Wekeza muda wako mwingi katika mambo ya Rohoni.
Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
“Usipoyatendea kazi mambo ya rohoni utayatendea kazi mambo ya mwilini.”
“ Usiposhugulika na mambo ya rohoni utashughulika na mambo ya mwilini.”
“ Usipotembea katika roho utatembea mwilini”
Watoto wa Mungu wengi katika nyakati hizi za Mwisho muda wao mwingi wanauwekeza katika mambo ya mwilini na muda wao mchache sana(uliobakia. Maana hakuna desturi wala nidhamu na mambo ya rohoni..) ndio wanautumia kumtafuta Mungu.
Na ndio maana mambo ya rohoni kwa Wakristo wengi yamekuwa kama mzigo kwao na magumu kwao hiyo yote ni kwa sababu muda wao mwingi wameuweka katika mambo mengine tofauti na ya rohoni.
Leo utakuta Mkristo anamuda mwingi sana wa kukaa kwenye mitandao ya kijamii na kufatilia habari za udaku/umbea(zisizomjenga na kuchati chati tu kwenye magroup na kuunga hoja za wapagani mbaya bala ya kuhubiri injili huko.) zisizojenga roho yake bali zinazobomoa na mwisho wa siku moyoni mwake badala likae neno la Mungu kwa wingi ndani yake lakini vinakaa vituko vya tik tok na habari za watu wa mataifa. Kizazi hiki tuko katika hatari kubwa sana shetani yupo kazini.
Wakristo wengi hawayatafakari tena yaliyo juu bali wanayatafakari zaidi yaliyo chini kuliko ya yale yaliyo juu.
Wakolosai 3
1 Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.2 Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
Unaona hapo katika Mstari wa 2? Paulo aliliona jambo hili katika kanisa waliooshwa kwa damu ya Kristo akilini mwao/mioyoni mwao hawayatafakari yaliyo juu (utajiri na neema zilizo katika Kristo na mpango wa Mungu kwao na kwa ulimwengu wote).
Zaidi sana walikuwa wamewekeza akili zao kutafakari zaidi mambo ya hapa hapa duniani, huenda ni mali,ndoa,nk ambayo ki msingi sio mabaya lakini haitakiwi fahamu na mioyo yetu iwe huko asilimia kubwa.
Leo hii Wakristo wengi hawawezi hata kuomba Mungu awape kuishi maisha matakatifu, hawawezi kuomba Mungu alisimamishe kanisa lisimame imara liupindue ulimwengu kwa watu kuiamini injili(wewe ni moja ya watu wanaotakiwa kuupindua ulimwengu kwa injili) nk
Lakini Mkristo kila anapoingia kuomba hawezi kuwaombea wengine/washirika nk lakini atajiombea mwenyewe afya na biashara yake ikae vizuri.
Haombi hata kujua kusudi la Mungu katika maisha yake. Hawezi kuomba Mungu ampe nguvu kwa ajili ya kusimama katika nafasi yake kwenye mwili wa Kristo (kuliombea kanisa yaani watakatifu) kama ilivyokuwa kwa Epafra yeye alikuwa akiomba ..
Wakolosai 4:12
“Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.”
Unaona hapo? Maandiko yanasema alikuwa anaomba kwa bidii akiomba kanisa likue kiroho kwa kila mmoja mmoja ili watembee vyema katika mapenzi ya Mungu yote na si machache/baadhi..
Kanisa limekosa watu wa namna hii kanisa kila mmoja analia mbele za Mungu maisha yake ya kimwili yawe safi na sio ya rohoni ndugu zangu tunakwenda wapi kama kanisa?.
Bwana Yesu amesema tuutafute kwanza ufalme wake na haki yake hayo mengine tutazidishiwa… Lakini tunatafuta yale tutakayozidishiwa na si ufalme wake ambao ndani yake kuna kila kitu.
Leo Mkristo yuko bize kabisa ufahamu wake kwa asilimia kubwa kauwekeza katika Tamthilia, mipira nk ndugu yangu zinakufaidia nini? Zinakujenga kiroho? Je huo mpira unakujenga kiroho uzidi kutembea katika mapenzi yote ya Mungu?
Au unakubomoa roho yako kwa kutaka timu fulani ifungwe ili ufurahi na uanze kuongea mizaha na kuwatania watu unasahau maandiko yanayosema..
Zaburi 1
1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
Mazungumzo na matusi unayoyasikia yanakuharibu usidanganyewe..
1 Wakorintho 15:33
“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.”
Usidanganyike unaharibika ndugu.. hutajiona kwa sasa ni kama kansa tu itakuja kuonekana na madhara makubwa.
Ndugu haya mambo yanakuharibu hujui tu.. ndio maana kuchelewa ibadani kwako ni jambo la kawaida lakini si jambo la kawaida kuchelewa kwenye mabanda umiza nk kwa sababu kinachochukua nafasi ya kwanza ndicho chenye nguvu na ndio Mungu wako.. unaanza kuzungumzia mechi nayochezwa kesho lakini huwezi kukaa na kutafakari ibada ya kesho itakuwaje ni wapi hapo sawa niombe?.
Ni rahisi kupiga kelele kwa sauti kubwa katika sehemu hizo na kushangilia kwa nguvu kubwa lakini sio rahisi kumshangilia Mungu kwa nguvu kubwa kumsifu Mungu..
Ni rahisi na ni kawaida kusinzia kanisani na sio rahisi kusinzia mpirani nk.
Ndugu yangu haya yote yanatokea huwezi hata kuomba nusu saa kila muda unakimbilia kuangalia muda uishe kwa sababu umewekeza muda wako mwingi katika mambo ya mwilini wewe na tamthilia na taarifa za uombea ni zako.
Ndugu unafikiri hapo utamuelewa Mungu Zaidi? Unadhani utakua kiroho?
Unadhani Kristo atajifunua katika maisha na kukupa hekima na kukushirikisha/kukupa taarifa za mambo yajayo kupitia Roho wake Mtakatifu?.
Haiwezekani wala usidanganyike umeamua kumfata Kristo basi wekeza Muda wako mwingi kwake
Maandiko yanasema…
Wagalatia 5:16
“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.”
Maana yake usipoenenda kwa Roho lazima utazitimiza tamaa za Mwili haiwezekani ukawa katikati na tamaa za mwili ni mauti mwishoni.
Kadiri unavyowekeza mwingi na mambo ya rohoni ndio yanazidi kuwa mepesi kwako na utaanza kuona mambo ya mwilini yanaanza kutoweka yenyewe tu kama ni kiu ya mipira,kufatilia habari za umbea,uzinzi nk vinatoweka.
Wekeza Muda mwingi katika kusoma neno,kusikiliza mahubiri, dumu sana katika kuomba wakati mwingi, washuhudie wengine habari njema wewe mwenyewe utaanza kuona kuna namna unahama katika ulimwengu wa Mwilini na kuingia ulimwengu wa rohoni na utaanza kuona mambo mengi sana na kujifunza.
Ubarikiwe sana.
Maranatha.
Mawasiliano: 0613079530.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.