Usifungue mlango wa dhambi katika maisha yako.

Dhambi No Comments

 

Usifungue mlango wa dhambi katika maisha yako.

Jina la Mwokozi wetu wetu Yesu Kristo lihimidiwe Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Dhambi ni kitu kinachoweza kukusababishia madhara makubwa sana katika maisha yako ya wakovu( hata kuharibu hatima yako). Na siku zote dhambi huwa inakuja kwa namna ya kawaida sana yaani kukufanya uone hakuna madhara yoyote hata ukifanya.

Na siku zote dhambi huwa inakuja na ushawishi mkubwa kukufanya ukubali na baada ya kukubali utajikuta katika shimo kubwa sana ambalo hutaweza kutoka kirahisi.

Ikiwa umempokea Yesu Kristo na ukapewa nguvu ya kushinda dhambi ndugu endelea mbele usitazame nyuma maana ukinaswa na dhambi itakuwa ngumu sana kutoka itakugharimu sana na inahitajikanguvu ya ziada maandiko yanasema….

2 Petro 2:20
“Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. ”

Mfano tunamuona Kaini ambae dhambi ilianza katika udogo sana kumuonea wivu ndugu yake Habili. Na kilionekana kitendo cha kawaida tu na Mungu alimuonya Kaini juu ya jambo hilo. Lakini alichukulia kawaida tu na kuipa dhambi nafasi katika maisha yake na akajikuta katika hali mbaya.

Mwanzo 4:7
“Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.”

Unaona hapo? Anasema “….. _dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.”

Kitu kingine unaona hapo? Kumbe dhambi inatutamani tena si kidogo bali sana lakini tumepewa nguvu/uwezo wa kuishinda.

Leo dhambi itakuja na ushawishi kwako katika maeneo mbali mbali hasa uliyo dhaifu. Dhambi haikufati katika eneo ulilo imara bali katika eneo ulilo dhaifu.

Ikiwa utaipa nafasi ndugu utakuwa umeingia katika shimo refu sana na itakugharimu sana kutoka.

Leo hii dhambi itakuja na ushawishi mkubwa tu itakwambia “kazini tu mara moja halafu basi hutafanya tena utatubu na Mungu atakusamehe.”  ndugu yangu pindi utakapokubali kufanya hivyo hutaishia mara moja tu itakuwa ni mwendelezo tena hutaishia huyo tu uliezini nae utaenda na kwa mwingine na mwingine.

Au ikiwa katika eneo la kutazama picha za uchi dhambi inaushawishi mkubwa ni Kama wazo tu litakuja na usipolipinga ndugu utakuwa katika hali mbaya sana itakwambia..” angalia mara moja tu leo tu basi halafu hutaangalia tena. Na ukimaliza hapo utafuta kabisa..” ndugu ukitii tu na ukafanya hivyo..

Nataka nikwambie hutaishia kuangalia tu utafikia hatua mpaka utaanza kujichua na hali yako itakuwa ni mbaya zaidi ikiwa ulikuwa unafanya mara moja kwa wiki itafukia hatua kila siku utafanya hivyo.

Vivyo hivyo katika swala la rushwa,wizi nk utajisemea mara moja tu sitafanya tena ndugu kwa kuwa umefungua mlango utakuwa katika hali mbaya sana.

Na siku zote kufungua mlango wa dhambi ni rahisi sana lakini kuufunga ni vigumu mno yaani itakugharimu sana sana.

Na ndugu yangu usidanganyike na dhambi.. itakwambia “ hata ukifanya hivyo hamna madhara utafanya na utatubu maisha yataendelea utamehewa..…”

Ndugu yangu nataka nikwambie kweli Mungu atakusamehe kabisa lakini utalipa kwa hilo kumbuka siku zote unapofanya kitu kina matokeo yake.

Kweli Mungu atakusamehe lakini matokeo ya kile kitu lazima ulichokifanya/matokeo ya dhambi lazima yakupate tu..

Na hapa ndio Wakristo wengi huwa tunachanganya ashukuriwe Yesu Kristo anaetufundisha kila siku kwa Roho wake.

Pale madhara ya dhambi yanapoanza kuonekana wakati mwingine tunasema “ ni pigo kutoka kwa Mungu juu ya kile nilichokifanya Mungu ananiadhibu..” ndugu nataka nikwambie na lifahamu hili wala sio pigo kutoka kwa Mungu bali ni matokeo ya kile ulichokifanya yanaonekana katika maisha yako.

Maana mwanzo ulifanya ukahisi kuwa hakuna madhara yoyote yanaweza kutokea.

Dhambi ina matokeo ikiwa mambo tunayoyafanya mwilini yana matokeo vipi kuhusu rohoni..?

Ikiwa Mungu atakuadhibu basi ni katika namna nyingine kabisa tena ya kuhakikisha anakunyenyekesha na kufanya urudi kwa kujua ukichofanya si sahihi.

Hivyo matokeo ya dhambi tunayatafasiri katika namna isiyo sahihi na kusema ni Mungu anatuadhibu.

Ndugu yangu ikiwa kuna mlango wowote umeufungua ufunge kuanzia wakati huu kataa kutoka ndani yako na dhamiria kabisa kutoka huko..

Dhambi inaudanganyifu sana na inafanya moyo wako kuwa mgumu na uone ni kitu cha kawaida tu..

Waebrania 3:13
“Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.”

Dhambi inaudanganyifu ndio maana Leo hii mambo ambayo biblia imeyakataza ni Dhambi yanaonekana ni kawaida tu.. ikiwemo uzinzi(kuna watu watakaambia ni hali za mwili tu wala sio dhambi maana Yesu Kristo alikuja kutuokoa roho zetu na sio miili..nk) jambo ambalo ni uongo kabisa..

Maandiko yanaweka wazi aziniye na mwanamke hana akili kabisa afanya jambo linaloangamiza nafsi yake.. ulevi, kuvaa nusu uchi makanisani imekuwa ni jambo la kawaida kabisa kitu ambacho si sawa.

Hivyo iepuke dhambi kwa gharama zote. Daudi alianza kumuona Bethsheba mke wa Uria Mhiti akiwa anaoga akavutiwa kumuangalia tu.. akadhani itaishia pale tu..

Lakini dhambi ikaanza kumshawishi ndani yake kutaka kujua taarifa za Bethsheba na akaambiwa ni mke wa Jemedari wake kwa kawaida ilibidi aishie hapo kwa sababu ameshajua ni mke wa Mtu tayari..

Lakini hakuishia kutafuta taarifa tu lakini ataka kuzini nae ijapokuwa alikuwa anajua Bethsheba ni mke wa Uria(unaona jinsi dhambi inavyochukua maumbile tofauti tofauti siku baada ya siku?)

Unaona jinsi ambavyo dhambi inaufanya moyo wa Mtu kuwa mgumu?

Baada ya kuzini nae akajua basi nimeshatimiza haja yangu ilimbidi atulie lakini akaanza kutafuta namna za kufanya ili mimba aliompa Bethsheba ionekane ni ya Uria lakini inashindikana akajikuta anapanga mikakati ya kumuangamiza Uria afe (unafikiri Daudi kipindi anamuona Bethsheba anaoga na baada ya kujua ni mke wa Uria unadhani wazo la kumuua Uria lilikuwepo?)

Ukweli ni kwamba wazo hilo Daudi hakuwa nalo yeye alitaka azini nae tu basi kisha amuache lakini haikuwa hivyo akajikuta anamwaga damu ya mtu isiyokuwa na hatia..

Unaona jinsi dhambi inavyoanza katika uchanga mpaka inakomaa na kuzaa mauti?

Inakupasa uishinde kwa kuomba,kusoma neno na kukataa jambo lolote ambalo ni kinyume na mapenzi ya Mungu na unaona kabisa ni dhambi wala huhitaji kuambiwa na mtu..

Ushawishi unapokuja kataa maana ndani yako umepewa nguvu ya kusema HAPANA, tamka kataa sema “ mimi sio wa huko wala mimi sio huyo mimi ni kiumbe kipya..” songa mbele wala usianze kutafakari sana endelea mbele utashangaa msukumo na ushawishi vinatoweka na utajikuta umeishinda dhambi kwa namna hiyo.

ikiwa ni uzinzi usiuchochee kwa kuchati chati na huyo mtu unaezini nae punguza chatting na kuwa na mipaka katika mazungumzo yanayoamsha tamaa..

Ikiwa mlizini basi geuka leo mwambie tulifanya dhambi na sasa tugeuke. Ule ulikuwa ni ujinga na haitajirudia tena kisha songa mbele..

Toba ni geuko wala sio kulia na kujuta sana bali ni moyo uliokusudia kugeuka hiyo ndio toba ya Kweli kama Daudi hatuoni anarudia tena mpaka siku anakufa na kuletewa msichana mzuri kuliko wote Israeli na umri mdogo alale nae ili amtie joto Daudi hakurudia makosa.

Nimekuombea katika jina la Yesu mlango wowote wa dhambi ambao utaleta uharibifu ufunge kuanzia sasa.

Yesu Kristo akuwezeshe katik haya uliojifuza.

Ubarikiwe sana.

Maranatha.

Mawasiliano:0613079530

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *