Sadaka za unga na kinywaji zilitumikaje,

Maswali ya Biblia No Comments

SWALI,

Naomba kufahamu sadaka za unga na kinywaji zilitumikaje, na zina ufunuo gani kwa kizazi chetu,

JIBU:

katika biblia enzi za agano la kale Mungu aliagiza zitolewe sadaka mbali mbali, na ilikuwa ni lazima hizo sadaka zifikishwe madhabahuni pake, maana ili sadaka iitwe sadaka ni lazima ipelekwe madhabahuni. Ikitolewa nje na madhabahu haiwi tena sadaka bali inaitwa mchango, au zawadi, au msaada. Lakini chochote kinachotolewa na kufikishwa mbele ya madhabahu ya Mungu, hicho kinaitwa sadaka.

Sasa katika nyakati za agano la kale, Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wamtolee sadaka kadha wa kadha na kila mtu alipaswa kutoa kwa hiari yake mwenyewe, pasipo kulazimishwa,

Tusome katika….

Kutoka 35: 4 “Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema,

5 Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; MTU AWAYE YOTE ALIYE NA MOYO WA KUPENDA, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba”

Hapo tunaona Bwana anasema..“kila mwenye moyo wa kupenda” na sio kulazimishwa.. Maana yake kama mtu hajajisikia moyoni mwake kumtolea Mungu, basi halazimishwi, lakini atakuwa amejipunguzia Baraka zake kutoka kwa Mungu.

Na sadaka ambazo zilikuwa zinatolewa na wana wa Israeli zilikuwa zinatoka kwenye vyanzo au katika vitu mbali mbali..mfano zilikuwepo sadaka zilizotoka kwa wanyama, kama vile Ng’ombe, Mbuzi, kondoo, na Njiwa, wanyama hawa walikuwa wanaletwa kwenye nyumba ya Bwana, na kuchinjwa, na kisha damu yao kutumika kufanya upatanisho, na baadhi ya viungo vya miili yao kuteketezwa juu ya madhabahu, na sehemu ya nyama iliyobakia isiyoteketezwa juu ya madhabahu, walikuwa wanapewa makuhani, pamoja na watoto wao..

Ila pia zilikuwepo sadaka za vyakula.. Ambapo watu walikuwa wanaleta nafaka zao kama sadaka kwa Mungu, Ndio hapo tunaona sadaka za Unga na sadaka za vinywaji. Na katika makundi yote hayo ya sadaka, yote yalitolewa fungu la kumi, na malimbuko.

Sasa sadaka za unga, zilihusisha unga (wa ngano au shayiri) uliosagwa vizuri, na kisha kupelekwa kwenye madhabahu, huo unaweza kuwa kilo kadhaa, au au pungufu kidogo, na mtu akishaupeleka, Kuhani anachukua kiwango kidogo cha huo unga, na kuuchanganya na ubani, na kisha kuuchoma huo unga pamoja na ubani ule..Na kiwango kingine cha unga kilichobakia kisichochomwa (ambacho kinakuwa ni kingi) wanapewa makuhani, kama riziki yao,

Soma…

Walawi 2:1 “Na mtu atakapomtolea Bwana matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake;

2 kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana;

3 na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto”.

 

Na kama mtu atapenda asilete unga, bali alete unga uliokadwa tayari na kuokwa (Yaani mkate kamili), basi yalikuwepo maagizo ya jinsi ya kuuandaa huo unga (mkate), na kuuleta madhabahuni.. kwamba huo unga uliokandwa na kuokwa haupaswi kuwekwa hamira wala asali. (Walawi 2:4-11).

Vifungu vingine inayozungumzia sadaka hiyo ya unga ni pamoja na Kutoka 29:40-41, Kutoka 30:9, Kutoka 40:29, Walawi 5:13, Walawi 6:15, Walawi 9:17, Walawi 14:10.

Pia mbali na hiyo sadaka ya unga, ilikuwepo pia sadaka ya kinywaji ambayo ilikuwa inaambatana na hii ya unga, Isipokuwa katika sadaka ya kinywaji kilichokuwa kinatolewa ni Divai, (Kwasababu ndio kinywaji kilichokuwa cha gharama na heshima, kwa enzi hizo, na kwa tamaduni za kiyahudi), Na Divai haikutumika kwa matumizi ya ulevi, wala anasa, kama ilivyo leo, bali kwa matumizi matakatifu. (Kutoka 29:41)

Je sadaka ya unga na kinywani ilifunua nini katika agano jipya?

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji (Divai) zinafananishwa na mwili na damu ya Yesu. Kristo aliutoa mwili wake na damu yake kama sadaka, kwa ajili yetu..Na Mungu aliruhusu watu wamtolee sadaka hiyo ya unga na ya kinywaji katika agano la kale, kufunua mwili wa Yesu na damu yake katika agano jipya. Na pia aliruhusu makuhani wa agano la kale washiriki sehemu ya sadaka hiyo, kufunua “ushirika wa meza ya Bwana” kwa makuhani wa agano jipya.

Mathayo 26:26 “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.

27 Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;

28 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”

Kwahiyo kama vile kama makuhani walivyoshiriki sehemu ya unga(mkate) na sehemu ya divai iliyokuwa inaletwa madhabahuni, vivyo hivyo na sisi pia tunashiriki mwili na damu ya Yesu, ili tuwe na sehemu katika madhabahu ya Bwana, kwa sababu wote tuliompokea Bwana Yesu ni makuhani wa Bwana.

 Ufunuo 1:5 tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

6 NA KUTUFANYA KUWA UFALME, NA MAKUHANI KWA MUNGU, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una yeye hata milele na milele. Amina.”

 

Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kushiriki meza ya Bwana, kwa kila aliyemwamini Bwana Yesu, na kuishi sawa sawa na Neno lake.

Yohana 6:53 “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu, na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywani cha kweli.”

Kama hujajua namma ya kushiriki meza ya Bwana na ungetamani kujua..basi unaweza kututumia ujumbe inbox na tutakutumia somo linalohusu “kushiriki meza ya Bwana ” kwa urefu,

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *