Ni nini unachokiona kwa Yesu?.
Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Je! Yesu Kristo katika maisha yako unamtazama kama nani? Na ni nini unachokiona na kukitaka kwa Yesu Kristo?
Wengi wetu tutasema Yesu Kristo tunamtazama kama Mwokozi, tutasema tunachokiona kwake ni ukombozi,tutasema tunachokiona na tunataka atufanyie nini hapa ndio wengi tunapoteza/kukosa shabaha shabaha.
Ikiwa Yesu leo hii atakutokea na kukwambia unataka nikufanyie nini? Utamjibu nini? Wengi wetu tutasema nataka unibariki,nipate kazi,pesa,nk mambo ambayo si mabaya lakini kama tunamtazama Bwana Yesu katika nyanja kama hizi basi tumekosa shabaha.
Wakristo wanataka/kuona magari na mafanikio,uponyaji nk kwa Yesu Kristo mambo ambayo si mabaya lakini hayatakiwi kabisa kuwa ndio kiini/kitu tunachokiona kwa Yesu Kristo.
Leo hii Wakristo wengi kila siku wanalia wanataka Mungu awabariki awape Familia nzuri,awape kazi nzuri, awapatie fedha nk sio vibaya(tunatakiwa kweli kuomba lakini kumbuka haya ni mengineyo ambayo Mungu atakupa tu, hatutakiwi kuyafanya haya kuwa ndio msingi wa maombi yetu kila siku)lakini kama haya ndio maombi yako ya muda wote nataka nikwambie ndugu uko mbali na ufalme wa Mungu au hujamuelewa vizuri Yesu Kristo.
Sasa tusome kisa kimoja katika maandiko tuelewe tunapaswa kuona nini au kuomba nini kwa Yesu Kristo!?.
Marko 10
46 Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia.
47 Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.
48 Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu.
49 Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita.
50 Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.
51 Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.
52 Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.
Wote tunaifahamu hii habari lakini nataka tuangalie jambo moja hapa kwa kina..
Bartimayo alikuwa kipofu, yeye hajawahi kuona kabisa na hakuwa kipofu tu lakini maandiko yanasema alikuwa ombaomba , maana yake kila mtu aliekuwa anapita pale haijalishi ni nani alikuwa akimuomba ampatie fedha.
Lakini aliposikia habari za Yesu Kristo (huenda aliwahi kusikia sikia mambo ya Bwana Yesu na Bwana Yesu alikuwa mtu maarufu sana anaejulikana)
Bartmayo baada ya kujua kwamba Yesu ndio anaepita siku hiyo hapo alianza kumuita Yesu Mwana wa Daudi unirehemu. Watu walimzuia lakini aliita sana mwisho Yesu akamsikia(si kwamba Yesu hakumsikia mara ya kwanza la! Alisikia lakini aliemdelea kwenda)
Na baada ya Bartmayo kuitwa na Bwana Yesu hapa ndio nataka tupatafakari tupate kitu kitakachotusaidia..
Marko 10:51 “Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini?Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona”
Unaona hapo? Baada ya kuulizwa “ wataka nikufanyie nini?”
Sio kwamba Yesu alikuwa hajui Bartmayo ni kipofu alikua anajua na si kwamba hakuwa anajua akipita njia hiyo atakutana na kipofu, na si kwamba Yesu hakuwa anafahamu jambo analolitaka Bartmayo alikuwa anajua na bado akamuuliza ili kutufundisha sisi jambo.
Maana yake alipewa uwanja mpana wa kuchagua nini Yesu amtendee pale angesema chochote angefanyiwa na Bwana. Lakini majibu ya Bartmayo anasema “… Mwalimu wangu nataka nipate kuona.” unafikiri Bartmayo alikuwa na Pesa nyingi sana ndio maana akahitaji kuona? Kama ni pesa hakuwa nazo ndio maana akawa pale.
Tafakari Bartmayo alikuwa ni ombaomba ndio ilikuwa kazi yake kubwa kwa nini hakujibu “.. Mwalimu wangu nataka Pesa nyingi nikafungue biashara niachane na hii kazi ya kuombaomba” kwa maana nyingine amgeomba mtaji! Lakini anaomba nataka kuona.
Na baada ya kuona maandiko yanasema alipopata kuona ALIMFATA. Aliomgozana na Yesu Kristo kila mahali na katika nyakati zote.
Nini tunajifunza hapa?
Hatuwezi kumfata Yesu Kristo ikiwa bado ni vipofu(yaani kujikana nafsi na kukubali mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha yetu,hatujamfahamu vizuri itakuwa ni ngumu kukubali kuangamia ikiwa huijui vizuri thamani ya Yesu Kristo Yeye ni nani).
Kitu tunachotakiwa kukiomba kila siku kwa Mungu ni sisi kumuona(kumuelewa zaidi Yesu Kristo) ambaye huyo utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya mwili upo katika Yesu Kristo .
Wakolosai 2:9
“Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”
Maombi yako siku zote yaegemee sana kuomba kumjua Yesu Kristo tamani Yesu Kristo ajifunue katika maisha yako.
Kwani ukimuelewa vizuri Yesu Kristo ukamfahamu ndugu yangu hivyo vitu vyote unavyofunga na kuomba kila siku kazi,fedha,Elimu,mke,Mume nk viko ndani yake maana yake ni kwamba vitakufata mahali popote ulipo Haleluya.
Hivyo vitu vingine vyote vitakuja lakini wekeza Muda wako vizuri kumfahamu Mwana wa Mungu. Hekima zote na maarifa yote na kila kitu kizuri vyote viko ndani yake.
Unapomkaribia zaidi Yesu Kristo na kumfahamu milango itaanza kufunguka yenyewe tu huhitaji kulazimisha. Kumbuka kadili unavyozidi kumfahamu Yesu Kristo ndio kadili unavyozidi kuwa nae karibu zaidi na kupata vitu vyake vya ndani zaidi.
Omba maombi haya kwa imani.
“Ee Yesu Kristo ninaomba unifumbue macho yangu nipate kukuona na nikufuate Kama Bartmayo alivyokuona alikufata. Hamu ya kukujua wewe izidi kuongezeka ndani yangu,nipe wepesi wa kukuelewa na kutembea katika njia zako, sihitaji tena nitembee kwa kupapasa papasa(kuwa kipofu rohoni kwa kuona mambo tu ya ulimwenguni hapa bali nilione tumaini la utukufu wako) bali nataka nikujue sana, ninakushukuru Baba yangu kwa kuwa unanipenda,unanijali,unanithamini,na unanisikia yote niombayo ni katika jina la Yesu Kristo Amen.”
Amini hayo umepokea.
Maranatha.
Ubarikiwe.
Mawasiliano:0613079530.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.