MAMBO HAYO YAANZAPO KUTOKEA.
Jina kuu tukufu..jina la Bwana Yesu Kristo Mfalme wa dunia yote na Mkuu wa Uzima libarikiwe.
Karibu tuyatafakari maneno ya Uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Na leo kwa msaada wa Roho Mtakatifu nataka tutafakari kwa umakini kauli moja ambayo Bwana Yesu alisema kuhusu ujio wake wa mara ya pili.
Bwana alisema…
- Luka 21:28 “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”
Unaelewa maana ya hiyo kauli kwa usahihi?
Bila shaka kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia…naamini sio mara ya kwanza kusoma andiko hilo, ila yamkini bado hujaelewa maana ya hilo andiko katika nyakati hizi tunazoishi…na leo naomba Roho Mtakatifu akujalie uweze kuelewa na kuchukulia kwa uzito wake.
Mimi binafsi Roho Mtakatifu aliponifumbua macho nikaelewa, nilishutuka na kushangaa sana… maana Bwana Yesu alisema mambo ambayo yamekwisha kutokea siku nyingi.
Sasa ukisoma kwa umakini.. Bwana alisema “..mambo hayo yaanzapo kutokea…”
Ni mambo gani hayo ambayo Bwana alisema yaanzapo kutokea tuchangamke tukaviinue vichwa vyetu maana ukombozi wetu umekaribia?
Ukirudi nyuma kuanzia mstari wa 7..utaona Bwana alikuwa anasema dalili za kuja kwake na ya mwisho wa dunia, alisema kutatokea vita kati ya taifa na taifa, kutatokea matetemeko ya ardhi, kutatokea tauni, kutatokea manabii wa uongo na makristo wa uongo, n.k…Soma tena Mathayo 24 na Marko 13 utaona hayo mambo ambayo Bwana alisema yaanzapo kutokea basi tujue kuja kwake kumekaribia sana.
Kumbuka anasema YAANZAPO KUTOKEA NA SIO YAKISHATOKEA!.
Sasa hayo mambo (hizo dalili) zilianza kutokea miaka mingi iliyopita… kabla hata hatujazaliwa…Yaani yalianza hayo mambo yalianza kutokea kuanzia karne ya 20.. miaka zaidi ya mia imepita sasa tangu yaanze kutokea…hii ni kuonyesha ni kwa namna gani Bwana Yesu amekaribia…yawezekana kabisa sisi tunaoishi kizazi hiki yaani mimi na wewe tukashuhudia tukio la kurudi kwa Bwana kuja kulinyakua kanisa lake yaani tukio la UNYAKUO…kwani hayo mambo karibia zote yamekwisha tokea huko nyuma. Alisema tena..
Luka 21:29 “Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingi e yote.
30 Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu.
31 Nanyi kadhalika, MWONAPO MAMBO HAYO YANAANZA KUTOKEA, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.
32 Amin, nawaambieni, Kizazi hiki, hakitapita hata hayo yote yatimie.
33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Ndugu unaona ni wakati gani tunaishi? Huu ni wakati wa jioni sana… Bwana alisema kizazi hiki hakitapita mpaka hayo yote yatimie.
Kizazi ambacho Bwana alisema ni kizazi kilichoshuhudia hayo mambo yakianza kutokea…ikiwemo kuchipuka kwa mtini yaani taifa la Israeli kuwa huru.. Taifa la Israeli linafananishwa na mti unaozaa matunda ya tini (soma Yeremia 24). Na katika historia Israeli haikuwa huru zaidi ya miaka 2500 mpaka mwaka 1948 ilipofanyika kuwa huru ili kutimiza unabii wa “Isaya 11:11-12″ sasa hicho kizazi kilichoshuhudia Israeli kuwa taifa huru na dalili zingine ambazo Bwana alisema katika Mathayo 24 na Marko 13… hicho kizazi hakitapita mpaka hayo yote yatimie… Kumbuka anasema hakitapita na sio hakitatimia.
Je! Bado umeinamisha kichwa chini kuutazama ulimwengu? Bwana anakuambia leo inua kichwa chako mtazame maana yupo karibu.
Ikiwa na maana kama hujaokoka, basi huu ndio muda sahihi kwako wa kumpkokea Yesu kabla mlango wa neema haujafungwa.
Unachopaswa kufanya ni kudhamiria kutubu dhambi zako zote na kuamua kuacha ulimwengu kabisa kwa kujikana nafsi yako na kumfuata Bwana Yesu.
Dhamiria kuacha matendo yote ya giza kama uasherati, ulevi, anasa, wizi, uongo, usengenyaji, kujichua, uvaaji mbaya, na mengine yote yaliyotajwa katika wagalatia 5:19-21 na yanayofanana na hayo… baada kutubu kwa vitendo hatua inayofuata ni kutafuta kanisa la kweli ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo sawa sawa na matendo 2:38 ili kukamilisha toba yako na kupokea mhuri wa Roho Mtakatifu…atakayekusaidia kishinda dhambi na kukufundisha mengineyo.
Na kama uliokoka ukarudi nyuma.. basi fahamu tupo ukiongoni mwa siku za mwisho na Bwana Yesu yupo karibu. Kumbuka ni wapi ulikoanguka ukatubu na kuurudia upendo wako wa kwanza, huu ni wakati wa kukesha kweli kweli..sio wakati wa kulegea na kutazama nyuma kwenye ulimwengu…huu ni wakati wa kuinua vichwa vyetu na kumtazama Kristo maana ukombozi wetu umekaribia.
Luka 21:28 Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.