Usimtafute Yesu kwasababu ya faida zako tu!.
Bwana Yesu Kristo asifiwe mwana wa Mungu. Karibu tujifunze maneno ya Mungu..
Watu wengi leo wamechoka kwa kuhangaika huku na huku kwa watumishi wa Mungu wakitafuta suluhisho la matatizo yao pasipo kufanikiwa…Mpaka wengine wamesafiri umbali mrefu wakitafuta kuponywa na kufunguliwa katika vifungo mbali mbali, Ila bado hawaoni matokeo yoyote…
Leo tutaona shida iko wapi? Je! ni kweli Yesu ameshindwa kukuponya au kusuluhisha matatizo yako, yamkini ni wewe ambaye umekuwa ukihangaika bila mafanikio na mpaka sasa umefikia hatua ya kukata tamaa na kusema labda Mungu hakupendi.
Nataka nikuambie Mungu anakupenda sana na anaona shida zako, ila kuna kitu ambacho labda hujakielewa ambacho laiti ungeelewa, leo hii usingefikia hiyo hali ya kukata tamaa..tena usingekuwa unahangaika namna hiyo kusafiri kuwafuata watumishi ambao wewe ulidhani wataweza kukusaidia.
Wakati pale jirani au mtaani kwako pengine kuna mtumishi tu wa Mungu wa kweli ambaye angeweza kukusaidia, au wewe mwenyewe ungeweza kumtafuta Yesu akakusikia. Utasema mbona nilimwita sana hakunisikia, au mbona nimeenda kwa watumishi wote waliopo pale kijijini sikupata suluhisho, ni kweli hujapata suluhisho kwasababu hii..
Yamkini upo miongoni mwa watu wanaomtafuta Yesu kwa faida zao tu.. huku ndani ya mioyo yao hawataki kuacha yale ambayo Yesu anayachukia, hawataki kuacha dhambi ila wanataka kupona, hawataki kuacha usengenyaji ila wanataka kufanikiwa kwa Yesu…Hawataki kuacha uvaaji mbaya wa vimini, masuruali, na mapambo ya kidunia ila ni wepesi kukimbilia kwa watumishi wa Mungu ili waombewe biashara zao zinawiri, ndoa zao ziwe salama, n.k mioyo yao inatafuta faida yao tu..
Mpaka hapo ndugu yangu kama uko hivyo, fahamu kuwa umeshapishana na Yesu…hata kama utasafiri kuwafuata watumishi wa mbali, huwezi kupata suluhisho la matatizo yako mpaka ukubali kumtafuta Yesu yule ambaye anasema mtu akitaka kunifuata na ajikane nafsi yake achukue msalaba wake kila siku anifuate..na sio yule Yesu wa miujiza tu ambaye wewe unamtafuta akutatulie matatizo yako na kisha uendelee na maisha ya dhambi. Ukimpata huyo Yesu wa kweli anayechukia dhambi basi umepata suluhisho la mambo yako yote.
Jiulize leo ndugu; je! unamtafuta Yesu kwa faida yako tu, au kwasababu unataka urithi uzima wa milele?..
Hebu sikia Neno la Mungu linavyosema…
Ezekieli 33:30-32 “Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA.
31]Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, LAKINI MIOYO YAO INATAFUTA FAIDA YAO.
32 Natazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi.
Bwana Yesu alisema..
Mathayo 15:8 “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami.”
Watu wengi ndivyo walivyo leo, wanaenda kanisani ili waitwe wakristo ila mioyo yao iko mbali na Kristo.
Wanajipendekeza kwa watumishi wa Mungu na kujifanya kuwa ni watu wa Mungu, kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. Kwa maana wanasikia maneno ya Mungu wasiyatende. (huo ni unafiki ambayo Bwana Yesu aliuita).
Kipindi fulani Yesu alifanya muujiza mkubwa wa kulisha watu elfu tano, baada ya kukaa nao siku tatu akiwafundisha habari za ufalme wa mbinguni… Ndipo wakahisi njaa na mahali hapo ilikuwa ni jangwa hawakuwa na vyakula isipokuwa mikate mitano na visamaki viwili tu, Ila hizo mikate mitano na hizo samaki viligeuka kuwa chakula cha kuwalisha watu zaidi ya elfu tano wakala na kushiba wote mpaka wakabakiza…Huo ni muujiza mkubwa sana.
Sasa baada ya siku kadhaa Yesu alienda zake mahali pengine kuendelea na huduma, baadaye wale watu waliofanyiwa ule muujiza wa kulichwa mikate mitano na visamaki viwili walimtafuta..wakasikia yupo mahali fulani, wakamfuata sio kwasababu ya ile ishara waliyoiona kupitia ule muujiza ila kwasababu walimjua Yesu anafanya miujiza…hivyo pengine wakataka tena wafanyiwe muujiza kama ule. Hebu tusome hiyo habari ili uone majibu ya Bwana Yesu…
Yohana 6:24 “Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashutumu wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.
25 Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwasababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye alitetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu.”
Umeona hapo, watu hawa walimwendea Yesu kwasababu mioyo yao inatafuta faida yao wenyewe. Sio kwasababu waliona ishara itokayo mbinguni ambayo ingewafanya wamwamini Yesu na kutubu dhambi zao…Ili wapokee uzima wa milele, ila wanamtafuta Yesu ili wapewe muujiza wa chakula, wapate suluhisho la matatizo yao, halafu waendelee na maisha yao ya dhambi, ndicho watu sasa hivi wanachokifanya.
Wanawaendea watumishi wa Mungu huku wakijifanya kwa vinywa vyao wanampenda Yesu, kumbe mioyo yao iko mbali sana, na ndio maana hawapokei nguvu za Mungu ambazo ingewafanya wawe huru na vifungo vyote, kwasababu mioyo yao inatafuta faida zao tu, mioyo yao haijapondeka na kukubali kuacha machukizo, hawajakubali kuondoa sanamu ndani ya mioyo yao.. wanataka tu wafanyiwe muujiza!! Hawajui kusudi la kwanza la Mungu kumleta Yesu duniani si kwamba tuwe matajiri tu bali kusudi la kwanza ni ili tupate uzima wa milele kupitia yeye baada ya kuwa tumemwamini na kudhamiria kutubu dhambi zetu kwa kuziacha kabisa.
Ndugu, fahamu leo kuwa Mungu haangalii moyo unaotafuta faida yake tu, bali anaangalia moyo uliopondeka na kukubali kuacha dhambi., Wala haangalii kwamba unahudhuria kanisani kila jumapili au unatoa fungu la kumi kwa uaminifu, au unaimba kwaya, au unawatunza watumishi wa Mungu..hayo yote ni vizuri kufanya kama mkristo. Ila angalia moyo wako, je! unayafanya hayo yote kwasababu gani? Je ni kwasababu unatafuta faida yako mwenyewe au kwasababu unampenda Bwana Yesu. Je! unaposikia Neno la Mungu kupitia watumishi wake au wewe mwenyewe ukisoma..je! unalitii hilo Neno? je ni mahubiri mangapi umesikia yanayokuambia ubadilike na ukayatii?
Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; LAKINI MTU HUYU NDIYE NITAKAYEMWANGALIA, MTU ALIYE MNYONGE, MWENYE ROHO ILIYOPONDEKA, ATETEMEKAYE ASIKIAPO NENO LANGU.
Amri kuu tuliyopewa ni kumpenda Bwana kwa mioyo yetu yote, na kwa roho zetu zote, na akili zetu zote, na kwa nguvu zetu zote. (Mathayo12:30)
Na kumpenda Bwana ni kuzichika amri zake (Neno lake)
Yohana 14:21 Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote… usimtafute Mungu kwasababu ya faida yako tu!. ukimpenda Bwana kwa moyo wako wote utabarikiwa, hayo unayoyatafuta utazidishiwa na zaidi uzima wa milele. Ila moyo wako ukiwa unatafuta faida yako tu…basi fahamu kuwa unajitafutia laana kwa Mungu, ndivyo biblia inavyosema…
1Wakorintho 16:22 Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa..”
Leo hii unaposikia Neno la Mungu ambalo linakuambia mwanamke kuvaa mavazi ya mwanamume(Suruali) na kuvaa vimini na kujipamba kwa mapambo ya kidunia yaani kusuka, kuvaa hereni, kutumia mkorogo/makeup, kuweka kucha rangi, kuvaa hereni, wigi na kuvalia mavazi yanayochora maungo yake ni machukizo mbele za Mungu sawasawa na 1Petro3:3 na kumbukumbu 22:5 na kwamba wachukizao sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kibiriti sawa sawa na Ufunuo 21:8..unaposikia Neno hilo na ukalitii hapo ndipo utafunguliwa na kubarikiwa na Bwana.
Vile vile na machukizo mengine kama kujichua/masturbation, kutazama picha chafu/pornography, kucheza kamari, magemu, kusikiliza miziki ya kidunia, kuzini, kuiba, kupokea rushwa, kusengenya, n.k leo hii ukidhamiria kutubu na kuacha hayo machukizo yote na mengine yanayofanana na hayo ukaamua kumfuata Bwana Yesu… basi hapo ndipo umeweza kuufuta upendo wa Mungu kwako…na utaona jinsi Bwana atakavyokushangaza kwa kusuluhisha matatizo yako yote na zaidi kukupa uzima wa milele. Ila kinyume chake ukikataa kutii hii sauti ya Mungu halafu ukaendelea kuhangaika huku na kule… fahamu kuwa umepishana na Kristo, na ni vigumu kupata suluhisho la matatizo yako huko nje.
Tunaishi katika siku za mwisho.. Bwana Yesu amekaribia kurudi.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.