
USIIHARIBU SIKU YAKO.
Ukitaka kujiharibia mwenyewe siku yako, amuka asubuhi na mapema, anza kufanya mambo yako badala ya kuanza siku yako na Mungu.
Bwana Yesu alikuwa na desturi ya kuamka asubuhi na mapema na kuanza siku yake na Baba wa mbinguni kabla hajafanya jambo lolote. Tunasoma..
Marko 1:35 “Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.
Mungu mwenyewe alikuwa akiamka alfajiri na mapema na kutuma watumishi wake kuwarudisha watu wake,
Yeremia 44:4 “Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo”.
Unaona Alfajiri siku zote ni ya Mungu..sehemu nyingi sana katika biblia utaona tukio fulani lilifanyika alfajiri au asubuhi na mapema. Mungu alipoiumba hii dunia kwa siku sita, utaona alisema ”ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya kwanza, ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya pili mpaka uumbaji ulivyokamilika…Na sio ikawa mchana ikawa usiku siku ya kwanza. Hivyo kibiblia siku inaanza asubuhi na sio usiku kama tulivyofundishwa kwa hekima za wanadamu, Ijapokuwa hakuna dhambi kutumia hiyo kalenda.
Sikuzote asubuhi na mapema ni wakati mtulivu ndio mwanzo wa siku, ambao mtu analazima kukatiza usingizi wake kwa ajili ya mambo ya muhimu sana. Na jambo la kwanza kabisa mtu akiamka asubuhi anachopaswa kufanya ni Kumbariki Mungu wake (kwakumshukuru, kumwimbia na kumsifu). Ndege wakiamka asubuhi jambo la kwanza wanalolifanya ni kumsifu Mungu kwa sauti kuu ya shangwe, utawasikia kila mahali kwenye viota vyao kabla hata hawajaenda popote huko ndani wanamsifu Mungu. Daudi aliamka ALFAJIRI na kumbariki Mungu kwa vinanda na vinubi kwa sauti Kuu sana.
Zaburi 57:7 “Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu uthabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,
8 Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, NITAAMKA ALFAJIRI. 9 Ee Bwana,nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
10 Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Nauaminifu wako hata mawinguni. 11 Ee Mungu, utukuzwe juuya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako”.
Ukiamka na Bwana, basi siku yako yote itakuwa ni ya Baraka. Lakini ikiwa utamka asubuhi jambo la kwanza ni kukimbilia SMARTPHONE yako uangalie message zote jana zilizotumwa whatsapp na facebook. Jambo la kwanza ni kuchati na kupiga simu za biashara zako, jambo la kwanza ni kuamka na kuwatukuza wanadamu badala ya muumba wako, Jambo la kwanza ni kuongea na mpenzi wako ambaye hata si mke wako/mume wako. Basi fahamu kuwa hata siku yako nzima umeiharibu mwenyewe.
Mika 1: 1 “Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao”
Isaya 5:11 “Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao!”.
Leo anza kutengeneza siku yako na Bwana, Unapoamka kabla ya kufanya kitu chochote kile, hata kabla ya kwenda kupiga mswaki…nenda mbele za Mungu tumia hata lisaa limoja, mshukuru Mungu kwa kukuamsha salama lakini hata kama haupo vizuri mshukuru Mungu pia, msifu, litukuze jina lake, ombea siku yako yote. Baada ya hapo utakuwa umeibariki siku yako na utakutana na baraka za Mungu na amani ya Bwana itakuwa nawe siku nzima.
Kumbuka ujumbe huu ni kwa mtu aliye mkristo kweli kweli, kama bado hujaokoka, yakupasa kwanza umpe Yesu maisha yako. Ndio mambo mengine yafuate.
Na kama utahitaji muongozo wa maombi ya asubuhi basi wasiliana nasi kupitia namba zilizopo chini ya makala hii kisha tutakutumia.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Maran atha (Bwana Yesu anarudi)