JIHADHARI NA DHAMBI YA UONGO.

Dhambi No Comments

JIHADHARI NA DHAMBI YA UONGO.

Shalom, karibu tujifunze biblia.

Biblia inasema waongo wote hawataurithi ufalme wa Mungu, bali sehemu yao ni ziwa la moto kama ilivyo kwa wazinzi, wachukizao, waabuduo sanamu n.k

Ufunuo wa Yohana 21:8

Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, NA WAONGO WOTE, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Dhambi hii ya uongo ni dhambi ambayo inachukuliwa na watu wengi kiwepesi sana katika siku hizi za mwisho, kiasi kwamba kusema uongo umekuwa ni jambo la kawaida. Tena teknolojia imerahisisha sana kutendeka kwa dhambi hii KUBWA, ni kawaida mtu kupiga simu au kutuma ujumbe na kusema uongo wasi wasi.

Lakini biblia inasema waongo wote sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti. Kumbuka ni WAONGO WOTE. Hakuna uongo mdogo wala mkubwa..na wala kwa Mungu hakuna kutaniana kwa maana kitakacho kinywani mwa mtu ndivyo yaujazayo moyo wake.

Na jambo lingine la kufahamu ni kuwa uongo sio huu tu ambao wengi tunafahamu, lakini hata kubadilisha muonekano wako jinsi Mungu alivyokuumba ni uongo mbele zake.

Unapobadilisha rangi ya ngozi yako, rangi ya nywele zako, rangi ya kucha zako, rangi ya mdomo wako kwa kuweka rangi ya bandia unakuwa umetenda pia dhambi hii ya uongo. Utauliza kwa namna gani?

Tusome..

Warumi 1:18,21 “Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.

[21]kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.

[22]Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;

[23]wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.

[24]Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.

[25] KWA MAANA WALIBADILI KWELI YA MUNGU KUWA UONGO, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina”.

Unaelewa maana ya uongo?

Uongo maana yake ni kwenda kinyume na kweli, unapobadilisha muonekano wako unakuwa na muonekano wa uongo, unakuwa umeenda kinyume na ukweli halisi.

Ukweli halisi ni kwamba Mungu alikuumba ukiwa na ngozi nyeusi, nywele nyeusi, kope nyeusi, lakini unapojibadilisha unakuwa na ngozi ya uongo, nywele za uongo, kucha za uongo, macho ya uongo, kwa ufupi unakuwa muongo mazima.

Na hivyo huwezi kuwa mtoto wa Mungu kwa namna hiyo kwasababu Mungu ni wa kweli siku zote, hivyo watoto wake pia ni wakweli. Lakini ibilisi yeye ni muongo siku zote na baba wa huo, hivyo watoto wake nao vivyo hivyo.

Je! upo tayari kuendelea kuishi maisha hayo ya uongo? Hebu leo uvue huo uongo na kuvaa kweli ili usiende kutupwa jehanumu ya moto.

Waefeso 4:25 “Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.”

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *