Nitajuaje kuwa ninaomba kwa Mungu wa kweli?

Maombi na sala No Comments

Nitajuaje kuwa ninaomba kwa Mungu wa kweli?

Shalom. Jina la Bwana Yesu Kristo mwokozi wa ulimwengu libarikiwe, utukufu na heshima vina yeye milele na milele.

Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Katika somo lililopitia tulijifunza maana ya maombi..kwamba maombi ni nini na ni kwanini tuombe? hivyo siku ya leo tutaangalia ni kwa jinsi gani tunaweza tukawa na uhakika kuwa maombi yetu yanamfikia yule Mungu wa kweli, muumba wa mbingu na nchi… maana ni yeye pekee ndiye tunapaswa tumuombe na si mwingine.

Ni kweli tunaweza tukawa tunaomba, kila mmoja akawa na njia yake au imani yake au namna yake ya kuomba na kumwabudu Mungu, lakini je! tuna uhakika gani kuwa Mungu tunayemwabudu na kupeleka maombi yetu kwake ni yule aliyetuumba.

Ni kweli wewe ni mkristo, au muislamu, au mubadha, au dini yako pengine ni ile inayoamini katika kuomba miti mikubwa, au chochote kile ambacho una imani nayo kuwa kupitia hicho maombi yako na ibada yako yanafika kwa Mungu aliye juu mbinguni ambaye anastahili kuabudiwa peke yake na kila kiumbe.. lakini unauhakika gani kuwa Imani ambayo pengine umerithishwa tu kwa wazazi au umeaminishwa kuwa ni sahihi na ndiyo Mungu anaitambua.. unauhakika gani kuwa ni sahihi?

Ukweli ni kwamba Mungu tunayemwabudu na kuomba kwa njia hizo tunazozijua sisi, sio yule mmoja aliyeumba mbingu na nchi japokuwa sisi tunasema ni mmoja. Na leo tutafahamu ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa na uhakika kuwa Mungu tunayemuomba ni yule anayestahili kuabudiwa.. Mungu wa kweli aliyeumba mbingu na nchi ili tusiendelee kuabudu miungu.

Kwamaana maandiko yanasema iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu lakini mwisho wake ni njia za mauti (Mithali 14:12), tena shetani hujibadilisha kuwa malaika wa nuru ili kuwafanya watu wamuabudu pasipo wao kujua.

Unaweza ukadhani kwasababu wewe ni mkristo na unakesha kuomba na kufunga lakini kumbe unayemuomba si Mungu wa mbingu na nchi, au wewe ni muislamu ukadhani kwasababu unasali sana na kuwa na matendo mema..lakini kumbe unayemwabudu na kumuomba sio yule Mungu wa kweli aliyetuumba, (Sipo hapa kwa ajili ya kukosoa imani fulani au kusifia imani fulani hapana, bali nipo kwa ajili ya kukuelekeza njia sahihi ya Mungu ambayo tunapaswa tuifuate kulingana na ukweli wenyewe)

Sasa swali; nitajuaje kuwa Mungu ninayemwomba ni Mungu wa kweli aliyeniumba na sio shetani?

Jibu: kwanza fahamu kuwa Mungu ni Roho (haonekani kwa macho ya nje), na hivyo tunamwendea na kumuomba kwa imani..tukiamini kuwa anatusikia

Waebrania 11:6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

Sasa ni imani ipi ambayo ni sahihi kuamini na kumwendea yeye kupitia hiyo, maana tumeona kuwa kuna imani nyingi.

Jibu: kwakuwa Mungu ni Roho, basi na sisi tunapaswa tumwabudu yeye na kumuomba katika Roho (katika Roho yake), utanielewa tu vizuri namaanisha nini ninaposema katika Roho yake, hebu tusome haya maandiko kwa utulivu.

Yohana 4:19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

[20]Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

[21]Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, SAA INAKUJA AMBAYO HAMTAMWABUDU BABA KATIKA MLIMA HUU, WALA KULE YERUSALEMU.

[22]Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

[23] LAKINI SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

[24]Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Umeona hapo, maandiko yanasema saa ipo ambayo hatutamwabudu tena Mungu kule mlimani au kule Yerusalemu (hekaluni), anasema saa inakuja, na sasa ipo ambayo WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI kwamaana Mungu ni roho na anawatafuta watu wanaomwabudu na kumuomba katika Roho, na wala sio katika milima tena, au miti, au majengo ya ibada, au watu fulani.. Mungu wa kweli anaabudiwa katika Roho na kweli.

Na tunaposema katika Roho, tunamaanisha katika Roho yake ambaye ni Roho takatifu, na sio roho nyingine, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuwa na Roho wa Mungu ndani yake ili maombi yake na ibada yake iweze kumfikia Mungu vinginevyo maombi yetu yataishia tu hewani au yatakuwa ni kelele mbele zake..haijalishi tunaomba usiku kucha na kulia, haijalishi tutafunga mwaka mzima..kama hatuombi kwa Roho yake, hapo ni sawa tunamuomba mungu asiye na uhai/sanamu.

Kwahiyo imani sahihi ambayo wote tunapaswa tuamini na kuomba kupitia hiyo, ni ile inayoweza kutupa nguvu ya Mungu na tukahisi kabisa ndani yetu hata tunapokuwa kwenye maombi, nguvu ya Mungu ni Roho wa Mungu mwenyewe. Na imani hiyo ndiyo itakayotufikisha mbinguni Mungu aliko.. kwasababu pasipo kuwa na Roho wa Mungu ndani yetu, hatuwezi kumuona Mungu kamwe, haijalishi tunajiona wasafi kiasi gani, haijalishi tunajitahidi kutenda mema kwa namna gani! Mungu ni Roho nao wamwabuduo imewapasa wamwabudu katika Roho na kweli.

Umeona hapo ndugu, Roho wa Mungu ni Roho Mtakatifu mwenyewe, ambaye tunampokea kama zawadi kutoka kwa Mungu pale tunapomwamini YESU KRISTO na kukubali kumfuata. (Yeye ndiye njia ya kweli ya kutufikisha mbinguni), kwamaana kupitia yeye tunapokea Roho wa Mungu bure ambaye anakuja kutusaidia madhaifu yetu katika kuomba, katika kuishi maisha yampendezayo Mungu (anatupa nguvu ya kushinda dhambi), hiyo nguvu hatupati kwa Nabii fulani, au Mtume fulani…tunapata kwa Roho Mtakatifu (Roho wa Mungu) kupitia kumwamini Yesu Kristo ambaye alishuhudiwa kuwa aliishi pasipo kutenda hata dhambi moja na akatoa uhai wake kwa ajili yetu. Haleluya.

Je! Umemwamini Yesu ipasavyo, au umemwamini kwa namna ile ya kidini/kidhehebu.

Ndugu yangu, leo hii unaamini dini yako kuwa ndiyo sahihi, au imani yako ndiyo ya kweli na wakati mwingine unapokea majibu ya maombi yako kupitia hiyo, Lakini leo tambua kuwa pasipo Roho wa Mungu ndani yako..imani yako haikufaidii kitu, haijalishi unaomba na kupokea. (Fahamu kuwa shetani naye anauwezo wa kukupa utakacho ila sio uzima), ni kweli unafanya vizuri kutenda matendo mema, sawa, lakini pasipo Roho wa Mungu..bado wewe sio kitu.

Kwahiyo jibu rahisi la swali letu nitajuaje kuwa Mungu ninayemuomba ni Mungu wa kweli; Ni kwa kuwa na Roho wa Mungu mwenyewe (Roho Mtakatifu)

Hivyo kama mtu hana Roho Mtakatifu basi amekosa kitu kikubwa sana na cha maana sana, ni heri angekosa utajiri wote wa ulimwengu huu au kukosa kila kitu kuliko kumkosa Roho Mtakatifu..kwasababu Biblia imesema katika Warumi 8:9 kuwa “Mtu yeyote asiye na Roho huyo sio wa Mungu”

Je! Umepokea Roho Mtakatifu?…Au bado unaomba tu bila msaada wake? Bado tu unaomba kwa njia zako mwenyewe?..Lakini Utauliza nitampokeaje? Jibu lipo ndani ya Biblia Takatifu katika Mstari ufuatao…

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Fomula ya kumpokea ndiyo hiyo, kutubu kwanza kwa kumaanisha kuacha Maisha ya dhambi kama ulevi, anasa, uasherati, uvutaji sigara, chuki, visasi, utazamaji picha chafu, utukanaji, ulawiti, usagaji, ushoga, ushirikina, uchawi, n.k Kisha ukishatubu kutoka moyoni kabisa na Bwana akiiona Toba yako na Imani yako kuwa ni ya dhati kabisa…ATAKUSAMEHE KABISA! Na baada ya msamaha huo wa Bure utakaoupata hatua inayofuata ni kwenda kutafuta ubatizo sahihi, ambao huo ni wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji na kwa JINA LA YESU KRISTO, Kisha baada ya huo Roho Ataingia ndani yako, Msaidizi wetu ambaye ni Zawadi kutoka kwa Baba, ambayo tumepewa sisi na Watoto wetu na wote tutakaowahubiria kumjua yeye.

Kumbuka Roho Mtakatifu sio dini au dhehebu fulani, ni nguvu ya Mungu…kama tulivyoona unaweza ukawa mtu wa dini sana, au ukawa kwenye dhehebu kubwa, Lakini usiwe na Mungu ndani yako kama huna Roho wake… Kwahiyo ni muhimu sana kuacha udini na udhehebu na kutafuta Roho wa Mungu aje ndani yetu…na njia ya kumkaribisha ni hiyo kama tulivyoona hapo juu. (Kumwamini Yesu, kutubu dhambi na kubatizwa kwa jina lake)

Mungu akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *