
BWANA ASUBUHI UTAISIKIA SAUTI YANGU
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu. Na leo tutajifunza umuhimu wa kuamka asubuhi na mapema na kuanza siku na Bwana.
Moja ya jambo lililomfanya Daudi aupendeze moyo wa Mungu ni upendo aliokuwanayo kwa Mungu wake. Japo Daudi aliwahi kufanya kosa la kulala na mke wa Huria lakini alijutia makosa yake akatubu kweli kweli na Mungu akamsamehe. Hivyo katika maisha yake yote ..mpaka uzeeni hakuwahi kumuacha Mungu tena, japo alikutana na magumu mengi lakini bado alimpenda Mungu, Daudi alikuwa ni mtu wa kumsifu Mungu sana hadi mara saba kila siku.
Zaburi 119:164 “Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako”.
Mbali na mengi Daudi aliyokuwa anayafanya kwa Mungu wake ikiwemo kumtafakari Mungu usiku na mchana, kupenda na kushika maagizo yake, kumwamini na kumtegemea, lakini pia kwasababu ya moyo huu wa upendo… Daudi alijiwekea desturi ya kuamka asubuhi na mapema sana na kumpangia Mungu dua yake kila siku. Huu nao ni moyo ulioelekea kwa Mungu… kwanini Mungu naye asikupende sana.
Zaburi 5:3 BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.
Wakati leo hii sisi tunamkia simu zetu na kuangalia taarifa mpya zilizotumwa, Daudi yeye alikuwa akiamka anashibishwa kwanza na wema wa Mungu.
Zaburi 17:15 Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
Je tunaweza kuwa na moyo huu kama wa Daudi??
Zaburi 88:13 Lakini mimi nimekulilia Wewe, BWANA, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia.
Jenga tabia ya kuamka asubuhi na mapema kabla jua halijachomoza.. kumshukuru Mungu na kumpa dua zako kama Daudi alivyokuwa akifanya.
Bwana Yesu alikuwa anaamka asubuhi na mapema kuomba. Je! Sisi ni nani tusiamke kuomba?
Marko 1:35 “Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.”
Ayubu mtu mkamilifu alikuwa anaamka kila siku asubuhi na mapema na kuwaombea watoto wake rehema, je! wewe unaujasiri gani wa kuamkia kazi zako wakati familia yako hawajamjua Mungu.
Ayubu 1:5 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha AKAAMKA ASUBUHI NA MAPEMA, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.
Kuamka asubuhi na kufikiria mambo yako au kufanya mambo yako ni sawa na kutumikia miungu mingine. Na kama kweli umeelekeza moyo wako kwa Bwana Yesu huwezi kufanya hivyo.
Kuanzia kesho anza kujitengenezea tabia ya kuamka alfajiri na mapema kuomba, na kumsifu Mungu. Usiruhusu mwili/usinginzi ikushinde au jambo lolote lichukue nafasi ya Mungu ndani ya moyo wako.
Ndege na wanyama huwa wanatabia ya kumpa Mungu dua kila alfajiri kabla wajatoka kwenda kwenye shughuli zao. Je sisi ni akina nani?
Zaburi 57:7-8 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,
8]Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, NITAAMKA ALFAJIRI.
Kama utahitaji muongozo wa maombi ya asubuhi.. wasiliana nasi kupitia namba uzionazo chini ya makala hii.
Bwana Yesu akubariki.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.