Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu..
Kwa Neema za Bwana tutakwenda kuangazia ni namna gani tunaweza kujua njia ya wokovu kupitia kitabu cha warumi..
Pengine ulishawahi kukisoma,au ni msomaji wa kitabu hicho ila leo tutajifunza jambo lingine ambalo hukuwahi kulifahamu.. njia ya wokovu ndani ya kitabu cha warumi ni mpango wa wokovu kwa mwanadamu uliowekwa vema,au kuainishwa Katika mtiririko Katika kitabu hicho..
Kama utakuwa ni msomaji wa kitabu hichi basi kitakupa wigo mpana wa kuelewa ni namna gani mpango wa Mungu alivyoweka wa mtu kupokea wokovu, kwasababu ni kitabu kilichoainisha baadhi ya vifungu vinavyoweza kumsaidia mtu kuupokea wokovu kamili..
Ukiachana mbali tu na hilo,pia kitabu hichi kinakupa uelewa mzuri wa jinsi gani unaweza kwenda kushuhudia, kuhubiri injili kwa wengine waupate wokovu, kupitia kitabu cha warumi kinakupa mwongozo huo,
Embu tuungalie ndani yake…
Vifungu hivi ni vifungu bora vitakavyokusaidia wewe wakati wa kushuhudia..
KIFUNGU CHA KWANZA
Warumi 3:23
[23]kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
Hili ni jambo la kwanza analopaswa kufahamu unayemshuhudia,kwamba sisi sote tumetenda dhambi,tumepungukiwa na utukufu wa Mungu, hakuna aliyemsafi na aliyempendeza Mungu,hakuna Mwanadamu aliye mwema Katika hii dunia, hivyo tunauhitaji msaada ya Mungu wa kutuokoa kwenye dhambi..
KIFUNGU CHA PILI
Warumi 6:23
[23]Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Kifungu hichi kinatuonyesha kuwa dhambi inamatokea mabaya zaidi pale ambapo tutaukataa mpango wa kiMungu wa kutuokoa, mwisho wa dhambi inatupelekea kwenye umauti na ziwa la moto, hivyo huna budi kumshuhudia kuwa mwisho wa kudumu kwenye dhambi matokeo yake ni kifo…
KIFUNGU CHA TATU
Warumi 5:8
[8]Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.
Kwa kifungu hichi unaanza kumpa matumaini kwamba pamoja na kwamba tulikuwa wenye dhambi lakini pendo la Mungu lilituletea wokovu mkuu kwa kifo cha YESU KRISTO pale msalabani,, yeye ndiye aliyezichukua dhambi zetu ili tupate uzima wa milele, kwasababu sisi wenyewe tulishindwa kumpendeza Mungu, Bwana Yesu ndiye aliyechukua maovu yetu kwa kupigwa kwake sisi tumepona…
ukishamaliza hapo sasa utakuwa umeshaanza kumpa ufahamu mwingine, hivyo kifungu kifuatavyo ni namna ya kupokea wokovu..
KIFUNGU CHA NNE
Warumi 10:9-10
[9]Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
[10]Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
Wewe kama muhubiri muelezee kuwa ni namna gani tunaweza kuupokea wokovu, ni kitendo cha kumwamini tu Yesu Kristo, kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako,na kukiri kwa kinywa chako mwenyewe, hapo msamaha wa dhambi unaupokea bila malipo, muelezee kusamehewa dhambi hakutokani na matendo ya mtu, asijisifu kwa chochote, ni kuikubali kazi ya Yesu Kristo aliyoifanya pale msalabani,ndio inayotupa sisi msahama wa dhambi
Hakikika kama muhubiri vifungu hivi vinakaa kwenye akili yako ili kuwe na wepesi na umakini wakati wa kushuhudia
KIFUNGU CHA TANO
Warumi 5:1
[1]Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Mfundishe pia baada ya kumwamini Yesu Kristo lazima awe na Amani ndani yake kuwa amesamehewa dhambi zake na hakuna hukumu yoyote juu yake, kwa kufanya hivyo utakuwa umemjenga Katika kiini cha kwanza cha wokovu.
Na huu ndio mtiririko wa jinsi ya upatikanaji wa wokovu ambao umeainishwa Katika kitabu hichi cha warumi, hivyo baada ya hapo unaanza kumfundisha jinsi anatakiwa aukamilishe Wokovu kwa tendo la ubatizo sahihi ili apokee Roho Mtakatifu azidi kudumu Katika Imani,
Mungu akubariki
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.