MZAZI MRUDI MWANAO

Watoto No Comments

MZAZI MRUDI MWANAO

(Masomo yahusuyo malezi kwa watoto)

Wewe kama mzazi/mlezi unawajibu wa kumlea mwanao katika njia ipasavyo kama biblia inavyotuambia (Mithali22:6)

Usipomlea mtoto wako katika njia iliyobora na ukamwacha tu ajiamulie kila kitu ujue shetani atakusaidia kumlea na kumwongoza katika njia ya uharibifu,

Katika biblia tunasoma habari moja ya kijana aliyeitwa Adonia..ambaye alikuwa miongoni mwa watoto wa Daudi, huyu Adonia kipindi baba yake alipokuwa mzee, alinyanyuka na kuanza kijitangazia ufalme bila baba yake kuwa na habari, huyu alikuwa ni mdogo wake Absalomu ambaye naye kuna kipindi alijaribu kuteka ufalme wa baba yake…hali manusura Daudi apoteze ufalme kama sio Mungu kuhusika,

Sasa huyu Adonia naye alikuja kujaribu kuchukua utawala kwa nguvu bila kupewa na baba yake, jambo ambalo sio tabia njema, sasa maandiko yanasema baba yake hakuwahi kumchukiza kwa kusema nae/ama kumwonya kwa jambo lolote, labda kwasababu alikuwa anampenda sana kwahiyo hakutaka kumkemea pale anapokosea, hakutaka kumhuzunisha, hivyo siku zote alisema nae tu maneno ya kufumrahisha huku tabia yake ikiendelea kudorora, mpaka baadaye anakuja kuchukua maamuzi ya ya namna ile ambayo mwisho wake ilikuja kuwa ni mauti, hebu tusome habari hiyo kisha tuendelee..

1 Wafalme 1:5-6 “Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake.

6 TENA BABA YAKE HAKUMCHUKIZA WAKATI WO WOTE KWA KUSEMA, MBONA UMEFANYA HIVI? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.”

Endelea kusoma habari hii kwa muda wako uone alichokifanya huyu kijana.

Wazazi wengi leo hii hawataki kuwakemea watoto wao pale wanapoonekana kuwa na tabia fulani isiyo sawa, na ndio maana watoto wengi na vijana wengi wa kizazi hiki wanamezwa sana na dunia, watoto na vijana wengi wanapotea kwasababu ya kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi/walezi wao, laiti wazazi na walezi wangesimama imara kuwafundisha watoto wao mapema kumjua Mungu na kuishi kulingana na maneno ya Mungu..leo hii kusingekuwepo na wimbi kubwa la vijana wanaojiingiza katika matendo ya giza kama ulevi, uasherati, ujambazi, uhuni, ukahaba n.k,

Mzazi anachojua tu ni kumpeleka mtoto shule nzuri, kumnunulia vitu vya anasa, kumlisha chakula kizuri awe na afya bora, na kumbembeleza kila wakati kwa maneno mazuri, jambo ambalo sio baya, ila itamfaidia nini mzazi kumlea mwanaye kwa njia hizo na huku mtoto hana habari na Mungu? Ni kweli atakuwa na afya, na akili, n.k, ila hayo yote itamfaidia nini na baadaye anakuja kuwa kahaba, shoga, jambazi na mwisho kuishia jehanum, je! ni kweli hapo utakuwa umempenda au umemchukia.

Ni wazi unamchukia na unamtengenezea mazingira ya kwenda kuzimu, huku ukidhani ya kwamba unampenda pale unapomchekea kila wakati, na huku hutaki kumwadhibu au kumkemea pale anapofanya jambo baya, hutaki kumchukiza pale inapobidi, biblia inasema  “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. (Mithali 23:13).

Je! unamleaje mwanao? je! unamlea katika njia ya Bwana, unamwadhibu pale inapombidi au unamchekea tu ili asichukie tabia yake mbaya, fahamu kuwa ukishindwa kuwajibika wewe kama mzazi… mtoto wako atakuja tu kuharibikiwa na kumezwa na hii dunia iliyoharibika,

Katika nyakati hizi za mwisho, shetani anawaharibu sana watoto pale wanapokosa uongozi kwa wazazi wao kwani mzazi ni kama Mungu kwa mtoto, mzazi ndio anawajibu wa kumwongoza mwanae katika njia ipasavyo na sio mtoto amwendeshe baba yake, kwamba kila kitu mtoto anachokihitaji anapatiwa, akihitaji kutumia simu anapewa, akihitaji kuangalia katuni zenye maudhui ya kishetani na kucheza magemu anapewa, na ndio hapo utakuta mtoto muda wote yupo na simu, tv, akiangalia picha na video zisizofaa, akisikiliza nyimbo zisizofaa, na hapo ndipo milango ya mapepo yanapata nafasi ndani ya mtoto, na kama tunavyojua kazi ya shetani ni kaharibu na kuua, ndio hapo mtoto ataanza kuwa na tabia zisizoeleweka, ataanza kuwa na kiburi, lugha chafu, n.k, na mzazi kwakuwa hataki kumchukiza..hasemi neno lolote kwa mtoto, mwisho wa siku yule mtoto atakuja kupotea kabisa.

Hebu tafakari ile habari ya yule kijana aliyekuwa akisumbuliwa na mapepo wabaya hadi wanafunzi wa Bwana wakashindwa kutoa hayo mapepo, mpaka Bwana alipokuja na kuzikemea, angalia swali ambalo Bwana alimuuliza yule mzazi…

Marko9:17 Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu;

18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.

19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.

20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.

21 AKAMWULIZA BABAYE, AMEPATWA NA HAYA TANGU LINI? AKASEMA, TANGU UTOTO.

22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia.”

Sasa sio kwamba Bwana hakujua taarifa za huyo kijana, ila alimwuliza swali hilo ili kutujulisha kuwa mapepo yanawaanza watoto tangu wakiwa wadogo, hivyo ni jukumu la mzazi kumtunza mtoto wake na kumwongoza katika njia ya haki, ambayo ni kumfundisha kumjua Mungu mapema kupitia kusoma biblia, kuwapeleka kwenye madarasa ya mafundisho ya biblia, (bible study), kuwatafutia waalimu watakaomlea kiroho wakiwa mbali na wewe, vilevile na kuwaepusha kutumia simu, na kutazama movies za kidunia, picha chafu, na kusikiliza miziki ya kidunia maana hizo ni moja ya milango ya mapepo wabaya.

Vilevile usiache kumrudi pale anapokosea, mpe maonyo huku ukitumia fimbo, mvalishe mavazi ya adabu, mfundishe kuhusu namna ya kuwasiliana na watu mbali mbali, hakikisha anajifunza kusoma biblia kila siku..mwekee huo msingi wa kumjua Mungu..itamsaidia kuepuka dhambi na kuvamiwa na roho chafu, na atakuwa mtoto mwenye adabu, heshima kwako na kwa jamii yote, atakuwa nuru mahali popote atakapokuwepo, hataiacha hiyo njia mpaka atapokuwa mzee maana ni ahadi ya Mungu..Mungu hasemi uongo, Na wewe kama mzazi utapokea baraka tele kwa Mungu kwa kumlea mwanao katika njia iliyobora, Mungu atakulipa aidha kupitia huyo huyo mtoto au kwa njia nyingine.

Sasa ili mzazi uweze kumlea mtoto wako namna hiyo…huna budi na wewe uwe kwenye wokovu, tofauti na hapo itakuwa ni hatari sana kwako na kwa watoto pia, Neno la Mungu linasema kama msingi ikiharibika mwenye haki atafanya nini? (Zab.11:3) maana yake kama mzazi akipotea/akiharibika, mtoto atasalimikaje?

Kama mzazi akiwa ni vuguvugu, akiwa mkristo jina, ni mtu wa kwenda kanisani jumapili kwa jumapili, hana ratiba yake binafsi na Mungu, hana ratiba ya kufanya ibada nyumbani na familia yake, hana desturi ya kusoma biblia kila siku na kuomba kila wakati, sasa mtoto atawezaje kusoma biblia, utamkuta mzazi muda wote moyo wake upo kwenye biashara, kazi, hana muda na Mungu.. kufungua biblia mpaka kanisani, kuomba ni mpaka siku ya maombi, na bado  anasema ni mkristo, na huku Mungu kidogo na dunia kidogo, moyo wake upo kwa Mungu na pia upo kwenye mambo ya kidunia kama vile anasa za kidunia, movies, mipira, miziki ya kidunia n.k, sasa mtoto ataponaje?

Kama mzazi akiwa anafanya uzinzi kwa siri, ni msengenyaji, mwili wake amejaza kila aina ya sanamu..(hereni, bangili, hirizi, n.k), kichwa amesuka ama ameweka nywele bandia na kupamba uso kama Yezebeli, ameweka kila aina ya rangi, lipustick, wanja, n.k, na bado anadai ameokoka!. mtoto ataepukaje kuwa kahaba, ikiwa mzazi mwenyewe ni mlango wa kila aina ya roho chafu, ndio hapo utakuta mtoto amesukwa kila aina ya mtindo, ametobolewa masikio yake, amechorwa-chorwa kama mdoli, huku amevalishwa mavazi ya nusu uchi,

Ndugu mzazi/mlezi jitathimini juu ya maisha yako na ikiwa maisha yako unajua kabisa yapo nje ya Kristo, hata kama unaenda kanisani, fanya maamuzi sahihi…ya kumpa Yesu maisha yako kweli kweli.

Tubu na mgeukie Bwana Yesu akuoshe dhambi zako, na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa JINA LA YESU upokee Roho Mtakatifu ili uwe salama na watoto wako kwa ujumla.

Ukifanya hivyo, ukatubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha kabisa, ukabatizwa ubatizo sahihi, ukapokea Roho Mtakatifu, ukawa unaishi kulingana na Neno la Mungu, ukajitenga na udunia, ukaishi maisha ya utakatifu, fahamu kuwa Mungu atakuheshimu na hata watoto wako watafundishwa na yeye.. Tofauti na hapo mwisho wa siku utaangamia wewe mwenyewe na watoto wako katika lile ziwa liwakalo moto na kibiriti.

Isaya 54:13 “Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi”

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *