UVUMILIVU WA MUNGU NI NAFASI YA KUOKOKA.

Siku za Mwisho No Comments

UVUMILIVU WA MUNGU NI NAFASI YA KUOKOKA.

Kuna watu wanasema mbona tangu enzi za mababu zetu tunasikia tu kuwa tunaishi katika siku za mwisho lakini ule mwisho mbona haufiki. Hakuna mwisho wa dunia ni habari za kutunga tu!

Lakini biblia inasemaje?

2Petro 3:1 “Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,

[2]mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.

[3]Mkijua kwanza neno hili ya kwamba KATIKA SIKU ZA MWISHO WATAKUJA NA DHIHAKA ZAO WATU WENYE KUDHIHAKI, wafuatao tamaa zao wenyewe,

[4]na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

[5] MAANA HUFUMBA MACHO YAO wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

[6]kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

[7] LAKINI MBINGU ZA SASA NA NCHI ZIMEWEKWA AKIBA KWA MOTO, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.”

Unaona hapo, watu hawa wanafumba macho, walishatabiriwa na sasa tunawashuhudia wakinena maneno ya kumdhihaki Mungu. Maneno kama haya yamesuka katika siku hizi, utasikia mtu anasema “unakuja umekuwa kama Yesu.” Ni maneno mabaya sana ya kumdhihaki Mungu lakini yaliyashatabiriwa.

Ndugu Yangu, fahamu kuwa Yesu hajakawia kurudi ANARUDI UPESI. Lakini kwanini mpaka leo hii imepita miaka mingi hajarudi bado?

Ni kwasababu ananivumilia mimi na wewe tufikilie toba, hataki tupotee katika jehanum ya moto, lakini uvumilivu wake unakikomo.

2Petro 3:9-10 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, BALI HUVUMILIA KWENU, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.

[10]Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

Unaona, Bwana hajakawia kurudi, bali anatuvumilia tutubu.. Ndio maana leo hii unaendelea kuishi vizuri na bado unaishi katika dhambi, japokuwa imepita miaka mingi tangu uliposikia injili, sio kwamba Mungu hakuoni au anafurahishwa na matendo yako bali anakuvumilia ili utubu na umgeukia yeye kwa maana haufurahii kufa kwake mtu mwovu (Ezekieli 18:23).

Lakini huu uvumilivu unakuwa na kikomo, na kikomo kikishafika hakuna nafasi tena ya kutubu haijalishi utalia kwa machozi ya damu. Mungu hatasikia tena Ndio maana biblia inasema baada ya kufa ni hukumu (Waebrania 9:27) na tena anasema mkumbuke Muumba wako kabla roho haijamurudia aliyeitoa (Mhubiri 12:7).

Watu wa kipindi cha Nuhu walihuburiwa na kuonywa kwa muda mrefu wamgeukie Mungu..waache matendo mabaya lakini walikuwa na shingo ngumu wakazidi kutenda maovu na kumdharau Nuhu aliyekuwa anawashuhudia. Lakini siku uvumilivu wa Mungu uliposema basi, ndipo walipofahamu kuwa ule uvumilivu wa Mungu ulikuwa unawavuta ili watubu na waache njia zao mbaya, gharika ilishuka na kuwameza wote.

1Petro 3:18 Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,

[19]ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;

[20]watu wasiotii hapo zamani, UVUMILIVU WA MUNGU ULIPOKUWA UKINGOJA, SIKU ZA NUHU, SAFINA ILIPOKUWA IKITENGENEZWA; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.”

Umeona hapa, inaogopesha kusikia watu hawa sasa wapo kuzimu wanasubiria hukumu ya ziwa la moto. Kristo alishuka huko kwenda kuwahubiria kosa lao walilolifanya mpaka wakajikuta huko.

Na dhambi yao ilikuwa si nyingine Zaidi ya kupuuzia “Uvumilivu wa Mungu” uliokuwa ukilia juu yao siku baada ya siku..

Walipokuwa wanajua kabisa ni kweli dunia inakwenda kuangamizwa lakini wanafanya makusudi kushupaza shingo zao, wakiiona Safina ikijengwa, kwa muda wa miaka yote hiyo, walipokuwa wakihubiriwa na Nuhu kwa muda mrefu sana wa miaka 120 watubu waache dhambi zao lakini wanakataa..Wakimsikia Nuhu akiwaambia Mungu anawapenda, hataki hata mmoja aangamie, lakini wao wanaenda kinyume chake, wanaishi Maisha ya uovu, wanazini makusudi, walewa makusudi, wanafanya uchawi na ushirikina..wanasema huyo Mungu anayesema ataangamiza dunia mbona hatumwoni akiangamiza, kashakufa, wewe Nuhu acha ukichaa, wewe ni mvivu, hutaki kujishughulisha wewe unawaza tu mbinguni, na Maisha mwilini utaishije sasa, umaskini wa akili na ulimbukeni wa kifikra?..

Lakini siku ilipofika uvumilivu wa Mungu uliposema Basiii…Hakusalia hata mmoja..na wote moja kwa moja wakapelekwa katika gereza lao moja mahususi, lililokuwa limetengwa kwa ajili ya watu wa namna hiyo wanaostahili hukumu ya juu Zaidi..Na ndipo huko Kristo alipowafuata kuzimu..

Biblia inatuambia kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa siku za kuja kwake mwana wa Adamu, Siku za Nuhu watu walipuuzia wokovu, japokuwa walielezwa kuwa dunia inakwenda kuteketezwa lakini walitukana..Ndivyo ilivyo leo hii, dalili zote za kuja kwa Kristo zimeshatimia katika karne hii ya 20 na 21,..Na mojawapo ya dalili ya juu kabisa ni kutokea na kuongezeka kwa kasi kwa manabii wa Uongo na makristo wa uongo..mambo ambayo ukimuuliza hata mtu aliyekufa mwaka 90’, atakwambia jambo hilo hatujawahi kuliona wala kulisikia kama limeshawahi kutokea katika historia..Lakini sisi leo hii atakwambia jambo hilo hatujawahi kuliona wala kulisikia kama limeshawahi kutokea katika historia..Lakini sisi leo hii tunalishuhudia kwa macho yetu, lakini badala watu watubu wamgeukie Mungu, ndio kwanza wanatoa maneno ya kudhihaki…huyo Yesu mpaka leo miaka 2000 imepita hajaja amekufa..,mizaha, jina la Kristo linatajwa kiholela holela mpaka kwenye comedy …. wanaudharau uvumilivu wa Mungu…

Moja ya siku hizi, hii dunia itafika mwisho.. Na kibaya Zaidi tumeambiwa mwisho huo utakuja kwa ghafla sana. Hakuna mtu atayetazamia kama kweli huo ndio wakati wenyewe..kwasababu biblia inatuambia utakuja wakati wa amani..sio wakati wa vita..leo hii tunaishi katika hicho kipindi.. Na kama ikitokea umekufa katika hali ya dhambi, ukijua kuwa kila siku umekuwa ukikutana na mahubiri na injili zinazokuhubiria ugeuke lakini hutaki..basi ujue gereza lako litakuwa ni lile la hali ya juu Zaidi kuliko lile la watu wa Nuhu na lile la watu wa sodoma na Gomora.

Ukiona kwanini dunia mpaka dakika hii haijateketezwa, ujue kuwa sio kwamba Mungu anafurahia ulawiti wako, au uzinzi wako, au ulevi wako, au uvaaji vimini vyako, ni kwasababu uvumilivu wake unakungoja utubu, ili usiingie katika adhabu kuu ya siku ile.

Warumi 2:4 ”Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?

[5]Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,

[6]atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;”

Kama bado unasua sua, au upo vuguvugu ni wakati sasa wa kuanza kuyatengeneza mambo yako sawa na Mungu wako..Usijivunie dini au dhehebu,..wakati tuliopo ni wakati wa kuutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu wako. Jiulize je! Ikiwa unyakuo utapita leo nitakuwa na uhakika wa kwenda na Bwana..Je! nikifa leo nitakuwa na uhakika wa kwenda mbinguni, au kuzimu ambapo kuna mateso yasiyoelezeka.

2Petro 3:15 “Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa”;

Uvumilivu wa Mungu ni upendo kwetu.

Ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *