JIBU,
1Wakorintho 1:25 “Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu’’
Unaweza ukawa umeshajiuliza haya maswali, Je Mungu ni mpumbavu? Mungu wetu ana udhaifu? Mtu yoyote aliyeumbwa ma Mungu akapewa akili na uwezo wa kutambua mambo mbalimbali ambayo Mungu amefanya kama vile kuumba sayari, nyota, milima, mabonde na vingine vingi kamwe hawezi kusema Mungu ni mpumbavu au hata kudhani Mungu ni mdhaifu…
Basi biblia ina maana gani kusema upumbavu wa Mungu?Hii inatokana na mitazamo yetu sisi wenyewe, unapofanya jambo unaona upo sahihi lakini si watu wote wataona hivyo kuna ambao watakuona mpumbavu hata kama kile ufanyacho kipo sahihi. Ndivyo ilivyo hata kwa baadhi ya watu, wanaujua vizuri uwezo wa Mungu lakini bado wanadharau mambo anayofanya…
Ukisoma mistari iliyotangulia utaona wayahudi walitegemea kumuona Mungu katika ishara kubwa mfano wa zile za wakati wa Musa na Eliya, lakini haikuwa hivyo walipomuona walimuona wa kawaida sana hakutoka familia ya kitajiri, ni masikini tena anaishia kufa kifo cha aibu kwa kutundikwa msalabani wakamdharau wakasema mtu kama yeye hawezi kuwa masihi. Wayunani (watu wa mataifa mengine) nao walitegemea kuona ni mtu wa hekima ya kidunia ambayo ingebadilisha maisha yao kwenda viwango vingine lakini walimsikia akisema’Msisumbukie maisha, watafakarini ndege hawapandi wala hawavuni’ nao pia walimpuuzia wakaona hawezi kuabadilisha chochote kwao..,
1Wakoritho 1:22 “Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;
23 bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi;
24 bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.
25 Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu”
Watu wote waliona habari za Yesu hazina maana, kuna wasiomjua walimpuuzia na hata wale walokuwa washika dini waliona hana maana yoyote, kuna wakati Yesu aliwaambia makutano (HERI MTU YULE ASIYECHUKIZWA NA MIMI, Mathayo 11:6)Wayahudi na wayunani hawakutambua kuwa ndiye Masihi mwanzilishi wa kila kitu lakini kama wagelijua wasingethubutu kumsulubisha Bwana wa utukufu….
1Wakorintho 2:7 “bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;
8 ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;
Ni kama vile mtu asiyejua thamani ya Almasi akakutana nayo akaidharau na kuitupa kama mawe mengine asijue kuwa kuna wapo watu hawalioni jua wala mwezi yaan hawauoni usiku wala mchana kwa mda mrefu wakiwa ndani ya mashimo wakiitafuta bila kukata tamaa kwa sababu wanajua hata kipande kidogo tu kitabadilisha maisha yao, mfano mtanzania mmoja ambaye hakupata elimu alipata Almasi yenye thamani ya Bilioni tatu pesa ambayo wakurugenzi 10 na mameneja 10 wanaitafuta mpaka kustaafu kwao na hawawezi kuipata…
Mungu wetu ameificha Almasi yake (YESU KRISTO) na watu wengi hawaitambui thamani yake, leo hii mtu anayeamua kuokoka anaonekana kama amekosa mwelekeo tena kapungukiwa na akili au mtu anayetafuta kumjua Mungu kwa kusoma neno lake watu wanamuona mpumbavu na mvivu asiyetaka kufanya kazi…
Hawatambui kuwa mtu huyo kadri anavyozidi kumjua Kristo ndivyo anavyozidi kuwa mbali na jinsi wao wanavyomfikiria kwa sababu yeye yupo kwenye chanzo cha yote ambayo wengine wanayasumbukia kila siku. Tambua kuwa hakuna mtu aliyejuta baada ya kumjua Mungu, binafsi sijawahi kuona jambo hili hata mfalme Daudi hakuliona..
Ndo mana anasema,
Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.”
Na hapa bado hatujauona vizuri utukufu wake, tukifika mbinguni ndo tutapata majibu kwa nini anaitwa Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme na wamfuatao wanaitwa makuhani wake uzao mteule watu wa milki ya Mungu. Ikiwa leo hii humtaki Yesu aliyekufia msalabani na kukupa uzima ulionao unakimbilia vitu visivyokupa uzima unavihangaikia unasahau ipo siku utakufa na havitakuhifadhi, kumbuka neno hili maana litatimia kwako (1 Wakorintho 1:18 Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”
Mrudie Bwana Yesu anakupenda, usikatae wito wake yeye ni HEKIMA YA MUNGU ambayo wanadamu wanaidharau lakini ni LULU YA THAMANI mbele ya Mungu, akakupenda kwa pendo ambalo hakuna mtu mwingine yeyote anayekupenda hivyo..
Bwana akubariki..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.