TUMEANDALIWA NCHI NZURI YA KUMETA META

Biblia kwa kina No Comments

TUMEANDALIWA NCHI NZURI YA KUMETA META

Mtunzi wa tenzi namba 143, katika ule ubeti wa kwanza anaimba akisema..

Nchi nzuri yametameta, Huonekana kule mbali, Naye Yesu hutuongoza. Tukafike na sisi huko”.

Je! na wewe unaiona ile nchi nzuri ya kumeta meta mbele yako?

Kuna nchi nzuri ambayo Bwana ametuandalia mbele, hiyo nchi ni nchi yenye utukufu mwingi sana hatuwezi kuuelezea uzuri wake kiubinadamu. Lakini biblia inasema ndani yake…

“…mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita”.(Ufunuo 21:4), na tena ukisogea mstari wa 23 anasema..

“.. mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo”. Haleluya.

Mji huu, ndio ile ambayo Ibrahimu baba yetu wa Imani alikuwa akiutazamia kwa shauku mwingi, hivyo akaishi hapa duniani kama mpitaji tu.

Waebrania 11:8-10

[8]Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.

[9]Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

[10] MAANA ALIKUWA AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

Unajua ni kwanini leo watu hatutaki kujikana nafsi kweli kweli na kuacha vyote kwa ajili ya Kristo, ni kwasababu hatuoni yaliyo mbele yetu, tunaona ya hapa hapa tu, hatuoni majira ya neema yanayokuja huko mbeleni, hatuioni Yerusalemu mpya na nchi mpya tuliyoahidiwa na Mungu. Hatuoni Karamu ya mwanakondoo ambayo Yesu alikwenda kutuandalia kwa miaka 2000 sasa ipo karibuni kuanza.

Na ndio maana hatutaki leo hii kumfuata Kristo kwa mioyo yetu yote ijapokuwa tunatamka katika vinywa vyetu kuwa tunampenda lakini mioyo yetu bado imeshikamana na dunia, ndio maana hatutaki kujitia katika utimishi wake,

Tunachojua ni kujitia katika utumishi wa kusumbukia maisha, tupate magari, tupate majumba, mashamba, tuwe mabilionea., hayo tu, Mambo ambayo fahari yake inaishia hapa hapa duniani.

Hata kuhudhuria ibada tunaona ni mzigo mzito, lakini tupo radhi kufanya kazi siku 365 bila kuchoka, usiku na mchana, tupo radhi kutazama Tv kila siku, lakini kusoma aya moja ya biblia na kuitafakari ni mtihani kwetu..Kama hayo yakitushinda tutawezaje, kuwa watumishi wa Mungu? Tunawezaje kuingia katika ile nchi? Kwamaana anasema…

.. ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo,..” (Ufunuo 21:27)

Ndugu yangu, hebu leo fumbua macho yako uone ile nchi mpya, nzuri ya kumeta meta ambayo tumeandaliwa, kuwa tayari kuacha ulimwengu na kumfuata Kristo ambaye ni njia ya kutufikisha kwenye nchi hiyo kama vile torati ya Musa ilivyokuwa njia ya kuwafikisha wana wa Israeli kwenye nchi yao ya ahadi.

Kumbukumbu la Torati 8:5 “Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo.

[6]Nawe uzishike amri za BWANA, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.

[7]Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;

[8]nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;

[9]nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba.

[10]Nawe utakula ushibe, utamshukuru BWANA, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa.”

Shalom

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *