Iepuke injili ya namna hii.

Biblia kwa kina No Comments

Iepuke injili ya namna hii.

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Injili ni habari njema kutoka kwa Mungu kwa watu wote. Yenye lengo au kusudi la kumrejesha mwanadamu katika mpango mkamilifu kwa Mungu.

Wakati fulani nilipokuwa katika kuhubiri(uinjilisti/kuwashuhudia watu).
Nilikutana na dada mmoja ambae hakutaka kabisa kuhubiriwa habari ya toba(geuko) akaanza kunifundisha kuhubiri akitaka nihubiri upendo tu wa Mungu basi, mambo ya dhambi niache kuhubiri nitapoteza watu wengi hawatakuja kanisani…

Hivyo alitamani maneno ya kufarijiwa tu na kusema watu saivi wanataka faraja unowahubiria nihuburi upendo tu wa Mungu Maana ninapohubiri habari ya kugeuka inamchoma. (Nikatafari anachokisema anakielewa? Kwa sababu Injili tu Tayari huo ni upendo wa Mungu)

Lakini nikatafari hata mahali anapoabudu je ni salama? Anafundishwa nini haswa? Kama anaujua upendo wa Mungu kwa nini tena ahubiriwe huo huo?

Katika tafakari Mungu akaniambia “ Ni lazima watu muwaambie ukweli.”

Katika tafakari neno hili likaja..

Isaya 30:10
“wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;”

Kwa nini injili  ya kweli?
injli ya kweli siku zote inamfanya mtu kutubu(kugeuka) kutoka katika njia mbaya na kwenda katika njia amabayo alikusudiwa kuwepo toka awali.

Injili ya kweli ni lazima imchome mtu katika moyo wake na haiishii hapo tu Lakini inamfanya mtu kufanya uamuzi ndani yake aidha kwa kuitii au kutokuitii.

Matendo ya Mitume 2:37
“Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?”

Unaona hapo? Baada ya Petro kuwahubiria walichomwa mioyo yao maana yake walihitaji kugeuka kutoka katika njia waliyokuwepo kwenda katika njia ambayo mitume na Petro walikuwa wakiwahubiria.

Injili ya kweli ni lazima imbadilishe mtu mwenendo wa maisha yake,inamtaka mwamini kila siku kujitwika msalaba wake na kumfata Yesu Kristo kalvari yaani kwenda kuangamizwa kabisa. Injili ya kweli inamtaka/kumfundisha mwamini kuiepuka dhambi na kuishi maisha matakatifu.

Ukisoma katika nyaraka zote za mitume utaona kwa sehemu kubwa wanawaandikia waamini mambo gani wanatakiwa kuyafanya jinsi wanavyotakiws kuishi maisha yanayoendana na kile walichokipokea.

Kwa nini natangulia kusema mambo kama haya? Moja ya ugonjwa unaolitafuna kanisa la mwisho hili(Laodikia) ni injili inayohubiri kwa habari ya kuamini peke yake kisha baada ya hapo mtu anaendelea na maisha yake anayotaka kuishi.

Na kanisa la leo halitaki kusikia injili ya kweli inayotaka watu warlike dhambi na kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu kanisa la leo halitaki kusikia kabisa.

Linataka kusikia habari za kufarijiwa tu (ajabu mpaka makanisa ya kilokole yaliyo kuwa yamesimama vizuri yameanza kutoka katika misingi halisi na neno).

Mafundisho ya jumapili nk yamekuwa ni ya kuwapa faraja tu kwamba Watafanikiwa katika Biashara zao wasikate tamaa Mungu anayaona mateso yao nk. Si kwamba ni mafundisho mabaya lakini sio kiini cha fundisho(si fundisho kuu) la mwamini.

Leo makanisani watu hawafundishwi juu nyakati gani walizipo na inatakiwa waishi kama wale wanawali tano welevu. Bali wimbi kumbwa la Wakristo linaishi katika giza nene kama wale wanawali wato wapumbavu.

Sasa ni injli gani hasa ambayo unatakiwa kuiepuka?

Injili inayokufundisha msamaha wa dhambi peke yake tu. Haikufundishi kwa habari ya badiliko(toba ya kweli) inakufundisha tu umeokolewa tayari umeshapigwa muhuri wa Mungu huwezi kupotea hata ufanye nini.

Hata ukiishi pasipo badiliko wewe utakwenda Mbinguni ndugu yangu epuka injili ya namna hii nk

Injli hii inamhesabia haki mwenye dhambi/ anaeendelea katika dhambi na sio kumhesabia haki mtu alie geuka,  yaani mwenendo mpya .”

Ni injili ya kufarijiana tu kwa watu walioko dhambini amabo wao hawataki kugeuka hata baada ya kuujua ukweli.

Watu wenye kuipinga kweli ya neno la Mungu na kuweka maneno yao.
Watu hawa ni wenye masikio ya utafiti tafiti wanaposikia ukweli wanatafuta walimu wao makundi makundi ili kupata kile wanachotaka kukisikia..

2 Timotheo 4
3 Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;

4 nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.

Hivyo injili inayokufundisha tu msamaha wa dhambi na kukwambia ukishamini basi imetosha huhitaji Kufanya kitu ndugu iepuke kabisa sio injili ya Yesu Kristo hiyo.

Injili ya Yesu Kristo itakufundisha msamaha wa dhambi kweli, itakufundisha badiliko ndani yako na Roho Mtakatifu ataanza kukushuhudia ndani yako juu ya mwenendo wako,  huwezi kuendelea kuishi maisha ya dhambini ni lazima ikutoe huko.

Tumeokolewa kwa neema kweli si kwa matendo lakini hii neema haikupatikana bure bure tu, ilimgharimu Mungu kuingia gharama kubwa hata kusulubiwa msalabani uchi wa mnyama. Hii ikiwa na maana ikiwa kitu kilichomgarimu Mungu gharama kubwa namna hiyo hatuwezi kukichukulia kwa wepesi wepesi.”

Ni lazima kuna gharama sisi tuzilipe tu. “ Kupokea neema ni bure lakini kuishi ndani ya neema ni gharama

Lazima ujitwike msalaba wako, itakulazimu kuacha vyote na kumfata Yesu Kristo, itakugharimu kuacha wakati mwingine familia,mke,mume,kazi nk kwa ajili ya Kristo.

Itakugharimu kubadilisha mfumo mzima wa maisha yako.

Kumbuka mwito wa Yesu Kristo kuwa mwanafuzi wake una gharama (kuokoka) pale  unapookoka maana yake umekubali kufa katika kila eneo la maisha yako na kuruhusu Kristo akuhuishe ndani yako kisha uishi kama atakavyo na si kama utakavyo.

Unapokuwa Mkristo wewe na ulimwengu ni vitu viwili tofauti kabisa. Mwelekeo wa ulimwengu na mwelekeo wako ni tofauti na hatuwezi kwenda mwelekeo sawa..

Na Yeye Kristo ameahidi nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi. Wala sio vigumu kuishi maisha matakatifu.

Mathayo 11

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

Hivyo tafakari ni Injili ya namna gani uliyonayo? Ikiwa haiamini hata unyakuo,siku za mwisho, inakufundisha kustawi tu katika mwili na kukufariji basi ndugu kimbia hapo.

Ubarikiwe sana.
Maranatha

Mawasiliano:0613079530

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *