TUKAJIONA NAFSI ZETU KUWA KAMA MAPANZI

Biblia kwa kina No Comments

TUKAJIONA NAFSI ZETU KUWA KAMA MAPANZI

Shalom. Jina la Bwana Yesu Kristo libarkiwe. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mungu wetu.

Katika safari yoyote bila shaka huwa kuna milima na mabonde, hakuna tu mteremko kwa wakati wowote, Vivyo hivyo na katika ukristo hakuna mteremko..ni lazima ukutane tu na milima (matatizo) kadha wa kadha.

Ndio maana Bwana wetu Yesu alitangulia kutuambia mapema kuwa ”tujipe moyo” maana ulimwenguni tunayo dhiki lakini tujipe moyo, ikiwa na maana kuna matumaini ya kushinda maana yeye mwenyewe alishinda.

Yohana 16:33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.

Ikiwa wewe ni mkiristo halisi uliyempokea Yesu kweli kweli, ikiwa na maana umeacha dhambi na ulimwengu, ukakubali kumfuata Kristo, basi ujumbe huu utakufariji sana katika safari yako ya wokovu.

Safari yetu ya wokovu inafananishwa na ile safari ya wana wa Israeli..walipotolewa Misri (utumwani) na kupelekwa nchi ya ahadi (kanaani), na sisi vivyo hivyo tunapomwamini Yesu, tunatolewa utumwani (kwenye dhambi) na kupelekwa kwenye kanaani yetu ambayo ni mbinguni (nchi ya maziwa na asali).

Lakini kama tunavyojua wana wa Israeli walipotolewa Misri hawakupelekwa moja kwa moja kanaani, bali walipitishwa jangwani, na safari yao kuelekea kanaani ilianzia huko, ila kama tunavyojua kati ya wale waliotoka Misri ni wawili tu walifika kwenye ile nchi ya ahadi…wengine wote waliishia jangwani. Kwasababu ya kutokumwamini Mungu aliyewatoa kwa mkono hodari huko Misri.

Walipopata taarifa kuwa ile nchi wanayoiendea ina watu hodari sana, majitu makubwa, tena ni nchi inayowala watu, wakaogopa na kuvunjika mioyo..wakaona kwamba biashara yao ndiyo imeisha, hawakuona tena uweza wa Mungu wao wala hawakutafakari maajabu ambayo Bwana Mungu aliwatendea huko nyuma, waliidharau uweza wa Mungu wa mbingu na nchi.

Hesabu 14:2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.

[3]Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

[4]Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.

[5]Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.

[6]Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;

[7]wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.

[8]Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.

[9]Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope.

[10]Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.

[11]BWANA AKAMWULIZA MUSA, JE! WATU HAWA WATANIDHARAU HATA LINI? WASINIAMINI HATA LINI? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.

Leo hii, unaweza ukakukutana na tatizo/kikwazo, ama vitisho ambazo zingekufanya urudi nyuma katika wokovu, lakini nataka nikuambie uweza wa Mungu huwa unaonekana katika udhaifu.

2 Wakorintho 12:9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu…”

Unapokutana na tatizo/jaribu lolote ambalo lingekufanya urudi nyuma, hebu tumia hilo jaribu au hilo tatizo kuona uweza wa Mungu, usiangalie ukubwa wake, we amini kuwa Bwana wa Majeshi ni mkuu kuliko hilo tatizo, adui anaweza akaja kwa vitisho, aidha kwa kukuletea taarifa mbaya na ya kutisha ili kukuogopesha uache imani, lakini kuwa kama Kalebu na Yoshua ambao ni mfano wa bibi arusi wa Kristo, hao walipokutana na hao majitu makubwa hawakuangalia ukubwa wao, waliamini uweza wa Mungu wao.. lakini wale wengine walijiona kuwa kama mapanzi, na bora hata ingekuwa hivyo tu, lakini nao walionekana kweli kama mapanzi..wakasema tumekwisha.

Hesabu 13:27 wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.

[28]Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.

[29]Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.

[30]Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.

[31]Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.

[32]Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.

[33]Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; TUKAJIONA NAFSI ZETU KUWA KAMA MAPANZI; NAO NDIVYO WALIVYOTUONA SISI.

Biblia inatuambia, Bwana wetu Yesu alijaribiwa sawa sawa na sisi, katika mambo yote, lakini hakutenda dhambi wala kutetereka katika imani, Sio kwamba alikuwa mgumu sana kuliko sisi, hapana, yeye mwenyewe alisema..

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.

Kwahiyo majaribu katika safari hii ya wokovu tutakutanayo tu, na wakati wa majaribu usishangae kukutana na mbwa mwitu wakali mbele yako, ambao pengine hapo nyuma hukuwahi kuwaona.., unapitia ugonjwa fulani mbaya, pengine unatarajia kuona faraja katika huo, kinyume chake ndio unaona watu wakikukimbia, wengine wanakusema vibaya, Umekuwa mkristo, ukitazamia familia yako ndio ikufurahie, kinyume chake ndio inakutenga na kukurushia maneno, wengine hawakudhara., Unakataa rushwa kazini, maboss wako ndio wana kuundia visa ufukuzwe kazi n.k.. Mambo kama hayo utakutana nayo kwa namna moja au nyingine.

