NIMEOKOKA NAMPENDA YESU.

Uncategorized No Comments

NIMEOKOKA NAMPENDA YESU.

Shalom: jina la Bwana Yesu libarikiwe. Karibu tuongeze ufahamu wa kumjua Mungu.

Unaelewa maana halisi ya kuokoka na kumpenda Yesu?

Katika  siku hizi za mwisho, Neno hili “kuokoka na kumpenda Yesu” au kukiri ukristo. Limekuwa likitumiwa kinyume na ukweli wa Neno lenyewe. Kwani kila mtu sasahivi ukimuuliza umeokoka?

Moja kwa moja atakujibu bila kusita ”ndiyo nimeokoka ” tena ataongeza nimeokoka na nampenda Yesu.

Hata kama matendo yake yanamshuhudia kabisa kuwa anayoyasema sio kweli, bado atakiri yeye ni mkristo “ameokoka na anampenda Yesu”.

Nimekutana na watu wengi wa namna hiyo, na wengi wa hao wanataka uwatatulie matatizo yao kwa “maombi” ukiwauliza umempa kwanza Yesu maisha yako! anakujibu ndiyo, nimeokoka na nampenda Yesu, ukimwambia ni lini umeokoka, anakuambia ana zaidi ya miaka mitano (5). Sasa ukimwangalia huyu mtu hafananii kabisa na mtu aliyeokoka kweli mwezi moja uliopita.

Neno hili “nimeokoka na nampenda Yesu” ni neno ambalo shetani ameachilia siku hizi za mwisho katikati ya watu ili kuzuia wasipate wokovu wa kweli! (Ni ajenda ya shetani).

Ndio maana hata mtu wa kidunia ambaye hamjui hata Yesu..anakiri ameokoka, utamwona mlevi, muasherati, mshirikina, muabudu sanamu, muhuni n.k anatumia hiyo fursa, kustiri dhambi zake.

Sasa mtu wa namna hii ataokokaje? ambaye ukijaribu kumleta kwenye ukristo wa kweli..anakuambia nimeokoka tena nampenda Yesu…bila shaka anahitaji neema kubwa.

Kitu ambacho pengine watu hawafahamu au wamedangwanywa na shetani ni kwamba “kuokoka na kumpenda Yesu” sio tu kwenda kanisani kila jumapili, sio tu kuwa mwaminifu kwenye eneo la utoaji, sio tu kujiunga na praise au kwaya, na kusema unampenda Yesu.

Tafsiri ya kuokoka ni kusalimika kwenye hatari fulani, sasa kwenye ukristo kuokoka ni kusalimika na hasira ya Mungu ambayo itamwagwa katika dunia yote kwa waovu, ukiokoka anakua umeikwepa hiyo hasira, wakati wa ghadhabu ya Mungu wewe hautakuwepo..utakuwa umefichwa mbali, pia utakuwa umeokoka na ziwa la moto.

Kwahiyo kuokoka ni kutolewa kwenye ulimwengu huu ulio haribika na kuingizwa kwenye ulimwengu mwingine ulio bora. Na mtu yoyote aliyeokoka, ni lazima awe na dalili ya kuchukia ulimwengu huu…na yeye mwenyewe kuchukiwa na ulimwengu kwakuwa yeye sio wa ulimwengu huu. (Yeye na ulimwengu ni vitu viwili tofauti). Ndio maana Bwana alisema..

Yohana 15:19 “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.”

Ukiona ulimwengu unakupenda na unakusifia kuwa we ni mrembo, we ni wa kisasa, na unasema umeokoka, fahamu kuwa bado hujaokolewa, bado we ni wa ulimwengu na ndio maana ulimwengu unakusifia. Ukiokoka jiandae kuonekana mjinga, mshamba na kutengwa na marafiki na ndugu ingawa sio wote,

Kuokoka ni kuachana na ulimwengu na kumfuata Yesu huku ukikana nafsi yako kila siku, kuokoka na kumpenda Yesu ni kuwa mtu wa ibada mara kwa mara, mtu wa kufunga na kuomba, mtu wa kusoma na kujifunza biblia kwa undani, mtu wa kushuhudia wengine habari njema, na kuchukia ulimwengu. Huyu ndiye mkristo aliyeokoka na kumpenda Yesu.

Mkristo ambaye hasomi Neno, anasubiri jumapili kwa jumapili, hawezi hata kudumu lisaa limoja kuomba angalau kwa siku mara moja, mwezi unapita bila kufunga, bila kukesha hata mara moja, mwaka unaisha bila kumaliza biblia, huyo sio mkristo (ni mkristo jina tu).

Vilevile mkristo ambaye hajaacha udunia, hajaacha kuvaa nguo za nusu uchi, suruali(mwanamke), hajaacha mapambo ya kidunia, fashion za kidunia, hajaacha kusuka, kuvaa hereni, kutumia vipodozi. Huyu bado hajaokoka (sio hukumu) ni ukweli kulingana na biblia.

Unasema umeokoka na bado unacheza kamari, unabeti, unasikiliza miziki ya kidunia, unashinda kutazama movies na kufuatilia mipira ila huwezi kushinda kuomba na kusoma Neno, unafanya uzinzi kwa siri, unazungumza kihuni, unalewa kisiri, unanyoa kiduku na stahili za wanamziki wa kidunia. Na bado ukiulizwa umeokoka, unasema ndiyo kwa ujasiri kabisa..tena unasema unampenda Yesu.

Utampendaje Yesu na bado unapenda dunia? Hujui ya kwamba mtu akiipenda dunia kumpenda Yesu hakumo ndani yake.

1Yohana2:15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Wawezaje kusema umeokoka na unampenda Yesu na huku bado unapenda ulimwengu. Hebu itazame njia yako ndugu, angalia matendo yako na unayoyafanya kwa siri…huwezi kusema umeokoka, na huku matendo yako na mwonekano wako unakushudia kuwa bado Yesu hajaingia ndani yako (unajidanganya).

Yeremia 2:23 Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake.

Achana na ukristo jina, acha uvugu uvugu, mpe Yesu maisha yako kweli kweli kwa kumaanisha kutubu na kuziacha kabisa dhambi zote na kuweka kando ulimwengu.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho na Bwana Yesu yupo mlangoni, na fahamu pia ukifa leo katika hali ya uvuguuvugu moja kwa moja sehemu yako itakuwa ni katika lile ziwa la moto. Usikubali shetani akudanganye, maandiko yanasema msimpe ibilisi nafasi (Waefeso4:27). Shetani ni muongo tangu mwanzo, anataka roho yako umsindikize kwenye ziwa la moto. Ndio maana anakushinikiza uwe vuguvugu kwani anajua Mungu anachukia watu vuguvugu.. Mungu anasema ni heri uwe baridi au moto kuliko kuwa hapo katikati soma Ufunuo 3:15).

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *