Je unayadhamini maagizo ya Bwana?
Zipo maagizo ya Bwana ambayo aliagiza kwenye biblia kila mtu aliye wake anapaswa kuzishika na kuzitenda.
Moja ya maagizo hayo ni pamoja na ubatizo wa maji, kushiriki meza yake, kutawazana miguu, kukusanyika kwa pamoja, na mengineyo. Lakini siku ya leo tutaangalia hiyo ya kukusanyika pamoja.
Biblia inasema..
Waebrania 10:25 Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
Kila mkristo aliyeokoka kweli kweli, anapaswa kuidhamini hilo agizo la Bwana la kukusanyika pamoja.
Je! wewe kama mkristo unalitii hilo agizo?
Ipo hatari kubwa ya kukaiidi maagizo kama haya..tukirejea katika Agano la kale, tunasoma kati ya maagizo ambayo Mungu aliyatoa kwa wana wa Israeli ilikuwa ni ile ya kushika pasaka, ambapo kila mwaka mwezi wa kwanza siku ya kumi ya mwezi walipaswa kushika hiyo pasaka. Tunasoma
Mambo ya Walawi 23:4 Sikukuu za BWANA ni hizi, NI MAKUSANYIKO MATAKATIFU, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake.
[5]Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA.
Katika siku hiyo kila mwisraeli alipaswa kuwepo kwenye kusanyiko na kushiriki hiyo pasaka, na iwapo itatokea dharura ambayo itamfanya mtu asiweze kushiriki labda safari, kulikuwa na pasaka nyingine ndogo kwa ajili ya watu kama hao, ambayo ilikuwa ni siku ya 14 ya mwezi unaofuata yaani mwezi wa pili. Hii ni kuonyesha umuhimu wa kushiriki hiyo pasaka. hii ilikuwa ni kwa wale watu tu ambao walikuwa safarini au walikuwa najisi hivyo ikawafanya washindwe kushiriki pasaka ya kwanza.
Lakini watu wengine ambao hawakuwa na sababu yoyote ya msingi, hawakuwa najisi wala safarini halafu hawakushiriki hiyo pasaka, walikuwa wanakatiliwa mbali aidha kwa kuuliwa au kutengwa na kusanyiko kabisa.
Hesabu 9:10 Nena na wana wa Israeli, kuwaambia, Mtu wa kwenu, au wa vizazi vyenu, ye yote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa BWANA;
[11]mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika; watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu;
[12]wasisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake; kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika.
[13] LAKINI MTU ALIYE SAFI, WALA HAKUWA KATIKA SAFARI, NAYE AMEKOSA KUISHIKA PASAKA, MTU HUYO ATAKATILIWA MBALI NA WATU WAKE; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake.
Umeona hapo, madhara ya kutotii maagizo ya Bwana, Leo hii ni rahisi mtu kutoa udhuru wa kutokwenda ibadani pasipo kuwa na sababu ya maana..bila kujua kuwa anajiweka hatiani, mwingine atasema nimechoka, ninaumwa, sijisikii vizuri, sina sadaka, nimeitiwa kazi, nimealikwa mahali, mvua inanyesha nitaenda week ijayo, n.k hayo yote Bwana anatafsiri kuwa ni kudharau na kukaidi agizo lake la kukusanyika kwa pamoja..na mwisho atakukatilia mbali usipoacha kukaidi na kupuuzia maagizo yake.
Ndugu usiruhusu kazi ile muda wa Mungu wako, usiruhusu familia, mihangaiko, mali zitafune muda wa Mungu wako. Wengine wanasema jumapili ndio faida ninapata, ndugu ziache hizo faida zipite, Ni nani kakuambia Mungu hatakupa hizo siku nyingine? epuka udhuru, idhamini agizo la Bwana.
Watu wanaotanguliza mambo yao mbele Zaidi ya Mungu katika kipindi hichi cha siku za mwisho, kwenye Unyakuo, kwenye karamu ya mwanakondoo mbinguni hawataenda.
Agizo la kukusanyika pamoja na watakatifu wenzako ni la muhimu sana kama ilivyo kwa maagizo mengine yote.
Hakikisha kila week hukosi ibadani tena kwa wakati (zingatia muda ulioamriwa), labda itokee sababu ya msingi sana ambayo Bwana mwenywe anaelewa.. vinginevyo unajitafutia laana.
Je! Umempokea Yesu ipasavyo? Je! Unafahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa nyakati na hukumu ya Mungu imekaribia?
Unasubiri nini mpaka dakika hii hujampokea Yesu? Huu ndio wakati wako sasa usiendelee kusubiria maana haujui siku ambao mlango wa neema utafungwa kwako, biblia inasema saa ya wokovu ni sasa na sio kesho.
Hivyo tubu dhambi zako zote umgeukie Kristo kabla hujachelewa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.