
NENO LA MUNGU NI KIOO
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia..
Neno la Mungu wetu linafananishwa na vitu vingi katika biblia, kuna mahali linafananishwa na “Taa” (Zab.119:105)”, sehemu nyingine linafananishwa na Upanga wa roho (Waebrania 4:12, Waefeso 6:17)” Na kuna sehemu linafananishwa na “Kioo”. Na leo tutajifunza ni kwa namna gani linafananishwa na kioo, ili tuelewe tabia nyingine ya Neno la Mungu.
Kama tunavyojua kioo kazi yake ni kuakisi taswira ya kitu. Kwa mfano mtu anapotaka kujijua yupoje kimwonekano, hususani uso wake, hakuna namna anaweza kujua uso wake upoje, bila kutumia kioo. Akitaka kujua uso wake upoje na sehemu gani na gani afanye marekebisho ni lazima atatumia kioo kama yupo peke yake.
Sasa ni kwa namna gani Neno la Mungu linafananishwa na kioo. Hebu tusome mistari ifuatayo..
Yakobo 1:22 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, MTU HUYO NI KAMA MTU ANAYEJIANGALIA USO WAKE KATIKA KIOO.
24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake”
Umeona hapo, mtu ambaye anasikia Neno lakini halitendei kazi, anafafananishwa na mtu anayejiangalia kwenye kioo, kisha akaenda zake na kusahau jinsi alivyo.
Sasa ni kwa namna gani Neno la Mungu linafananishwa na kioo?
Kama tulivyoona kioo kazi yake ni kuakisi taswira ya kitu. Kwa mfano unapojiangalia kwenye kioo chako unajiona jinsi ulivyo, unaona sura yako ilivyo, kama una kasoro utajiona, kwasababu kioo hakidanganyi…kinakuonesha taswira halisi.
Vivyo hivyo Neno la Mungu pia ni kama kioo, unaposoma au kusikia likihubiriwa, Lile ndio KIOO chako!!.. Linakuonyesha kasoro zako!… kasoro ambazo huwezi kuziona kwa macho! Lenyewe linakuonyesha.. Na lengo la kukufumbulia kasoro zako, ni ili ujirekebishe Papo kwa Hapo, na wala si kusubiri kesho au baadaye!.. Hapana bali papo kwa papo. Kwasababu ukisubiria na kusema baadaye au kesho utasahau, mfano wa mtu aliyejiangalia kwenye kioo akajiona kasoro zake halafu akasema ngoja kidogo nitajirekebisha tu. Ni wazi kuwa akishaondoka pale kwenye kioo anajisahau jinsi alivyo… mpaka akipita mahali penye kioo akijiangalia ndivyo atakumbuka kuwa alikuwa hajachana nywele, au hajajipaka mafuta n.k.
Ndivyo ilivyo kwa mtu ambaye anasikia Neno likimuonyesha kasoro zake mbadala ajirekebishe saa hiyo hiyo anapuuzia, na kusema baadaye au kesho, pasipo kujua kuwa akiondoka pale anajisahau kasoro zake.
Na wengine wamefanya wachungaji wao, manabii wao kuwa kioo cha kujitazama. Hivyo wanaposikia Neno la Mungu likihubiriwa na akaona kasoro zake kupitia hilo Neno, wanapinga na kusema kanisa letu haliamini hivyo, au mchungaji wangu amesema hivi na hivi.
Ndugu, ni vizuri leo kufahamu kuwa Neno la Mungu limehakikiwa, halina kasoro yoyote, ni kioo. Mchungaji ana kasoro zake, Nabii, Mtume wana kasoro lakini Neno la Mungu ni kioo. Hivyo ni vizuri utazame NENO zaidi kuliko wanadamu. (Sikuambii usiwasikikize watumishi wa Mungu au viongozi wako wa kiroho lakini sio kila neno ni kupokea tu na kuamini) Angalia Neno la Mungu linakuambiaje;
Mchungaji wako haoni kasoro zako zote lakini Neno la Mungu ni kioo, unaposoma mwenyewe au unaposikia likihubiriwa na watumishi wa Mungu wa kweli.. unajiiona kasoro zako hivyo kubali kurekebishwa na Neno la Mungu…wala usiseme mchungaji wangu amesema.
Kwa mfano unapolisikia au unaposoma hili Neno la Mungu katika 1Timotheo2:9, ambalo linasema..
”Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
[10]bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”
Unapaswa kubadilika kulingana na hili Neno. Kama umesoma leo Neno hili na unaona kabisa kasoro zako, uvaaji wako ni mbaya, unavaa mavazi yasiyositiri mwili wako (vimini, kaptula, magauni ya kubana kiasi kwamba shepu yako inaonekana, matiti yako yanaonekana, makwapa yako yanaonekana, mapaja yako yanaonekana) hayo ni mavazi ya kizinzi hivyo unapaswa kujirekebisha leo leo, muda huu huu baada ya kusoma huu ujumbe.
Wala usiseme mchungaji wangu amesema Mungu haangalii mwili anaangalia moyo tu, hayo ni maneno yake yeye, lakini Neno hili litasimama kukuhukumu siku ile.
Na maneno mengine yote kwenye biblia unapaswa kutii na kufanyia kazi unaposikia au unaposoma. Kama Neno la Mungu limesema mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume na mwanamume asivae mavazi ya mwanamke kwa maana ni machukizo kwa Mungu (kumb.22:5), unapaswa kutii hilo Neno na sio kwenda kuuliza kwa Nabii, Biblia inasema wanawake na wafunike kichwa ibadani (1Wakorintho11), biblia inasema wanawake na wanyamaze kanisani, hawana ruhusa ya kuwafundisha wanaume (1Wakorintho14:34 & 1Timotheo2:12) usiseme Neno hili limeandikwa kwa watu fulani wa kipindi fulani, hapana unapaswa kukubali kurekebishwa kasoro zako.
Biblia imesema “msijipambe kwa nje yaani KUSUKA nywele, kujitia dhahabu (hereni, mikufu, bangili, cheni, n.k)” 1Petro3:3 & 1Timotheo2:9.
Unapaswa kukubali kurekebishwa kasoro zako na KIOO, aondoa mapambo yote katika mwili wako maana ni machukizo kwa Mungu, hereni, vipini, lipustiks, wanja, wigi, mekaups, rangi kwenye kucha, na michoro yote uliyoweka kwenye mwili wako. Kumbuka usipokubali kurekebishwa leo ukapuuzia, mwisho wa siku utajikuta kuzimu, halafu utaonyeshwa katika kioo kubwa kasoro zako, na wakati huo utakumbuka uliwahi kujiona hizo kasoro lakini sasa utakuwa umechelewa.
Hivyo ni heri ukatii leo kabla kioo hakijaondoka machoni pako.
Unanyoa denge/kiduku na mitindo ya kidunia, unacheza kamari/kubeti, unasikiliza miziki ya kidunia na kutazama filamu za kidunia ambazo maudhui yake yamejaa uzinzi, unatazama picha chafu/pornography, Unafanya masturbation/kujichua, unafanya uasherati na uzinzi, unalewa pombe na kutumia madawa ya kulevya kama sigara, mirungi, bangi n.k hebu leo jitazame kasoro zako kisha jirekebishe leo leo.
Kumbuka watu watendao mambo ya jinsi hiyo na yanayofanana na hayo hawataurithi ufalme wa Mungu wasipotubu na kuacha/kubadilika (Wagalatia 5:19-21).
Hichi ni kioo kimewekwa mbele yako!.. kinakuonyesha kasoro zako, ni heri ukazirekebisha sasa, usingoje kesho wala baadaye.
Kama unataka kuzirekebisha sasa, hapo ulipo anguka piga magoti, na kisha kiri mbele za Baba wa mbinguni kuwa umekosa, na tubu kwa kudhamiria kutozifanya tena, kama ulikuwa unafanya uzinzi na uasherati unaachana na mtandao wote uliokuwa unafanya nao uasherati, kama ulikuwa unavaa nguo za kizinzi, unazichoma sasa hivi baada ya toba yako, wala usimpe mtu mwingine na wala usimpe mtu mwingine na wala usizingojeshe kesho, vivyo hivyo na mambo mengine yote..unayaacha kwa vitendo, angali bado kioo kipo mbele yako sasa.
Na baada ya kutubu hivyo, hatua inayofuata ni ya muhimu sana, nayo si nyingine zaidi ya ubatizo!. Ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, Na baada ya kubatizwa Roho Mtakatifu atakusaidia kufanya yaliyosalia, kwasababu tayari wewe utakuwa milki yake halali.
Bwana akubariki na Bwana atusaidie.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.