Lakini pia katika majaribu, huwa tunazungukwa na jeshi kubwa la malaika wa Mungu, lakini shida kubwa inakuja pale tunaposhindwa kuwa na hiyo imani na kuona kuwa tumezungwa na jeshi la mbinguni badala yake tunakimbilia kutafuta msaada na kulia lia, Bwana Yesu yeye hakuogopa wala hakukubali kumkosea Baba yake pale alipokuwa akiletewa yale majaribu kule jangwani, jicho lake halikuona hayo majaribu bali aliona kundi la malaika ambalo lilikiwa likimuhudumia, macho yake yalikuwa yanaona maadui waliomzunguka, lakini roho yake ilikuwa inawaona malaika wa Mungu wamemzunguka wakimuhudumia..kuhakikisha hadhuriki na maadui wake, kuhakikisha hafi, kuhakikisha analivuka lile jaribu haijalishi kuwa yupo katika wakati mgumu kiasi gani, kuhakikisha anapata faraja ya kweli kutoka kwa Mungu.

Hapa ndipo wengi wetu tunaposhindwa kupaona, na matokeo yake majaribu yanatuzidi nguvu mpaka kuiacha imani, au kurudi nyuma. Hilo ndio lililokuwa linataka kumtokea Yule mtumishi wa Elisha, siku ile walipozungukwa na majeshi ya maadui zao, jambo ambalo lilimpelekea  aogope sana na kupaniki, na kulia.. Alipoanza kufikiria jinsi atakavyokwenda kukatwa vipande pande, au jinsi atakavyoondolewa kichwa chake, hilo lilimfanya atamani hata ardhi ipasuke saa ile ile , azame.

Lakini jicho la Elisha lilikuwa linaona mbali zaidi, lilikuwa linaona upande wa pili yupo nani, lilikuwa linaona jeshi la mbinguni lililokuwa pamoja naye, pindi anapopitia majira ya majaribu kama hayo, Ndipo baadaye akamwomba Mungu, amfungue macho yule kijana, akafunguliwa na kuona idadi isiyohesabika ya malaika wa Mungu wakiwa karibu yao wamewazunguka, kwa lengo la kuwahudumia.

2Wafalme 6:15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.

Hizo ndio siri zilizowafanya manabii wote wa kale, kuyashinda majaribu mazito, kwasababu waliacha kuwaangalia maadui zao, wakaliangalia jeshi la Mungu mwenyezi lililo pamoja nao. Vile vile utaona wakati ule walipomkamata Danieli na kwenda kumtupa katika lile tundu la Simba, Danieli hakupeleka mawazo yake  sana kwa wale simba, bali alimuawaza Mungu wa majeshi, akijua kuwa jeshi alilonalo la malaika watakatifu la kumuhudumia yeye ni kubwa sana. Na ndipo alipotupwa tu mule tunduni, wale simba hawakumdhuru, Na baadaye  mfalme alipomuuliza ni nini?, Danieli akamwambia maneno haya

Danieli 6:22 “Mungu wangu AMEMTUMA MALAIKA WAKE, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno”.

Hivyo na wewe pia fahamu kuwa, katikati ya majaribu, wapo malaika wa Mungu kukuhudumia usipatwe na dhara lolote, katikati ya shida zako, mateso yako na magonjwa upo muujiza wa Mungu mkononi mwa malaika zake. Hivyo usiwe na hofu, wala wasiwasi wala uoga.

Subiri tu, utaona mambo ya ajabu. Ni vile tu, Mungu huwa si kila jambo atatufumbua macho yetu  tuone, lakini kama angetaka iwe hivyo uone kila kitu, usingekaa uogope jaribu lolote lililo mbele yako. Hivyo tulia,utahudumiwa kwa namna ya kimbinguni, ondoa tu woga,mtazame Mungu. Acha kufikiria juu ya mateso na dhiki, mfikirie Mungu hilo tu. Utaona kazi za malaika wa Mungu wazi wazi mbele ya macho yako.

Usijione kuwa kama mdudu mbele ya adui wako, we songa mbele ukijua lipo kuna ushindi upande wako, hata kama  utakutana na jitu kubwa kama Goliathi, usiangalie ukubwa wake, kuwa kama Daudi.

Zaburi 20:7 Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu.

Lakini kama hujaokoka! Haijalishi utataja jina la Bwana mara ngapi, au utalia kwa sauti kuu kiasi gani, hapo hakuna msaada, ni haki yako ujione kuwa mpanzi mbele ya adui yako.

Ni heri ukampokea Bwana Yesu leo, ili upate uhakika wa kuendelea mbele hata katika majaribu..kwani lile jeshi la malaika watakatifu watachiliwa wakuzunguke pande zote kuhakikisha unakuwa salama.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *