AKAMLAZA KIJANA CHINI YA KIJITI KIMOJA.
Jina kuu la Bwana Yesu Kristo mkuu wa mbingu na nchi libarikiwe milele na milele.
Nakukaribisha tujifunze maneno ya uzima ya Bwana Yesu.
Leo tutajifunza jambo moja katika ile habari ya Hajiri Mjakazi wa Sara ambaye tunamsoma katika kitabu cha mwanzo Sura ya 21.
Ili kufupisha hiyo habari, kama we ni msomaji mzuri wa biblia, unafahamu kuwa sara alikuwa tasa kwa muda mrefu..na ikafika kipindi aliona amchukue mjakazi wake (Hajiri) akampa mumewe Ibrahimu alale naye ili ampatie mtoto, na kweli baada ya hapo alipata mtoto kwa huyo Hajiri Mjakazi wake akamuita jina lake Ishimaeli.
Sasa, baada ya Hajiri kupata mtoto, hakuwa tena kama hapo mwanzo, hakuwa tena anajishusha na kuwa mnyenyekevu kama mjakazi mbele ya Sara mwaajiri wake, pengine alianza kujiona kuwa na yeye ni mke mwenza, hivyo akawa anamdhikaki bibi yake Sara, jambo hilo lilimchukiza sana Sara.. ila Bwana alimjalia Sara kupata mtoto katika huo huo uzee wake.
Hivyo baada ya Sara kupata mtoto (Isaka), alianza kumtesa yule Hajiri Mjakazi wake, na akawa hamtaki tena, akamwambia Ibrahimu amfukuze mbali, na baada ya hapo Hajiri kweli akafukuzwa yeye na mwanae Ishmaeli wakaelekea huko jangwani huku akiwa na mkate tu na kidumu cha maji basi..hebu tusome hiyo habari kwa ufupi.
Mwanzo 21:9 Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.
[10]Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.
[11]Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.
[12]Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.
[13]Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
[14]Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.
[15]YALE MAJI YAKAISHA KATIKA KIRIBA, AKAMLAZA KIJANA CHINI YA KIJITI KIMOJA.
[16]Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.
[17] MUNGU AKASIKIA SAUTI YA KIJANA. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, MAANA MUNGU AMESIKIA SAUTI YA KIJANA HUKO ALIKO.
[18]Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.
[19] MUNGU AKAMFUMBUA MACHO, NAYE AKAONA KISIMA CHA MAJI; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.
[20]Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.
Sasa nataka tuangalie huo mstari wa 15, unaosema “… AKAMLAZA KIJANA CHINI YA KIJITI KIMOJA” maana ndipo kiini cha somo letu kilipo.
Kama tunavyosoma, Hajiri baada ya kuishiwa na kila kitu na tena yupo jangwani sehemu kukame hakuna matarajio yoyote, ndipo aliona sasa hakuna namna nyingine ni kutafuta tu mahali pa kumuacha huyu kijana afe mwenyewe nisimuone akifa mbele yangu, ndipo akaona KIJITI KIMOJA akamlaza huko, akamuacha analia, na yeye akaenda kulia mbali.
Na katika kulia huko, ndiko malaika wa Mungu akamtokea na kumwambia Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko, AKAMFUMBUA MACHO AKAONA KISIMA CHA MAJI, akaenda kujaza kiriba chake na kwenda kumpa kijana na kijana akapona.
Sasa nataka tujiulize kabla hatujaangalia siri iliyojificha katika hiyo habari, je! kwanini Mungu asikie sauti ya kulio ya kijana na sio mama yake?
Ni wazi pale kijana alipolazwa, kulikuwa na jambo la kipekee, na jambo hilo sio lingine zaidi ya kile KIJITI ambacho Hajiri aliona tu kuwa ni kijiti cha kawaida, kumbe! kile kijiti kilikuwa kina mahusiano na Mungu na ndio maana sasa kijana alipoachwa analia hapo, sauti yake ikamfikia Mungu kwa wepesi na Mungu akaleta majibu.
Sasa hiyo kijiti kinafunua nini? Hiyo kijiti bila shaka kinafunua MSALABA WA YESU KRISTO. Haleluya
Mwimbaji mmoja wa tenzi za rohoni aliandika hivi “Kama alivyoonyeshwa Yakobo zamani, msalaba umekuwa ngazi ya mbinguni (Tenzi no. 81, ubeti wa 2)”.. akirejea wakati ule Yakobo alipokuwa amelala pale Betheli na akaona maono, ngazi kubwa kutokea mbele yake, na malaika wakikwea na kushuka kutoka mbinguni.
Mwanzo 28:11 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.
12 Akaota ndoto; na tazama, NGAZI IMESIMAMISHWA JUU YA NCHI, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake…..
16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. 17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, NAPO NDIPO LANGO LA MBINGUNI”.
Na ufunuo wa ngazi hiyo ni MSALABA.. Hakika! Kupitia msalaba wa YESU tunafika mbinguni, kupitia ufunuo wa msalaba wa BWANA YESU maishani mwetu, na si shingoni mwetu, au kulalia vijiti, tutamwona MUNGU!..
Hivyo kile kijiti ambayo Hajiri aliona tu ni kijiti kama vijiti vingine, kile kijiti kilikuwa kimebeba siri kubwa ya ufalme wa mbinguni, ukweli ni kwamba vitu vyote vya asili tuonavyo hapa duniani vimebeba siri ya ufalme wa mbinguni, na siri ya ufalme wa Mungu ni YESU KRISTO yeye ndiye siri ya Mungu…na yeye ndiye Mungu mwenyewe aliyekuja kwa umbile la wanadamu kuwaokoa wanadamu..Soma 1Timotheo 3:16.
Sasa ni nini tunajifunza kwa habari hiyo ya Hajiri kumlaza mtoto wake kwenye kile kijiti ambayo kama tulivyoona inafunua msalaba wa Kristo.
Tunachojifunza hapo ni umuhimu wa msalaba wa Yesu katika maisha yetu, kupitia msalaba wa Kristo tunapata uponyaji, kupitia msalaba wa Kristo tunapata uzima, furaha, amani n.k
Leo hii angalia umelaza maisha yako chini ya nini? Je! ni Elimu ya ulimwenguu huu? au ni fedha ambazo zinapotea, au ni wanadamu ambao watakuacha? Pale uwapo jangwani, je! matumaini yako yapo kwa nani? Unapoishiwa, au unapopitia mazingira magumu aidha magonjwa yasiyotibika, au kiu ya kufanikiwa..huwa unajilaza wapi? Na kumlilia nani?
Je ni kwa waganga? au kwa wanadamu? Hajiri alihangaika huku na huku kutafuta msaada, hakupata, na mwisho akaona acha amlaze mtoto wake kwenye kile kijiti..na hatimaye Bwana wa Majeshi alimtokea na kumsaidia.
Pengine wewe leo, mtoto wako ni kazi unayotafuta, au ni ndoa unayotafuta, au mafanikio unayotafuta usiku na mchana, au ni huo ugonjwa ambao umehangaika huku na kule pasipo kuona matumaini. Sasa suluhisho ni kujilaza chini ya msalaba wa Yesu Kristo.
Utauliza utajilazaje? Jibu rahisi ni kwa kumwamini kwanza Yesu na kumfuata kweli kweli kwa kujikana nafsi na kujitwika msalaba wako kila siku. Hapo utakuwa umejilaza kwake na hakika Mungu atasikia tu sauti ya kilio chako kama alivyosikia sauti ya Hajiri baada ya kumlaza mwanae kwenye kile kijiti.
Kumbuka tena msalaba wa Bwana YESU si Rozari shingoni, au sanamu madhahabuni, au mti wa msalaba juu ya kaburi, bali ni ufunuo wa Mauti ya YESU moyoni…Maana yake wokovu unaopatikana kupitia uelewa wa mauti ya BWANA YESU…ambao huo unazaa mtu kujitwika msalaba wake na kumfuata yeye.
Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.
Je! msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako??, Umeubeba msalaba wako na kumfuata yeye??.. Au unajitumainisha na kiriba cha maji na huo mkate ulio nao kwa sasa!..ukiamini kuwa haitaicha, hiyo elimu yako unayotumainia haiwezi kukutatulia kila kitu, haiwezi kukupa uzima, au hiyo kazi yako, cheo chako kinachokupa kiburi kiasi kwamba unaidharau msalaba wa Kristo..hayo yote ni ubatili, Hivyo vyote ukiwa navyo na KRISTO HAYUPO MOYONI MWAKO, UNAFANYA KAZI BURE!!!.
Na tena ni heri ukose hivyo vyote, Ukose elimu, ukose kazi, ukose cheo, ukose kila kitu…lakini msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako, kuliko kuwa na vyote hivyo halafu huna YESU moyoni!!…NI HASARA KUBWA!!!
Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa BWANA YESU leo, kama bado hujafanya hivyo, na BWANA ATAKUSAIDIA, Ikiwa utahitaji msaada huo wa kumpokea YESU, basi waweza wasiliana nasi na utapata msaada huo…
2 Wafalme 6:5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.
[6]Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. AKAKATA KIJITI, akakitupa pale pale, chuma kikaelea.
[7]Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.