JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA

Uncategorized No Comments

 

JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA

Ndugu yangu ni vizuri kufahamu kuwa hii dunia tayari imeshatamkiwa hukumu, na hakuna maombi yoyote yanayoweza kuifuta hukumu ya huu ulimwengu. Yaliyotamkwa na kuandikwa yatatimia kama yalivyo..

Hivyo kilichobaki kwetu ni sisi kuondoka na kujiokoa nafsi zetu, na katika safari yetu, hatupaswi kurejea/kutazama nyuma..tunapaswa tukazane kuzidi kusonga mbele, kwasababu nyuma yetu, moto unazidi kusogea huku tuendako, hivyo tunakaza mwendo.

Kutazama nyuma ni kitendo cha kupiga hatua kabisa kuurudia ulimwengu.. ulikuwa umeshaushinda uzinzi lakini sasa umeurudia, ulikuwa umeshaishinda pombe na ulevi, na utukanaji, ulikuwa umeshaanza kumtumikia Mungu, lakini sasa umeacha, ulikuwa umeshaacha mambo yote ya ulimwengu, ikiwemo uvaaji mbaya, na kujipodoa..lakini sasa umerejea nyuma, umeanza kuyafanya hayo tena na zaidi ya hayo. Na biblia inasema mtu anayerejea nyuma baada ya kuokoka ni sawa na mbwa aliyerudia matapishi yake au nguruwe aliyeoshwa akarudi kugaa-gaa matopeni.

2Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

[21]Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.

[22]Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.

Lutu na familia yake walipookolewa na hukumu ya Sodoma, waliambiwa wakimbilie mlimani waiponye nafsi zao wasitazame nyuma, lakini mbele tunaona mke wa Lutu alijiharibia mwenyewe kwa kutazama nyuma.

Mwanzo 19: 15 “Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu.

16 Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi Bwana alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji.

17 Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea.

[26]Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.

Ikiwa Mungu ametuokoa kwa neema yake bure akatuweka sehemu salama mbali na dunia, ni wajibu wa kila mmoja kuuthamini wokovu ule kwa kukimbia mbali zaidi na dhambi kama ilivyokuwa kwa Lutu na watoto wake..Ikiwa tulishaona mkono wa Mungu ulivyotuepua kutoka katika dhambi, hatupaswi kujilegeza tena, kusubiria tena neema itutoe kwenye dhambi tunazozitenda kwa uzembe wetu.. Tukishafikia hii hatua ni wakati wa kuziponya nafsi zetu…

Mke wa Lutu ambaye ni mfano wa wale waliookolewa ambao mioyo yao bado ipo ulimwenguni, yeye alipogeuka nyuma alibadilika na kuwa nguzo ya chumvi.

Hata sisi leo hii, ikiwa Bwana Yesu alishatuokoa, halafu tunauchezea wokovu wetu, leo tunaenda mbele, kesho tunarudi nyuma…hatuthamini ondoleo la dhambi tulilopewa siku ile tulipotubu bure, ..na wema wake wote Mungu aliotutenda, hatuoni kama kuokolewa kule ni jambo la bahati sana ambapo sio watu ulimwenguni wanaweza kupewa neema hiyo badala yake mguu mmoja kwa Kristo na mguu mwingine kwa shetani, Tujue tu tupo hatarini kuwa MAWE YA CHUMVI katika roho..

Wokovu sio jambo la kujaribu, na ndio maana biblia inatuambia..

Wafilipi 2:12 “………..utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

2 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.

Ikiwa ni wewe mmojawapo ndugu yangu unayesoma haya, na ndani yako bado kuna kanuru kadogo ambacho kanakaribia kuzima… basi usikubali izime kabisa…ni vizuri ukatubu kwa kumaanisha kabisa mbele za Mungu sasahivi, na kuacha kwa moyo wako wote mambo maovu yote unayoyafanya kwa vitendo, na kumfuata Kristo, neema hii bado ipo juu yako na ndio maana unasikia ndani yako kuhukumiwa unaposoma haya,….huyo ni Roho Mtakatifu anakuvuta kwake tena, anza kugeuka na kupiga hatua mbele, usipoitii hiyo sauti itafika kipindi hutaisikia tena ndani yako, utakuwa ukipita mahali na kukutana na maneno kama haya utaishia kudhihaki na kukejeli, lakini sasa kuna hofu ndani yako kiasi kwamba unaogopa hata kusema neno lolote la kejeli, hiyo hofu ni ya thamani na ya muhimu sana, na ndio inayokuvuta utubu,

Hivyo Tubu leo acha kwenda disko, acha ulevi, mrudie mke/mume wako, acha wizi, acha rushwa, acha kila aina ya dhambi unayoifanya maishani mwako na wala usigeuke nyuma kama mke wa lutu..…hizi ni siku za mwisho..Siku yoyote unyakuo unapita, na hii dunia inakwenda kuwa jivu, Maisha yatasimama…kilichosalia kwako sasa ni nini kama sio kuyasalimika maisha yako kwa Bwana Yesu ayaokoe, naye atakupokea kwasababu anakupenda na kukuhurumia…dini yako ya kiislamu haitakupeleka popote, dini ya kikristo haitakupeleka popote, dhehebu lako mashuhuri halitakupeleka popote bali YESU KRISTO pekee ndiye atakayekupeleka sehemu salama.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *