SISI NI TAIFA TEULE LA MUNGU.
1 Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, TAIFA TAKATIFU, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;
[10]ninyi mliokuwa kwanza si taifa, BALI SASA NI TAIFA LA MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”
Bwana Yesu Kristo asifiwe mtu wa Mungu, karibu tujifunze maneno ya uzima.
Ikiwa umeingia katika Agano la Damu ya Yesu kweli kweli (kwa kuzaliwa mara ya pili), basi fahamu we ni taifa teule la Mungu sawa na taifa la Israeli.
Sasa, sisi kama taifa teule la Mungu, Mungu ametupa sheria na maagizo yake ambazo ndizo zinazotutofautisha na mataifa mengine, na kwamba tukizishika na kuziishi tutaonekana watu wenye hekima na akili sana.
Kumbukumbu la Torati 4:5-8 Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.
[6]Zishikeni basi, mkazitende, MAANA HII NDIYO HEKIMA YENU NA AKILI ZENU, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.
[7]Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?
[8]Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
Swali ni je! wewe unayesoma ujumbe huu, ni raia wa taifa la Mungu? Na kama ni ndiyo, je unazishika sheria na amri za Mungu ipasavyo?
Kumbuka, kushika amri na sheria za Mungu hatumainishi zile amri kumi tu, bali ni maneno yote ya Mungu ambayo tunayasoma kwenye biblia ambayo ndiyo katiba yetu.
Na mtu awaye yote ambaye sio mwenyeji wa taifa la Mungu, hawezi kuzishika na kuziishi amri na sheria za Mungu, kwasababu hana msaidizi na pasipo huyo haiwezekani kamwe kuishi Neno la Mungu..hata iweje!.
Sasa, tutapataje huyo msaidizi atakayetusaidia?
Kwanza kwa kuwa mwenyeji wa taifa la Mungu, na hiyo inawezekana tu kwa kuzaliwa mara ya pili..hapo ndipo utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu ambaye ndiye msaidizi atakayetusaidia kuziishi amri na sheria za Mungu bila kutumia nguvu yoyote.
Na Kuzaliwa mara ya pili sio kuzaliwa kwa jinsi ya damu na nyama, bali kwa Roho na kwa Maji..kama tunavyosoma katika..
Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.
Maana ya kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa maji mengi (Yohana 3:23) Na kwa Jina la Yesu (Matendo 2:38). Na maana ya kuzaliwa kwa Roho ni kupata ubatizo wa Roho Mtakatifu. Hatua hizo mbili ndio zinazokufanya uwe umezaliwa mara ya pili na kuwa Mwananchi wa ufalme wa Mbinguni. (Taifa la Mungu).
Madhara ya kutokuwa na sehemu ya taifa takatifu la Mungu.
Usipozaliwa mara ya pili na kuwa sehemu ya taifa la Mungu, moja kwa moja hautakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu, sehemu yako itakuwa ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti, huo ndio ukweli..kasome ufunuo 21:8.
Na kabla ya hiyo hukumu ya ziwa la moto, ipo dhiki kuu ambayo inakuja kwa mataifa yote ya duniani..wakati huo wanadamu watalia na kusaga meno.
Obadia 1:15-16 Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.
[16]Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kubabaika, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe.
Siku hizo kutakuwa na maombolezo makuu kwa watu wa mataifa yote, Bwana anasema..
Sefania 3:8
[8]Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.
Ikiwa unapenda maisha yako, hebu tubu dhambi zako mpe Yesu maisha yako ili ufanyike taifa teule takatifu la Mungu na hapo utakuwa umeepuka hukumu ya Mungu.
Kumbuka hukumu ya Mungu kwa mataifa imekaribia, angalia ni nini kinakuzuia usizaliwe mara ya pili? Ili ufanyike taifa teule la Mungu na uepuke hukumu hiyo.
Mungu atusaidie
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.