JE! UMEUONA USO WA MUNGU?

Biblia kwa kina No Comments

 

JE! UMEUONA USO WA MUNGU?

Jina la Bwana Yesu mwokozi wa ulimwengu libarikiwe.

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu, Na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).

Leo kwa neema za Mungu tutajifunza maana halisi ya kuuona uso wa Mungu na umuhimu wake.

Je! tunaweza tukauona uso wa Mungu? Mbona kama tunasoma katika Yohana 1:18 kwamba “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; isipokuwa Kristo pekee ndiye aliyemfunua”

Maana halisi ya kuuona uso wa Mungu sio KUMTAZAMA USONI, kwamba anaonekanaje, mwonekano wake ukoje, uso wake unafananaje n.k. La! Sio kwa namna hiyo. Bali kuuona uso wa Mungu ni KUMFAHAMU.

Kwa mfano tunaposema TUMEUONA MKONO WA BWANA, haimaanishi tumeenda mbinguni tukauona mkona wake jinsi ulivyo, au ameshuka chini tukauona jinsi ulivyo, rangi yake na idadi ya vidole alivyo navyo! N.k. La! Bali tunamaanisha tumeona uweza wake mkuu!.. Vilevile tunaposema tumemwona Bwana katika maisha yetu, haimaanishi ameshuka mbele yetu na tukamwona sura yake, bali tunamaanisha tumeona uwepo wake na kuutambua.

Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo letu, ambalo leo tunajifunza umuhimu wa kuuona uso wa Mungu au kutembea na Mungu katika ufahamu sahihi.

Upo umuhimu mkubwa wa kumfahamu Mungu na kumwelewa ni nini anachokitaka kwetu. Na tunapozungumzia kuuona uso wa Mungu au kumfahamu, tunalenga kumfahamu Yesu Kristo, yeye ndiye aliyeona uso wa Mungu katika utimilifu wote, hivyo tukimwona yeye, basi tumemona Mungu.. kama alivyomwambia Filipo aliyeniona mimi amemwona Baba. (Yohana 14:8-9)

Unaweza ukasema unamemwona Mungu, na yawezekana umemwona kweli, pengine alikutokea ukauona uso wake, au alikutendea muujiza Fulani…Ila pamoja na hayo yote, huenda bado hujamwona uso wake katika utimilifu wote, huenda bado hujamfahamu vizuri, yamkini bado hujafahamu nini anachokitaka kwako pale anapokutokea, pale anapokufanyia huo muujiza.

Usipoweza kuelewa ni nini Bwana anachokitaka kwako? Haijalishi umemwona mara ngapi, na amekufanyia miujiza mingi kiasi gani, haijalishi unatembea naye na amekuwa rafiki kwako..kama haujafahamu nini anachokitaka kwako..basi, ujue bado hujamwona uso wake na wala humfahamu kabisa.

Haijalishi unashukiwa na nguvu zake, haijalishi  amekuponya mara ngapi, au umetumia jina lake kutoa pepo, na kuponya wagonjwa kiasi gani, siku ile utakaposimama mbele yake utamwambia nimefanya hiki na hiki, nimekutumikia sana, nilikuwa nahudumia maskini, na yatima, nilikuwa nafanya hiki na hiki…ila yeye atajibu na kusema “sikukujua  kamwe;..” Ni kwanini? kwasababu hukuwahi kumwona uso wake/kumfahamu, ijapokuwa alikuwa anatembea na wewe..na kukutendea miujiza mingi.

Mathayo 7:22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Luka 13:26 ”ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulitufundisha katika njia zetu. 27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.2

8 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno…”

Ogopa sana hayo maneno ya Bwana Yesu yasije yakatimia kwako!. Maana ni wengi watalia siku ile.

Sasa ni nini maana halisi ya kuuona uso wa Mungu au kumfahamu Mungu?

Kama tulivyotangulia kusema kuuona uso wa Mungu au kumfahamu sio kuishia tu kusema Bwana amenitokea na nimeona uso wake, au nimemwona Mungu amenitendea hiki na hiki. Hapana!  bali ni kufahamu nini Bwana anachotaka kwako! Ukiweza kufahamu kile ambacho Mungu anataka kwako na ukakitendea kazi…basi, hapo utakuwa umeuona uso wake.

Sasa ni vizuri leo kufahamu kuwa kitu pekee ambacho Bwana anataka kwako ni wewe kwanza kuokoka! Na tuposema kuokoka haimaanishi hiyo tafsiri unayoijua wewe, kwamba kuokoka ni kuongozwa sala ya toba na kujiunga na kanisa (hiyo ni hatua ya pili baada ya kuokoka).

Kuokoka ni kumfahamu Yesu Kristo kile alichokileta duniani, na baada ya hapo unaamua sasa kumfuata kwa kudhamiria kutubu dhambi zote na kuziacha kabisa…huko ndiko kuokoka, na ndicho Bwana anachokitaka kwanza ukifanye, ndio maana anakuvuta kwa kila njia, anatumia miujiza kadha wa kadha kwenye maisha yako ili tu ujue kile anachokitaka… kwamba uache dhambi na umgeukia yeye, ujikane nafsi yako na umfuate yeye…ndicho Bwana anachotafuta kwako…na huko ndio mwanzo wa kuuona uso wake.

Yakobo alipokutana na Mungu uso kwa uso bila yeye kujua.. baadaye alipokuja kujua kuwa yule alikuwa ni Mungu.. alisema..

Mwanzo 32:30 “Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, NIMEONANA NA MUNGU USO KWA USO, NA NAFSI YANGU IMEOKOKA.”

Hebu na wewe jiulize je! ulipokutana na Mungu uso kwa uso kupitia maono, ndoto, wahubiri, miujiza, n.k, nafsi yako imeokoka?

Au umekuwa kama yule kipofu ambaye Bwana alimtendea muujiza mkubwa wa kuponya macho yake..na baada ya hapo akaenda kuendelea na maisha yake pasipo kujua lengo la yeye kufunguliwa katika kile kifungo ni kujikana nafsi na kujitwika msalaba wake na kumfuata Yesu.

Yohana 9:1 “Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.

2 Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?

3 Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.

6 Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate, akampaka kipofu tope macho,

7 akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa).

Sasa ukiendelea mistari inayofuata…utaona huyu kipofu baada ya kwenda kunawa kama alipoambiwa, macho yake yalipata kuona na hivyo akaenda kuendelea na shughuli zake mpaka baadaye majirani zake na wale waliomjua hapo mwanzo kuwa ni kipofu walipomhoji kuwa umepataje kuona?

Ndipo akaanza kuelezea kumhusu Yesu aliyemponya…na aliposhurutishwa kumkana, aliamua sasa kujitwika msalaba wake na kukiri kuwa Yesu ndiye aliyemponya…alikubaki kutengwa na ndugu zake pamoja na jamii yote kwa ajili ya Yesu, ndipo walipomtupa nje…na Yesu akumkuta huko  nje na kumwambia..

Yohana 9:35 “Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?

36 Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?

37 Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiwe.

38 Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.”

Ukichunguza kwa makini utaona kuwa Yule mtu hakumjua YESU ni nani, wala alipotokea, wala alipoenda wala hakumwona uso wake hata baada ya kufunguliwa macho yake. Haikujalisha alifunguliwa macho kiasi gani, yeye alichoweza kufanya ni kwenda tu kuendelea kufanya  shughuli zake za nyumbani kwao za kila siku mpaka ilipofika wakati majirani zake walipoanza kumuuliza habari za kufunguliwa macho yake. Ndipo akaanza tena kunena habari za YESU.”

Dada/Kaka inawezekana Bwana alishakufungua katika vifungo vyako kule “KWA ALIYETUMWA (SILOAMU)”…Siloamu wako anaweza akawa mchungaji Fulani, mtumishi Fulani, huduma fulani vyovyote vile. Inawezekana ulipokwenda ulipokea majibu ya maombi yako uliyokuwa umemwomba Mungu siku nyingi, ulipokwenda uliponywa, ulipokwenda ulifunguliwa, Lakini je! NI KWELI ULIKUTANA NA KRISTO? ULIONA USO WAKE?

Yule kipofu japo alifanyiwa muujiza mkubwa kama ule lakini hakuwahi kumjua Kristo, wala kumwona sura yake..Lakini baada ya kuanza kumkiri tu na kuichagua ile njia ILIYOOGOPWA NA WENGI, iliyokuwa ya hatari ya kujikana maisha kwa ajili ya jina lake. Ndipo alipokwenda kukutana na YESU uso kwa uso kule nje! Na kumfahamu vizuri yeye ni nani. Unadhani alishindwa kumkana kusema tu vile ili kuwaridhisha mafarisayo. Hakushindwa lakini alitaka kutafuta kitu kilicho bora zaidi ya aliyotendewa, Alipotengwa kando ndipo Yesu akamjia.

Ni wengi leo hii, wanadai wamemwona Mungu katika maisha yao kisa tu wamefanikishwa katika mambo yao na shughuli zao. Lakini ukiyatazama maisha yao je ni kweli wameiendea njia ya msalaba, ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba wako kwa ajili ya Kristo, na kuamua kuishi maisha matakatifu, utagundua hawajafanya hivyo na bado wanadai wamemwona Mungu.

Wanaogopa wakijaribu kufanya hivyo watatengwa na wazazi wao, wanaogopa kudharauliwa na marafiki zao, wanaogopa kuonekana ni watu wa ajabu washamba, wakiogopwa kuchukiwa na watu wa ulimwengu huu… Hawajui kuwa kule kufanikiwa kwao ilikuwa ni kwa ajili ya kulikiri jina la Kristo kwa maisha yao na si kwa midomo tu. Na pia ni kwa ajili ya wao kujitengenezea njia nzuri ya kwenda kukutana na Kristo lakini wao wanaikwepa.

Ndugu/dada tafuta kuuona uso wa Kristo kweli, acha kujivunia udhehebu, Yule kipofu hakumfahamu Kristo akiwa katikati ya Mafarisayo bali Kristo alikutanane huko nje na akamwona uso wake, toka kwenye kamba ya madhehebu ambayo inakusuia usiuone uso wa Kristo, toka kwenye udunia na maisha ya dhambi maana Kristo hapatikani huko na wala hautakaa umwone uso wake haijalishi anakufanyia nini.

Amua kujikana nafsi na kuuchukua msalaba wako na kumfuata Yesu kila siku.

Kumbuka tunaishi  ukingoni mwa siku za mwisho Kristo amekaribia kurudi.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *