
ILE SIKU KUU IMEKARIBIA
Siku kuu ni siku ambayo ni KUU kuliko siku zingine, ni siku ambayo ni maalumu kwa ajili ya tukio fulani la kipekee sana.. mfano siku ya harusi huitwa siku kuu, siku ya maadhimisho ya jambo fulani la kipekee lililowahi kutokea nyuma huitwa siku kuu,
Halikadhalika kuna siku moja inayokuja huko mbeleni… ambayo ni siku kuu sana kuwahi kutokea katika historia ya mwanadamu.
Siku hiyo itaitwa tarehe Fulani ya Mwezi Fulani na mwaka Fulani, siku hiyo ndio siku ambayo watakatifu watamwona Mtakatifu wa watakatifu YESU KRISTO kwa mara ya kwanza. Ni siku ya shangwe kuu na furaha ya ajabu mno.
Siku hiyo ya tarehe Fulani, na mwezi Fulani na mwaka Fulani, Tutaisikia Parapanda ya Mungu.. Parapanda hiyo haitamuhusu kila mtu, hapana, bali kwa wale ambao walikuwa wanaingojea kwa subira,..siku hiyo pengine itakuwa ni asubuhi kwa upande wako, wakati jua linachomoza mapema kabisa na ndege wanalia kwenye viota vyao, pengine utakuwa unakwenda kupiga mswaki, ujiandae kwenda kanisani, ghafla, utaanza kuona mabadiliko ya tofauti angani, utaanza kusikia sauti nzuri za parapanda, ikitokea mbali sana, pengine utajiuliza jambo hili ni nini? Wakati unaendelea kushangaa shangaa hivyo, ghafla utaona makaburi mengi yanafunguka, na wafu wengi wanafufuka, utawaona unaowajua na usio wajua..
Wakati huo utakuwa unajiuliza labda unaona maono au nini.. kwasababu utakuwa ni wewe tu peke yako ndio unayeyaona hayo yote, hakuna mwingine yoyote atakayeyaona..Saa hiyo hiyo utakuwa unawaona wale wafu nao wanakuja kukufuata kwa furaha, wanakuambia..Hii ndio ile siku tuliyokuwa tunaisubiria, kwa kipindi kirefu, kwa miaka mingi sasa imetimia..
Na wakati mnafikiria hayo, kwa mshangao mkubwa wa furaha isiyo na kifani, Mtaona juu mbinguni jeshi la malaika wengi, linatokea likiambatana na Bwana, (Bwana wetu Yesu)..na ghafla muda huo huo mnaanza kuona miili yenu inabadilishwa na kuwa miili mingine ya kimbinguni, inameta meta na ya utukufu, na bila kupoteza muda mnaanza kunyanyuka mnaiacha ardhi kwa mara ya kwanza, mnaanza kwenda juu kwa kasi sana, kumkaribia YESU mwenyewe Mfalme wa wafalme,..
Kisha wote tunakutana naye pale juu akitungojea kwa tabasamu la upendo wa ajabu, embu fikiria utakuwa na furaha kiasi gani, unamwona kwa mara ya kwanza Yesu uliyekuwa unamsubiria kwa miaka mingi, uso wake unauona uliyekuwa unatamani kuuona.. ndio hili neno litatimia.
Isaya 25:9 “Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake”.
Kumbuka kitendo cha wewe kuyashuhudia hayo yote, kwa watu wengine huku duniani kitakuwa ni kitendo cha kufumba na kufumbua..watashangaa tu haupo, umetoweka. Hawatasikia parapanda wala hawataona makaburi yakifunguka.
Na kwa jinsi watu watakaonyakuliwa watakavyokuwa ni wachache, hata ulimwengu hautasadiki habari hizo, watasema tu wamepotea watu kadhaa, lakini watapatikana, hivyo watu wataendelea na shughuli zao kama kawaida, wakingojea dhiki kuu ya mpinga-Kristo.
“Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA BWANA; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya BWANA vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. (Zekaria 14:20).
Siku hiyo baada ya kunyakuliwa juu mbinguni, tutaingia kwa mara ya kwanza mbinguni…huku tukiwa na miili ya utukufu na maelfu ya malaika watatupokea. Na baada ya hapo tutakaribishwa kwenye ile karamu kuu..ambayo BWANA YESU alituandalia kwa miaka mingi…hiyo ndio siku kuu, Ni siku ambayo hapana nyingine inayofananayo.
Tukose mengine yote, tusiikose siku kuu ya Bwana, tusikose kuingia katika raha hii ya ajabu.
Waebrania 4:1 Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.
Kumbuka siku hiyo imekaribia mno. Hakuna kingine tunachokingojea sasa isipokuwa ni hii siku kuu tu ya Bwana (siku ya unyakuo).
Dalili zote zimekwisha timia, moja ya siku hizi parapanda italia na watakatifu watanyakuliwa.
Je! umejiwekaje tayari??
Ni jambo la kushangaza, kama wewe bado mpaka leo hii, unapuuzia habari za wokovu.. Unasubiri siku ile ikujie kwa ghafla ndio uamini?
Tubu dhambi zako sasahivi, mpokee YESU maishani mwako, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili upokee kipawa cha Roho Mtakatifu, sawasawa na Matendo 2;38, uupate wokovu.. kisha uishi maisha ya kama mtu anayemngojea KRISTO..Ili siku ile na wewe uwe mmojawapo wa watakaonyakuliwa na Bwana..
Maran atha. (Na uje Bwana Yesu)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.