Swali: je! Sadaka ya kutikiswa inayoongelewa katika agano la kale ilikuwaje? na je! bado ipo katika agano jipya.
Jina la Bwana Yesu Kristo Mkuu wa uzima libarikiwe daima.. Karibu tujifunze biblia (Neno la Mungu) lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu(Zab119:105)
Tukisoma katika Agano la kale Mungu aliamuru zitolewe sadaka mbali mbali, kwa mfano ilikuwepo sadaka ya Amani, sadaka ya dhambi, sadaka ya kuinuliwa, pia ilikuwepo sadaka ya kutikiswa na nyingine nyingi. Siku ya leo tutaitazama moja ya sadaka hizi ambayo ni sadaka ya kutikiswa na maana yake katika ulimwengu wa roho.
Jambo la kwanza ambalo linapaswa tulielewe ni kuwa katika Agano la kale shughuli zote ndani ya nyumba ya Mungu ilifanywa na makuhani pekee ikiwemo hiyo ya kupokea sadaka ambazo watu walimtolea Mungu. Baadhi ya sadaka zilizotolewa zilitoka kwa wanyama kama ng’ombe, kondoo, mbuzi, na pia nyingine ni baadhi ya ndege kama njiwa, kuku, na vilevile nafaka za mazao mbali mbali kama ngano,n.k,
Iwapo mtu alileta sadaka yake ya mnyama kama kondoo, kuhani alipokea na kumchinja huyo kondoo na ile damu itakayomwagika ndiyo itakuwa dhamana ya dhambi kwa huyo mtu..na baada ya hapo kuhani atachukua baadhi ya viungo na kuvichoma juu ya madhabahu ndani ya Hema au hekalu mbele za Bwana, na sehemu ya nyama iliyobakia ambayo haijachomwa, huyo kuhani alichukua kama mshahara wake yeye na familia yake ndivyo Mungu alivyoruhusu, Hiyo kazi ilifanywa na makuhani pekee na walikuwepo wengi.. kwahiyo walikuwa wanabadilishana zamu kwa zamu.
Pia na sadaka nyingine kama ya unga, sheria ni hiyo hiyo, kiasi kidogo ilichukuliwa na kuchomwa juu ya madhabahu mbele za Bwana na kiasi kingine kilichobakia ilitumiwa na makuhani kama sehemu yao… utaratibu huo ndio uliotumika katika Agano la kale kwa sadaka zote ambazo wana wa Israeli walitoa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi zao.
Sasa tukija kwenye sadaka ya Kutikiswa yenyewe ilikuwa ni tofauti kidogo, ilikuwa ni kwamba baada ya kuhani kupokea (labda inaweza ikawa ni mnyama au nafaka) alichukua kwanza sehemu ndogo ya sadaka hiyo na kuinyanyua juu na kisha KUIPUNGA HEWANI MBELE ZA BWANA, kwa mfumo wa KUITIKISA TIKISA, Kisha baada ya hapo ataishusha chini, na kuendelea na hatua nyingine za kutekekeza baadhi ya viungo juu ya madhabahu, na sehemu iliyobakia ni riziki yao.
Hivyo sadaka ya kutikishwa ilihusisha aina zote za sadaka, yaani za Wanyama, ndege pamoja na Nafaka. Sasa tuelewe pia sio kila sadaka wana wa Israeli walizokuwa wanazileta zilitikiswa namna hiyo mbele za Mungu, la! Bali ni baadhi tu!.
Soma…
Walawi 7:28 “Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
29 Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa Bwana, atamletea Bwana matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani;
30 mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa SADAKA YA KUTIKISWA MBELE YA BWANA.
31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe.
32 Mguu wa nyuma wa upande wa kuume mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka katika hizo sadaka zenu za amani.
33 Katika wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kuume kuwa sehemu yake.
34 Kwa maana, HICHO KIDARI CHA KUTIKISWA, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli.”.
Maandiko mengine yanayozungumzia aina hii ya sadaka ya kutikiswa ni Kutoka 29:27,Walawi 8:27, Walawi 9:21, Walawi 10:14, Hesabu 6:20, Hesabu 8:11, na Hesabu 8:18.
Je! sadaka kama hiyo inatufundisha nini Katika agano jipya?.
Lipo kusudi la Mungu kuruhusu baadhi za sadaka zitolewe kwa njia ya kawaida na nyingine zitolewe kwa njia hiyo ya kunyanyuliwa juu na kutikiswa tikiswa, (yaani kuipungia hewani)
Mungu alilenga kutufundisha kuwa na sisi hatuna budi kuzitofautisha sadaka zetu, kwa mfano sadaka ya kumpa Mungu shukrani kwa mambo makuu aliyokutendea katika mwaka mzima, au mwezi mzima, au namna alivyokuokoa na kukuepusha na majaribu mbali mbali ni lazima iwe tofauti na sadaka unazomtolea kila siku..hiyo ya shukrani ni lazima iwe ya kiwango cha juu kidogo, na uitangaze mbele zake, kwasababu ya matendo makuu aliyokufanyia, ni lazima iambatane na kuinyanyua mikono yako juu na kumsifu, na kumtukuza, na kumshukuru kwa nyimbo za shukurani.
Sadaka kama hii inakubalika na inampendeza Mungu.
Bwana Yesu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Nimebarikiwa sana na elimu ya biblia mnayoitoa mbarikiwe na Bwana
Amina utukufu kwa Mungu ubarikiwe zaidi ndugu yetu, pia unaweza kufikiwa na mafundisho haya Kila siku kwa njia ya Whatsapp yako karibu sana