Lakini si kama nitakavyo,bali kama utakavyo wewe.

Biblia kwa kina No Comments

 

“Lakini si kama nitakavyo,bali kama utakavyo wewe”

Nakusalimu katika Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Andiko hili tunalipata katika kitabu cha Mathayo 26:39 wakati ambapo Bwana Yesu anakaribia kwenda kusurubiwa.. Sasa katika mstari huu kuna mambo kadhaa ya kujifunza..

Sote tunafahamu kwa kufunuliwa na Roho Mtakatifu Yesu alikuwa Mungu asilimia miamoja na alikuwa mwanadamu pia asimilia miamoja maana yake kila hali tunayoipitia kama wanadamu basi Yesu Kristo nae aliipitia vivyo hivyo.

Sasa Yesu Kristo anasema “…ikiwezekana kikombe hiki(mateso ya Msalaba, ghadhabu ya Mungu juu ya dhambi ambayo Yesu aliibeba msalabani kwa niaba yetu) kimuepuke maana yake alielewa nini atakachokwenda kukutana nacho katika hari ya ubinadamu kabisa(kama unapopata taarifa za kwenda kunyongwa nk)”

Maana yake kama Kuna namna nyingine inaweza kufanyika ukombozi ukapatikana pasipo yeye kwenda msalabani ifanyike. Ila yeye asiende katika mateso yale..

Ijapokuwa alikuwa anajua ameandikiwa hivyo katika torati na manabii lakini anasema kauli kama hiyo unaweza kuona Yesu Kristo alikuwa katika hali gani..!

Sasa jambo ambalo nataka tujifunze hapa ni muhimu sana..

Leo hii Wakristo wengi wanataka mapenzi ya Mungu yatimie katika maisha yao lakini si kama atakavyo Mungu bali kama watakavyo wao .” na hii inafanya Wakristo wengi sana tupishane na Mungu..

Kwa sababu tunataka mapenzi yetu yatimie.. yaani tunataka Mungu atimize mapenzi/matakwa yetu na si matakwa ya Mungu yatimizwe katika maisha yetu. Yaani kwa namna nyingine tunataka Mungu aingie katika matakwa yetu na sio sisi tuingie katika matakwa ya Mungu.

Tunaona utii wa Yesu Kristo kwa Mungu (anamuita Baba kuonyesha mahusiano yake ya Karibu sana na Mungu) hebu tusome…

Mathayo 26:39
“Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”

Yesu alisema jambo hili si kwamba alikuwa anatania la! Lakini ni ombi ambalo aliliomba mara tatu kwa kurudia hivyo hivyo akiwa amejawa na huzuni kubwa sana.. anarudia tena kwa kusema..

Mathayo 26:42
“Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.”

Maandiko yanaendelea kusema tena..

Mathayo 26:44
“Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.”

Unaona hapo!? Ni ombi ambalo hakuliomba mara moja maana yake alikuwa anamaanisha kweli kama Kuna njia nyingine ifanyike..

Lakini haikuwa hivyo..

Tunaona unyenyekevu na utii wa Yesu Kristo kwa Mungu ijapokuwa alitamani iwe hivyo lakini anasema ikiwa haiwezekani mapenzi ya Mungu yatimizwe ikiwa ni yeye kwenda msalabani kuchukua dhambi zetu na iwe hivyo kama Baba yake atakavyo..

Sasa mapenzi ya Mungu hayawezi kutimizwa katika maisha yetu ikiwa hatutakuwa tayari..

Lazima tukubali kufa kwanza ndani yetu juu ya mapenzi yetu na tukubari mapenzi ya Yesu Kristo yawe katika maisha yetu yaani kama alivyo fanya Yesu Kristo (hakuishi kwa ajiri yake bali kwa ajiri ya wengine na sisi vivyo hivyo hatuna budi kuishi kwa ajiri ya wengine na sio kwa ajiri yetu kuwa tayari kufa kwa ajiri yake).

Bwana Yesu anasema ili chembe ya ngano iote ni lazima ife kwanza na oize kisha ichipuke na kuzaa..

Yohana 12:24
“Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.”

Lazima tukubali kufa kabisa kwa habari ya mapenzi/matakwa yetu na kukubali kuishi kwa ajiri ya Kristo maisha yetu yote na hapo ndio andiko linatimia linalosema..

Wagalatia 2:20
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”

Unaona hapo anasema “…. wala si mimi tena,bali Kristo yu hai ndani yangu…

Paulo kusema hivi tayari maisha yake yote na kila kitu alikuwa ameyatoa kwa ajiri ya Kristo. Na sisi vivyo hivyo kama Kristo atasema tuache kitu fulani kwa ajiri yake basi hatutakiwi kusita sita bali tutii, ikiwa Kristo atakwambia fanya hivi na vile kuwa hivi na vile basi tii..

Je? Unaweza kukubali kutokutimiza mapenzi yako na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie katika maisha yako kama Jinsi Mungu atakavyo? Jibu linaweza kuwa ni ndio lakini katika vitendo lisiwezekane kabisa..

Fikiria malengo na mikakati na jinsi unavyotamani kufanya halafu Kristo anakwambia acha vyote fanya hiki utakuwa tayari?

Paulo anasema…

Wafilipi 1:21
“Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.”

Umewahi kutafakari andiko hili? Jinsi gani mtu huyu alikuwa amejitoa kwa ajiri ya Kristo.  Yeye kwake kila kitu aliona ni sawa kwa ajiri ya Yesu Kristo..

Usidhani Paulo hakuwa na mapenzi yake ambayo alikuwa anataka yatimie alikuwa nayo lakini akakubali kuyaweka mapenzi yake chini na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha yake na ndio maana alikuwa tayari hata kufa kwa ajiri ya Yesu Kristo.

Alikubali kupoteza kila kitu kwa ajiri ya Kristo hivyo wewe na mimi tusiogope kupoteza kila kitu kwa ajiri ya Kristo kwa kuwa ameahidi atarejesha mara mia(100) hapa duniani na katika ulimwengu ujao Haleluya..!

Mathayo 19:29
“Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.”

Unaona hapo? Ikiwa umekubali mapenzi yako kuyaweka chini, ya ndugu zako,watoto nk ukaamua kweli kweli mapenzi ya Mungu yatimie katika maisha yako ikiwa utapitia dhiki, nk lakini Kristo ameahidi kukurejeshea mara mia muamini yeye si muongo.

Hubiri injili,omba,kubali kupitia dhiki ikiwa zitakuja lakini usikate tamaa, songa mbele mtumaini yeye atayanyoosha mapito yako.

Pata nafasi ya kuomba sasa Kristo aifanye upya nia yako(uwe na nia ya Kristo ndani yako kuazia sasa akili zako,ufahamu wako,Mtazamo wako uwe kama wa Yesu Kristo) ha hapo utaweza kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yako kwa kufanywa upya..

Simama na maandiko haya.. omba ameahidi na neno lake ni kweli..

Warumi 12:2
“Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Waefeso 4:23
“na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;”

Wakolosai 3:10
“mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.”

Yapo maandiko mengi sana.. huwezi kumuombea mwenzako,wala kanisa nk kwa sababu nia ya Kristo haijaumbika ndani yako vizuri amua leo.

Nimekuombea katika jina la Yesu Kristo mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha yako si kama utakavyo bali kama atakavyo Yeye..

Ubarikiwe sana.

Maranatha.

@Nuru ya Upendo.

Mawasiliano:0613079530

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *