MKUMBUKE MUUMBA WAKO SIKU ZA UJANA WAKO
Jina la Bwana Yesu Kristo Mkuu wa uzima libarikiwe.
Karibu tujifunze Neno la Kristo.
Neno la Mungu linasema…
“Maombolezo 3:27 “Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake.”
Vijana wengi wanadhani kumtafuta Mungu ni mpaka uzeeni, mara nyingi utasikia wakisema mpaka niutumie ujana wangu kwanza vizuri… mambo ya ujana yasinipite (nile ujana kwanza), halafu baadaye nitaokoka tu!!
Hiyo ni hatari sana, nimekutana na vijana wengi wakiniambia hivyo nilipojaribu kuwaleta kwenye wokovu. Hawajui kuwa kipindi ambacho mwanadamu anatakiwa kujifunga nira kwa Kristo na kumtumikia ni wakati wa ujana, akiwa bado ana nguvu ya kupanda milimani kuomba, akiwa bado ana nguvu ya kutembea huku na huku kupeleka Injili, akiwa na nguvu ya kumwimbia Muumba wake. Hizo nguvu wanatoa kwa wanawake kwa kufanya nao uasherati, na mambo yote maovu…Na huku wakijitumai kuwa wataokoka tu siku moja baadaye, hawajui kuwa nafasi ya kuokoka uzeeni ni ndogo sana, tena unaweza usifikie huko.
Ikiwa we ni kijana na hujaokoka.. basi leo ujumbe huu unakufikia ili ubadilishe mtazamo wako kwamba utaokoka kesho au baadaye, fikiri tena upya na ufanye maamuzi sahihi ya kumgeukia muumba wako ingali bado una nguvu..Neno la Mungu linakuambia mkumbuke muumba wako siku za ujana wako, na sio siku za uzee wako, tena linakuambia ni vema mwanadamu aichukue nira yake wakati wa ujana na sio wakati wa uzee…Kuokoka uzeeni ni kujidanganya.
Mhubiri 12:1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.
2 Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
6 Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani;
7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.
Kaka/Dada mkumbuke muumba wako kabla hazijaja siku zilizo mbaya.
Leo unaposoma ujumbe huu.. baada ya hapa tafuta sehemu iliyo tulivu yatafakari maisha yako na umwombe Mungu akusamehe dhambi zako huku Ukiwa umemaanisha kabisa kuziacha na kumgeukia Mungu… baada ya kuomba msamaha inayotoka moyoni kabisa…basi Mungu ataachilia amani ndani yako…Unachopaswa kufanya sasa ni kuanza kuonyesha badiliko la nje…
Yaani kutubu kwa vitendo…nikimaanisha kama ulikuwa unasikiliza miziki ya kidunia na unazo kwenye simu yako..basi unafuta zote, kama ulikuwa unatazama picha chafu na filamu zenye maudhui ya uzinzi na unazo kwenye simu yako unafuta mara moja, magruop yasiyo na maana unaleft, marafiki wanaokuvuta kwenye mambo ya kidunia unakata mawasiliano nao unawaambia umeokoka, magemu na kamari zote kwenye simu yako unafuta kabisa, fashion zote za kidunia na mavazi yasiyo na utukufu kwa Mungu unayachoma zote mfano vimini, suruali (ikiwa we ni mwanamke), na nyinginezo zote zinazoonyesha maungo yako unazitelekeza zote wala usimpe mtu mwingine…na mapambo yote ya kidunia unayaondoa ndani ya mwili wako na kwenye sanduku unalolihifadhia…unamua kujikana nafsi yako kabisa na kumfuata Bwana Yesu..
Ulikuwa ni mwenda disko, unasema kuanzia leo mimi na disko mwisho, ulikuwa ni mlevi unasema kuanzia leo mimi na ulevi ndio baye na unazitupa mbali hizo chupa za pombe, na hizo packet za sigara unachoma moto, uhuni wote unaacha kabisa kwa vitendo..hapo utakuwa umemkaribisha Yesu ndani yako… na Yesu anakua amefufuka kwako kweli kweli.
Bila kuchelewa hatua inayofuata unatafuta kanisa la kweli ili ukabatizwe na kuungana na waumini wenzako kuendelea kuukulia wokovu na kumtumikia Bwana Yesu. Kumbuka ubatizo ni wa muhimu sana na ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu Kristo.
Fanya hivyo ndugu…maana hujui kesho yako. Ondoa hayo mawazo ya kusema nitaokoka baadaye… nafasi ya kuokoka ni sasa hivi…haujui yatakayotokea kesho na ukifa nje ya wokovu na ilihali umesikia injili huko utakakokwenda ni hatari sana kwako…Na pia tunaishi katika siku za mwisho, wakati umeenda sana Kristo amekaribia kurudi kuleta hukumu duniani.
Hizo mali unazohangaikia sasa, kwa Kristo kuna zaidi ya hayo unayoyafikiri, kuna raha ya kudumu zaidi ya hiyo ya kitambo kidogo tu ambayo dunia inakupatia.
Bwana anasema..
“Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.” (Zaburi 34:8)
Usidanganywe na uongo wa shetani kwamba kwa Kristo hakuna raha, we mwenyewe jaribu kuonja Uone.
Ila endapo ukikataa kuonja na kuingia katika hiyo raha ya milele inayopatikana kwa Kristo, ukaendelea kuutumia ujana wako kwa anasa na starehe, ukaendelea kula ujana kama usemavyo. Basi fahamu neno hili…
Mhubiri 11:9 “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hujumuni.”
Mtafute muumba wako mapema. Kama Daudi alivyofanya…
Zaburi 63:1 Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema…”
Bwana akubariki.
Tafadhali usiache kuwashirikisha wengine habari hizi njema kwa kushea.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.