UVUMILIVU NI NYENZO MUHIMU KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Safari yoyote ya mafanikio aidha mafanikio ya rohoni au ya mwilini inahitaji uvumilivu, bila uvumilivu mafanikio hayaji kiwepesi wepesi kama unavyotaka, hakuna bahati nasibu kwenye mafanikio ni kuwa mvumilivu, wakati mwingine utaona kama hayaji lakini ukiwa mvumilivu hakika utafanikiwa tu, Ibrahimu ambaye tunamjua kama Baba yetu wa Imani alikuwa ni mtu mvumilivu.. usidhani ile imani alipata tu hivi hivi.
Siku moja alikaa kumsubiria Mungu kuanzia asubuhi mpaka giza linaingia hadi akapitiwa na usingizi akiilinda tu sadaka yake, na hatimaye Mungu akamtokea baadaye na kumbariki zile baraka zote ambazo mpaka leo sisi tuliofanyika watoto wake kupitia Mwokozi YESU tunazifaidii.
Mwanzo 15:1 Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.
[2]Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?
[3]Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.
[4]Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.
[5]AKAMLETA NJE, AKASEMA, TAZAMA SASA MBINGUNI, KAZIHESABU NYOTA, KAMA UKIWEZA KUZIHESABU. AKAMWAMBIA, NDIVYO UTAKAVYOKUWA UZAO WAKO.
[6]Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.
[7]Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi.
[8]Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi?
[9]Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.
[10]Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.
[11]HATA TAI WALIPOTUA JUU YA MIZOGA ABRAHAMU AKAWAFUKUZA.
[12]NA JUA LILIPOKUWA LIKICHWA USINGIZI MZITO ULIMSHIKA ABRAHAMU, hofu ya giza kuu ikamwangukia.
[13]BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne.
[17]Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama.
[18]Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,
Umeona hapo, Ibrahimu alivyokuwa mvumilivu, hakukubali kutoka uweponi mwa Mungu kiwepesi wepesi tu, hakukata tamaa kumngoja Bwana, na mwishowe alipokea zile baraka zote, na hata baada ya hapo ilimpasa tena asubirie mpaka ile ahadi ilipokuja kutimia baadaye sana.. kama we ni msomaji wa biblia utafahamu kuwa Ibrahimu alipotokewa na Mungu na kupewa hiyo ahadi kwamba uzao wako utakuwa kama nyota angani, Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka 75 na hakuwa na mtoto aliyemzaa mwenyewe, akaendelea kuvumilia miaka ikaenda, akafikisha miaka 80 hakuna hata dalili ya kuwa na mtoto, akafikisha 85 hakuna, miaka 90 amekuwa mzee sana ndipo anakuja kumpata Izaka.
Je! na sisi tunaweza kuwa wavumilivu namna hiyo? au ingekuwa ni wewe ungemwona Mungu ni muongo.. Ibrahimu hakuona hivyo yeye alikuwa mvumilivu akaipata ile ahadi kama maandiko yanavyotuambia.
Waebrania 6:11 Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho;
[12]ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na UVUMILIVU.
[13]Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake,
[14]akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza.
[15] NA HIVYO KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.
Pia tunaweza tukajifunza kwa mashujaa wengine wa imani kama akina Yusufu, Yusufu akiwa kijana mdogo Mungu alimpa ahadi ya kuwa atakuwa mtu mkubwa na ndugu zake wangekuja kumusujudia. Lakini tunasoma maisha ya Yusufu..aliuzwa utumwani, akakaa gerezani, miaka ikaenda bado yupo na Mungu, na tunafahamu mwisho wake ulikuja kuwaje.. baada ya uvumilivu ule wa muda mrefu.. Yusufu akiwa mtu mzima anakuja kuwa waziri mkuu wa Dola kubwa kipindi hicho , Dola ya Misiri.. hakika ahadi za Mungu hazikawii.
Neno uvumilivu siku zote limekuwa sehemu ya Mungu, na sisi vivyo hivyo tunapaswa liwe sehemu ya maisha yetu, Kama Mungu asingekuwa mvumilivu ni wazi kuwa mimi na wewe tungekuwa tumeshapotea siku nyingi, kwani wakati tu tuliposikia injili kwa mara ya kwanza, siku hiyo hiyo Mungu alitazamia tubadilike lakini wengi wetu tulikuwa wakaidi, ndio tukazidi kuwa watenda dhambi hata zaidi ya hapo mwanzo miezi ikapita, miaka ikapita, japo tulikuwa tunasikia kila siku mahubiri yanahubiriwa lakini hatukuzingatia, Sasa kama ingekuwa Mungu ni mtu wa kukataa tamaa mapema, sio mvumilivu, sidhani kama mpaka leo hii tungekuwa tunaishi,..
Lakini uvumilivu wake, umekuwa neema kwetu na umemzalia matunda si yeye tu, bali sisi pia. Mimi binafsi ninayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuwa mvumilivu kwangu, kwa maana maovu mengi niliyoyafanya huko nyuma nilidhani nilishamkufuru Mungu siku nyingi. Na ni kwanini Mungu anakuwa mvumilivu kwetu?..Jibu ni ili kutuvuta tufikie TOBA halisi.
Warumi 2:4 “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?”
Zaburi 86: 15 “Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli”
Vivyo hivyo na sisi tulio katika imani, Uvumilivu ni moja ya nguzo muhimu sana. Katika mbio hizi zilizo mbele yetu, japo tumewekewa thawabu kubwa huko mwisho mwa safari lakini ukweli ni kwamba milima na mabonde ya ibilisi hayakwepeki, majaribu na masumbufu, na wakati mwingine dhiki tutakutana nazo hapa duniani, na Bwana Yesu alishatueleza kabisa kuwa mambo hayo tutakutana nayo wala hakutuficha,(Yohana 16:33)..Hivyo ni safari inayohitaji uvumilivu.
Je! Umeokoka kweli kweli? Au umeokoka kwa namna ile ya kidini.
Kumbuka uvumilivu tunaouzungumizia hapa, ni ule unaolenga mtu aliyeokoka kweli kweli, ambaye anaishi maisha ya utakatifu, asiye na hofu ya majini, au kifo.
Maana kuna mwingine anaweza akawa labda anapitia matatizo yake binafsi, labda uchumi wake umeyumba, au amekumbana na matatizo ya kifamilia, au magonjwa n.k..na huku nyuma hata hana habari na Mungu, sasa mtu wa namna hii, anaweza akatiwa moyo kibinadamu awe mvumilivu katika hali ngumu anayoipitia kwa huo muda..Lakini huo sio uvumilivu unaozungumziwa katika maandiko.
Uvumilivu unaozungumziwa ni uvumilivu unaolenga Imani. Yaani kutokukatishwa tamaa na hali unayopitia sasa hivi ambayo inaweza kukusababishia kupoteza thawabu yako uliyoandaliwa mwisho wa safari..kwamfano wakati mwingine unaweza ukaona unapitia katika hali Fulani ngumu ambayo sababu yake tu ni uliamua kutokukifanya hicho kitu ambacho ni kinyume na mapenzi ya Mungu, unaweza ukawa unatengwa au unachukiwa kwasababu tu umeacha kufanya dhambi, mwanzoni ulikuwa unakunywa pombe na marafiki zako lakini sasa hunywi tena, mwanzoni ulikuwa unakwenda disco lakini sasa huendi tena, mwanzoni ulikuwa msengenyaji lakini sasa husengenyi tena, na matokeo yake kumetokea kundi la watu wanakutengenezea visa tu, wanakuwekea vikwazo,wanakusema vibaya..wakati mwingine ndugu, hata kazini kwako n.k.
Hapo ndipo unapopaswa uvumilie, biblia inasema katika Mhubiri 7: 8 “Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
Pasipo uvumilivu hatuwezi kumzaliwa Mungu matunda..Kama vile Bwana alivyotoa ule mfano wa mpanzi, akasema mbegu nyingine ziliangukia pembezoni mwa barabara nyingine zikaangukia kwenye miamba nyingine zikaangukia kwenye miiba,..nyingine kwenye udongo mzuri, hapo Bwana alikuwa anafunua aina tatu ya vipingamizi mtu atakavyokutana navyo kabla ya kuufikia mwisho mzuri wa safari yake, awali ya yote shetani atataka kumpokonya kile alichokisikia, itafika tena wakati ataudhiwa kwa ajili ya hilo Neno aliloendelea kulishika, baadaye tena baadhi ya mambo yatataka kumsonga asizae, na shughuli za ulimwengu huu na anasa, na tamaa ya mambo mengi …
Lakini Yule ambaye atazaa 30, mwingine 60 mwingine 100 Biblia inasema, hakuifikia hiyo hatua hivi hivi tu, bali aliifikia kwa KUVUMILIA vipingamizi vyote
Luka 8:11 “Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.
12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.
13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga.
14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.
15 Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda KWA KUVUMILIA.’’
Hivyo ndugu, tunapaswa tuilinde Imani Mungu aliyotupa mara moja tu, Na hiyo tutailinda kwa kuvumilia mabaya yote shetani atakayojaribu kutulea mbele yetu yatakayotufanya tuuache wokovu au turudi nyuma….Iwe ni magonjwa, iwe shida ya fedha, iwe ni kukosa mavazi, iwe ni kuwa yatima, iwe ni kuwa mjane, iwe ni kuwa tasa, iwe ni kupigwa au kutengwa au wakati mwingine kufungwa, vyovyote vile yasitufanye sisi kukosa uvumilivu wa kuyaongojea tuliyoandaliwa mbele. Tuige mfano wa Ibrahimu.
Ufunuo 2:3 “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.”
Dumu katika utakatifu na kuomba, huku ukimgojea Bwana kwa uvumilivu..hakika Mungu hatakusahau kabisa..ipo siku utamwoma akikuinua katika huduma yako au hata katika maisha yako ya kawaida haijalishi leo haoni matumaini, hata Ibrahimu na Yusufu walikuwa ni wanadamu kama sisi ila walivumilia mwishoye wakafanikiwa sana..kikubwa anachotaka Mungu ni uaminifu, tuwe waaminifu na wavumilivu..tutamwona Mungu hakika.
Lakini wewe ambaye bado hujaokoka, fahamu kuwa hakuna matumaini nje ya wokovu, ni heri ukampokea Bwana YESU leo ili uweze kushiriki baraka za Mungu.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.