu mlevi ni KUKOSA KUURIDHI MBINGU.

Biblia inasema walevi hawataridhi ufalme wa Mungu.

1 Wakorintho 6:9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

10 wala wevi, wala watamanio, WALA WALEVI, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.”

Umeona hapo, walevi wote pasipo kujalisha walevi wa pombe, au walevi wa aina yoyote hawawezi kuurithi ufalme wa Mungu bali sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti ndivyo biblia inavyosema..(Wagalatia 5:19).

Sasa swali nitaachaje ulevi?

Swali nzuri sana.

Jibu unaacha ulevi kwa njia moja tu, nayo ni kumpkokea YESU KRISTO, yeye tu ndiye atakayekupa maji ambayo itakata kiu ya ulevi ndani yako..kama alivyosema mwenyewe..

Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.”

Sasa nitampokeaje Yesu?

Unampokea Yesu kwa kumaanisha kabisa kutubu na kuacha dhambi. Unaamua kabisa ndani ya moyo wako kusema kuanzia leo mimi na ulimwengu basi, mimi na disko basi, mimi na pombe basi, mimi na kamari, kubeti, n.k ndio basi sitorudia tena, unasema hivyo na kuanzia wakati huo unazitupa kabisa hizo chupa za pombe, unazichoma hayo mavazi ya nusu uchi, unafuta magemu yote kwenye simu yako na miziki yote ya kidunia na mambo yote ambayo yalikuwa yanakulewesha, unampa Yesu maisha yote, na kuanzia wakati huo Yesu anaingia ndani yako na ghafula unapokea nguvu ya ajabu ambayo itakufanya uchukie dhambi kabisa, kiu yote inakatika kabisa ndani yako.

Baada ya hapo hatua ya pili unaenda kujiunga na kanisa ambalo Roho wa Mungu atakuongoza ili ukabatizwe kwa kuzamishwa kwenye maji na kwa jina la Yesu Kristo..na kuanzia huo wakati unaanza kulewa kwa Roho wa Kristo..na utaufurahia sana wakovu na kumpenda Mungu.

Hivyo ikiwa upo tayari kumpokea Yesu leo, basi nitaenda kukuongoza sala fupi ya kumkaribisha Yesu maishani mwako..

Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobaki ni wewe kuthibitisha toba yako kwa matendo na kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu.

Hongera kwa kuokoka.

Sehemu ya pili tutaangalia madhara ya ulevi ndani ya kanisa.

Je mtu aliyeokoka anaweza akawa mlevi? Tazama sehemu ya pili.

Ikiwa utapenda kupata msaada Zaidi, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *