Shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo tu!

Uncategorized No Comments

Shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo tu!

Ayubu 20:4 Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi,

[5]Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu?

Jambo ambalo watu wengi huwa hawajui ni kwamba uhai ni zawadi toka kwa Mungu, hivyo kwa kuwa hawajui hilo…badala wamshukuru Mungu kwa uzima waliopewa na kutafuta kufanya mapenzi yake, kinyume chake ndio wanadhihaki na kudiriki hata kumtukana Mungu huku wakishangilia mioyoni mwao kwa anasa na starehe za kila namna.

Na kwasababu ya kiburi cha uzima walichonacho hawafikirii wala hawatafakari kuwa uzima walio nao ni zawadi tu toka kwa Mungu na muda wowote Mungu anaweza akachukua.

Hawajui kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo tu, na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu!

Hawajui kuwa kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. (Mithali 1:32). Na tena..

Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi ni kwa kusudi waangamizwe milele.” (Zaburi 92:7).

Ndugu yangu, muda uliyonayo ya kuishi hapa duniani ni mfupi kulinganisha na miaka utakayoenda kuitumikia jehanum, hiyo furaha uliyonayo sasa ambayo dunia inakupatia, fahamu kabisa kuwa ni ya kitambo kidogo tu kulinganisha na mateso utakayoenda kukutanayo huko uendako  usipotubu na kumgeukia Bwana Yesu. Maandiko yanasema…

Mhubiri 11:8 Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Mambo yajayo ni ubatili.

9 Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.

Ikiwa leo unaruka-ruka kwa shangwe ya kutazama mambo ambayo hayana utukufu mbele za Mungu kama hizo mipira, miziki ya kidunia, movies zenye maudhui ya uasherati, na kutazama picha chafu (pornography), au unafurahia kujichua, kujisaga, kucheza magemu, kamari, kubashiri(kubeti), na mambo yote ambayo hayatokani na Mungu bali yanatokana na dunia.. nataka nikuambie usijidanganye kuwa ni kujiburudisha tu,

Hebu jiulize hayo mambo yanakuongezea nini kwenye roho yako kama si kukuweka mbali na Mungu, hiyo shangwe unayopata kwenye mambo ya kidunia unadhani inampendeza Mungu kama siyo inamtia wivu, leo amua kubadilika ndugu yangu, kumbuka hiyo shangwe ambayo dunia inakupatia, hiyo shangwe unayopata kwenye maisha ya dhambi… fahamu kuwa ni ya muda kidogo tu, kumbuka ziwa la moto lipo.

1Yohana 2:15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17 Na dunia inapita, pomoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.

Tafuta kufanya mapenzi ya Mungu (utakatifu), acha kiburi ya uzima.

Hiyo shangwe uliyonayo sasa kwenye dhambi ni kwasababu una afya njema, unapumua bure, unakula na kunywa unachotaka, una elimu kubwa, una pesa nyingi, n.k, hayo ndiyo yanakupa kiburi cha uzima. Ukasahau kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu!

Hujui siku wala saa ambayo utatoa hesabu ya mambo yote.

Salimisha nafsi yako kwa Kristo akuokoe na ziwa la moto, kumbuka alisema..

Marko 8:9 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

Fahamu pia ghadhabu ya Mungu ipo karibu, Bwana Yesu amekaribia kurudi.

Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Kumbuka..

Kwa Yesu lipo tumaini la uzima wa milele, Kwa Yesu Unapata utulivu wa nafasi na faraja. Alisema.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Kwa Yesu zipo Baraka, Na kwa Yesu upo msahama wa kweli:

Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.

Kwa hiyo unapokuja leo hii kwa kumaanisha, ujue kuwa hiyo mizigo ya dhambi uliyonayo haijalishi ni mingi kiasi gani ataitua mara moja, haijalishi uliuwa watu wengi namna gani, haijalishi ulizini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, haijalishi ulikwenda kwa waganga mara nyingi namna gani..Ikiwa tu upo tayari leo kumkaribisha Yesu moyoni mwako basi ataitua, na kukusamehe kabisa kana kwamba hakuna chochote ulichowahi kumkosea..Na atakupa amani.

Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..

Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..

Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Hongera kwa kuokoka.

Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namna hizi hapa chini..+255 789001312

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *