YATAFAKARI MATESO YA BWANA YESU
Hii neema ya wokovu ambao unapatikana sasa bure, tusidhani yule aliyetuletea hakuingia gharama yoyote kuupata,…haikuwa ni jambo la kutamka tu na kusema niaminini mimi mtaokoka!.
Kristo ilimlazimu aingie gharama ili kukamilisha kitu kinachoitwa WOKOVU. Kwani wokovu ili ipatikane ina kanuni yake, ilimpasa mtu apatikane ambaye atatolewa kama sadaka, na hiyo sadaka ni sadaka isiyo na hatia yoyote…ndipo hapo sasa Kristo alikubali kuacha enzi na mamlaka yote mbinguni..ashukuke hapa duniani, awe hana kitu, aishi kama mwanadamu mwingine yoyote yule, apitie maisha kama ya wanadamu, aumwe wakati mwingine, audhiwe, apitie umaskini, kisha na yeye pia ajaribiwe na shetani, aonekane kama atashinda au la,
Lakini kama tunavyosoma aliyashinda yote kwa muda wa miaka 33 bila kutenda dhambi yoyote ijapokuwa alipitia majaribu yote ya kibinadamu.
Na baada ya hapo sasa, ilimgharimu atoe uhai wake ili aweze sasa kukikamilisha hicho kitu kinachoitwa WOKOVU KWA MWANADAMU…Ndipo hapo Kristo akalazimika aende msalabani akapigwe afe, damu imwagike ili kusudi mimi na wewe tupokee huu wokovu kwa gharama alizoingia.
Sasa leo nataka tuyatafakari mateso ambayo Bwana Yesu aliingia ili mimi na wewe tupate wokovu..ambao unapatikana sasa bure. Wengi wetu tunadhani mateso aliyoyapitia yalikuwa ni ya kawaida tu…hebu leo tafakari kwa kina huku ukitengeneza picha akili mwako juu ya yale mateso ambayo Yesu alipitia…hebu soma hizi vifungu huku ukiwa unatengeneza picha kana kwamba unamwona akifanyiwa hivyo.
Mathayo 26: 65 “Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake;?
66 mwaonaje ninyi? Wakamjibu, wakasema, Imempasa kuuawa.
67 Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makofi, 68 wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?”
Marko 15:16 “Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakukusanya pamoja kikosi kizima.
17 Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;
18 wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! 19 Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia.
20 Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
22 Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.
23 Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane , asiipokee.24 Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini,
25 Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha.
29 Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana,wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, 30 jiponye nafsi yako, ushuke msalabani.
31 Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe.”
Hayo ni machache tu kati ya mengi ambayo Kristo alifanyiwa… mengine hayajaandikwa ila kwa hayo tu…ukitafakari utajua thamani ya wokovu huu ambao watu wengi wanaichezea leo, watu wengi hawajui kuwa wokovu ulipatikana kwa gharama ya Yesu kupitia mateso makali, vinginevyo wokovu tusingewahi kuupata…tungeishia tu kutengwa na Mungu milele.
Ingekuwa sio Yesu kwa upendo wake kukubali kujitoa na kupigwa mijeledi namna ile kama punda, alikubali kupigwa marungu kichwani, alikubali kupigwa makofi na mangumi, alikubali kudhihakiwa na kutemewa mate, alikubali kuchukua msalaba mzito huku akitukanwa na kupigwa bila sababu yoyote, yeye alikubali kuvumilia hayo yote ili mimi na wewe tupate wokovu, yeye hakuthubutu kufungua kinywa chake ijapokuwa alikuwa anao huo uwezo wa kukataa…ila alikubali kuchinjwa kama mwanakondoo ili achukue dhambi za ulimwengu.
Isaya 53:7 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; kama mwana-kondoo apelekwaye machinjioni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.”
Biblia inasema…
Kristo aliharibiwa uso wake na mwili wake, Zaidi ya mwanadamu mwingine aliyewahi kuishi hapa duniani.
Isaya 52:13 “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana.
14 Kama vile wengi walivyokustaajabia, (USO WAKE ULIKUWA UMEHABIRIWA SANA ZAIDI YA MTU YE YOTE, NA UMBO LAKE ZAIDI YA WANADAMU).
Jaribu kuchukua muda utafakari!, chukua muda utafakari hata dakika 20, fikiria huo uso uliwezekanikanaje kuharibiwa zaidi ya mtu yoyote hapa duniani, na mwili wake vivyo hivyo, ndipo utakapofahamu kuwa mapigo aliyopigwa Bwana hayakuwa ya mwanadamu wa kawaida, alikuwa kama nyama buchani, kile unachokifahamu kwenye filamu ni mfano mdogo wa jinsi Bwana alivyokuwa anaonekana, na hiyo yote ilimpasa apitie vinginevyo mimi na wewe tusingeupata wokovu…
Biblia inasema…
“bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, NA KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA.” (Isaya 53:5).
Uso wake na mwili wake usingeharibiwa kwa mapigo mabaya kama yale ambayo mengine hata hayajaandikwa kwenye biblia, mimi na wewe leo hii tusingeufikia uponyaji wa roho zetu. Lakini jiulize wewe ndugu ambaye bado hujamwamini yeye licha ya kwamba amekusogezea wokovu huo bure mbele yako bila malipo yoyote… jiulize, siku ya leo ukifa katika hali yako ya dhambi utawezaje kuokoka na hukumu ya jehanum?
Kumbuka wokovu unapatikana bure, sasa bila gharama yoyote, usisubiri mpaka mlango wa neema ufungwe ndipo uje uutafute, hilo halitawezekana tena, wakati huo ukifika wewe utakuwa ni wa kusubiria tu kwenda jehanum ya moto, lakini leo hii ukiyasalimisha Maisha yako kwake, ukiamua kuacha dhambi zote ikiwemo uasherati, uzinzi, ulevi, anasa, uchawi, rushwa, usengenyaji, uvaaji mbaya na mambo yote mabaya utakuwa umeikwepa hiyo hukumu ya Mungu…Na vile vile licha tu ya kwamba unayo ticket ya kwenda mbinguni, lakini pia ile damu yake ya thamani iliyomwagika pale msalabani wakati huo huo itaanza kukunenea mema juu ya Maisha yako angali ukiwa bado hapa duniani.
Hivyo ndugu tubu kama bado hujafanya hivyo, maadamu bado unayo nafasi..saa ya wokovu ni sasa na sio baadaye maana haujui yatakayotokea kesho.
Jina la Bwana Yesu libarikiwe.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.