JE WEWE NI CHOMBO KIPI??

Biblia kwa kina No Comments

JE WEWE NI CHOMBO KIPI??

Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe sana, karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu lililo taa na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

2 Timotheo 2:20-21 “Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.

[21]Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.”

Katika nyumba zetu huwa kuna vile vyombo maalumu kwa ajili ya wageni, na hivi huwa vinaheshimiwa sana..vinawekwa kabatini…havitumiki ovyo ovyo kama vile vingine vya siku zote ambazo vinaweza hata kuachwa nje.

Na halikadhalika katika nyumba ya Mungu yaani kanisa la Kristo…vipo vyombo vya thamani na heshima na vingine havina thamani wala havipewi heshima yoyote. Hawa ni wale wakristo jina, wakristo vuguvugu, wanawali wapumbavu… lakini vile vyombo vya thamani ni wale wakristo kweli kweli ambao wamekubali kuikana nafsi zao na kumfuata Yesu kweli kweli, wameacha ulimwengu na anasa zote za dunia…hawa ni wale wanawali wenye busara. (Mathayo 25)

Je! wewe ni chombo kipi? Ni chombo cha ghadhabu au cha rehema.

Warumi 9:22-24 “Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;

[23]tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;

[24]ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia.

Kama maisha yako yametawaliwa na dhambi basi fahamu kuwa ni dhahiri kuwa wewe ni chombo kilichoharibika, kama maisha yako yametawaliwa na ugomvi, uasherati, wizi, masengenyo, kiburi na mambo mengine yote ambayo ni kinyume cha Neno la MUNGU (yaliyotajwa kwenye Wagalatia 5:19-20), huu ni wakati wa wewe kumkimbilia mfinyazi Mkuu YESU KRISTO, akufinyange kuwa chombo kingine cha heshima..

Warumi 9:21 “Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”

Bwana YESU anaweza kukufanya kuwa mwingine kabisa, mtu wa maana kabisa, ambapo ile hali yako ya ulevi wa pombe au ulevi wa anasa inayokusumbua, kinachotakiwa tu ni kukiri kuwa wewe ni mkosaji mbele zake na unahitaji msaada wake, na baada ya hapo kutubu dhambi zako mbele yake huku ukidhamiria kabisa kuacha mambo yote mabaya, na kumwambia naomba unifinyange tena, kupitia Roho wake mtakatifu atakayeingia ndani yako atakugeuza na kuwa mtu mwingine.

Kumbuka toba isiyo ya kumaanisha haileti matokeo yoyote kwa mtu anayetaka mabadiliko, hakikisha unapotubu dhamiria kujitakasa, kwa kujitenga na vichocheo vyote vya dhambi, kama ulikuwa ni mlevi acha kwenda Bar, kama ulikuwa unajiuza jizuie kwa bidii kwenda vituo vya ulivyokuwa unafanya biashara hiyo, ili uumpe nafasi Roho Mtakatifu ndani yako kukufinganya upya kuwa chombo cha heshima.

2Timotheo 2:21 “Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema”.

Bwana YESU akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *