Shalom, karibu tujifunze neno la Mungu ambalo ndilo mwanga wa njia zetu na taa ya miguu yetu (Zaburi 119:105)
Ni muhimu sana kutoa sadaka, kwa kulitambua hilo shetani anatumia njia tofauti tofauti ili kuzuia watu wasitoe sadaka maana anatambua nguvu iliyo ndani ya sadaka..
Njia mojawapo anayotumia ni kuinua watu ambao wanalitumia vibaya neno la Mungu, watu hao huwalazimisha watu kutoa au kuwatapeli na wakati mwingine kuwaambia uongo kwa kujificha nyuma ya maandiko.
Mtu ambaye hajakomaa katika imani akiyagundua hayo anaghairi kabisa kutoa sadaka sehemu yoyote maana anaamini atatapeliwa, hapo shetani anakuwa amefanikiwa kumzuia mtu huyo kutoa sadaka.
Lakini yatupasa kujua sadaka ina nguvu, yeyote aliyemwamini Kristo anatakiwa kuwa mtoaji ili milango ya baraka ifunguke kwa ajili yake lakini pia kuzuia mambo mabaya katika maisha yake.
Sadaka ina faida nyingi tena muhimu lakini leo tutaangalia faida mojawapo ambayo ni ‘kuharibu nguvu ya madhabahu za shetani‘.
Ni kweli kuwa maombi yana nguvu ya kuharibu madhabahu lakini wakati mwingine inahitajika sadaka juu ya jambo hilo. Tuangalie habari za Gideoni
Waamuzi 6:25 ”kawa usiku uo huo Bwana akamwambia, MTWAE NG’OMBE WA BABA YAKO, yaani ng’ombe wa pili, wa miaka saba, UKAIANGUSHE MADHABAHU YA BAALI, aliyo nayo baba yako, UKAIKATE ASHERA ile iliyo karibu nayo;
26 UKAMJENGEE BWANA, MUNGU WAKO, MADHABAHU juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; UKAMTWAE YULE NG’OMBE WA PILI NA KUMTOA AWE SADAKA YA KUTEKETEZWA, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata”
Mungu alimuagiza Gideoni kufuata hatua nne ambazo zinatupa funzo kubwa sana.
1.MTWAE MG’OMBE WA BABA
Kwa nini Gedioni anaambiwa amchukue ng’ombe wa baba yake? Kwa sababu madhabahu ya baali haikumuachia baba yake tena ilikuwa na nguvu sana hata kuitawala nyumba yote ya baba yake. Hii inatufundisha kabla hatujashughulika na madhabahu za mababa yatupasa kutafuta sadaka kwa ajili yao ambazo zinawagusa wao moja kwa moja,mfano sadaka ya Gideoni ilitoka kwa baba yake.
2.UKAIANGUSHE MADHABAHU YA BAALI
Gideoni alipoitwaa ile ng’ombe alitakiwa kuiangusha madhabahu ya baali na ashera iliyokuwa imemshikilia baba yake kwa kuipondaponda isisalie kitu hata kidogo. Sisi pia tukishachukua sadaka tunaiendea madhabahu kwa damu ya Yesu kwa njia ya maombi ili tuivunje,
tena ikiwa ni madhabahu inayoonekana kwa macho basi iondolewe kabsa, mfano miti iliyopandwa kwa ajili ya ibada unatakiwa kuikata isiote tena, au mazindiko yaliyowekwa juu ya nyumba nayo pia unayaondoa bila kuogopa ikibidi usimwambie mtu fanya mwenyewe kama alivyofanya Gideoni, ukiwashirikisha watu wanaweza wasikuelewe na pengine mkaingia katika ugomvi.
Kama Gideoni angemwambia baba yake kuwa anataka kuivunja madhabahu ya baali basi ni hakika baba yake asingekubali maana ilikuwa imemshika na yeye aliiogopa ile miungu. Leo hii wanaoziabudu madhabahu za mababu wanaziogopa hivyo sio rahisi wao kukubali ziondolewe, hivyo wewe binafsi inakupasa uwe na moyo wa ujasiri uziondoe maana itakuwa msaada kwao na baadae watamshukuru Mungu kwa ajili yako
3.UKAMJENGEE BWANA MADHABAHU
Gideoni alipomaliza kuivunja ile madhabahu mahali pale pale aliijenga madhabahu ya Bwana. Sisi pia tukimaliza kuziondoa hizo madhabahu tunatakiwa kulisimamisha jina la Yesu mahali hapo hapo kwa kuanzisha ibaada au kanisa.
Watu wengi wakimaliza maombi ya kuvunja madhabahu hawafanyi mwendelezo na kitu ambacho ni hatari sana. Ni lazima jina la Bwana litajwe mahali hapo ili hizo madhabahu za adui zisiinuke tena ikiwa ni nyumbani basi ibaada na maombi yanatakiwa kufanyika asubuhi na jioni na watu waendelee kujifunza neno la Mungu. Tusiishie kuomba na kuondoka.
4.UKAMTOE NG’OMBE KUWA SADAKA
Gideoni alipomaliza kuijenga madhabahu ya Bwana akamtoa sadaka yule ng’ombe wa baba yake na ile madhabahu ya baali ikaishiwa nguvu na kumwachia baba yake na hata aliposikia madhabahu ya baali imevunjwa na mtoto wake hakuogopa kwa sababu roho ya woga ilkuwa imemuachia tayari na Gideoni mwenyewe alikuwa amefunguliwa. Na kisha Gideoni akaanza kuwa shujaa.
Sisi pia tunapomaliza kuvunja madhabahu tunatakiwa kutumia ile sadaka kujenga kanisa au kuimarisha ibaada sehemu hiyo kama ni fedha basi zitumike kununua bibilia au vitabu vya nyimbo na ikiwa mtu ametoa sadaka ya kiwanja basi kanisa lijengwe ili ibaada ziendelee mahali hapo..
Ikiwa mahali hapo huwezi kufika kwa urahisi pengine sababu ya umbali basi toa sadaka yako katika madhabahu nyingine kwasababu majibu ya sadaka yako itakuwa ni yale yale, Kumbuka Jambo hili, usiwe mwombaji bila KUTOA, TOA
Ubarikiwe
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.