NAKUPA SHAURI UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA.
Ufunuo wa Yohana 3:15 ”Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
[17] KWA KUWA WASEMA, MIMI NI TAJIRI, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
[18] NAKUPA SHAURI, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
Hayo ni maneno ya Bwana Yesu aliyowaambia watu wa kanisa la Laodikia, ambalo kanisa hilo kiroho ni sisi wakristo wa siku hizi za mwisho.
Utaona anawashutumu watu wa kanisa hilo na kuwaambia kuwa WANAJIONA KUWA NI MATAJIRI, kumbe ni MASKINI. Lakini Pamoja na hayo utaona anawashauri wakanunue kwake DHAHABU ili wawe matajiri!!!
Kristo hapa anajiweka sawa na mfanyabiashara na kwasababu yeye ni mfanyabiashara mwema…anatuhurumia sisi ambao tunajiona ni matajiri kumbe ni maskini na kibaya zaidi hatujioni, na hapa anatupa shauri tukanunue kwakwe dhahabu ili tuwe matajiri wa kweli.
Na kwanini iwe dhahabu na sio kitu kingine, ni kwasababu ufalme wa Mungu unafananishwa na dhahabu. Kama tunavyojua dhahabu ni kitu chenye thamani kubwa ambayo mtu akiipata anakuwa bilionea..ndio maana yule mfanyabiashara alipoiona ile lulu ambayo thamani yake ni sawa na dhahabu..alienda kuuza vyote alivyo navyo ili aipate.
Mathayo 13:45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
[46]naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.
Naam Kristo ni dhahabu kubwa. Ndiyo lulu yenyewe, lakini tunampataje? Ni kwa kuuza vyote.
Maana yake kama hatutakubali kuuza vyote tulivyonavyo ili tupate fedha za kuinunua hiyo Lulu, hatutaweza kuinunua na tutaendelea kuwa maskini hivyo hivyo hata kama tunajiona hatuna haja na kitu…kumbuka ni lulu yenye thamani kubwa ambayo gharama yake hakuna mtu anaweza kununua, lakini yeye amejishusha sana ili tumpate. Tukirudi kwenye huo mfano wa huyo mfanyabiashara..
Kumbuka huyu ni mfanya biashara, lengo lake ni apate faida awe Tajiri, hivyo katika pitapita zake akakutana na lulu mahali Fulani ambayo inauzwa kwa bei ya chini, na yeye anajua soko la mahali inapouzwa kwa bei ya juu.. na akaona endapo akienda kuinunua kwa bei hiyo ya chini na kwenda kuiuza kwenye soko la juu atapata faida nyingi sana…sasa kwa busara akaenda kuuza shamba lake, na vyote alivyonavyo ili aipate fedha ya kutosha kuinunua hiyo lulu inayouzwa kwa bei ya chini… Lengo la kwamba atakapoenda kuiuza kwa bei ya juu itamrudishia fedha ya kutosha ya kununua vyote alivyovipoteza na Zaidi sana kubakiwa na faida nyingi.
Ndicho Bwana Yesu alichokuwa anamaanisha hapo katika hiyo Habari ya dhahabu.. Kwamba mtu yeyote akitaka kuwa Tajiri basi aende kwake akanunue dhahabu hiyo, kwa bei ya chini, ili akaiuze kwa bei ya juu, na kubakiwa na faida ambayo ndio utajiri wenyewe.
Tukitaka kuupata ufalme wa mbinguni ambao ndio unaofananishwa na Dhahabu na Lulu. Hatuna budi kuacha vyote tulivyonavyo vinavyozuia sisi kuupata huo uzima wa milele (Hiyo Ndio maana ya kuuza vyote na kwenda kuinunua lulu/dhabahu).
Tukishaacha vyote yaani Ulevi wetu, uongo wetu, wizi wetu, anasa zetu, kiburi chetu, uasherati wetu, umaarufu wetu, ujuzi wetu ambao unatuletea kiburi, ujuaji wetu, na biashara zetu haramu, kama za madawa ya kulevya, au uuzaji wa pombe, au utapeli au rushwa n.k Tunapoviacha hivi vyote, na kumfuata Yesu hapo ni sawa na tumeuza vyote, na katika viwango vya kimbinguni tumejipatia credit tosha za kuupata Ufalme wa mbinguni (ambao ndio unaofananishwa na ile lulu au dhahabu safi).
Mathayo 19:20 “Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni”.
Umeona gharama za kuinunua ile DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO!!!.. Suluhisho ni kuacha vyote, kuvitoa ndani ya moyo wako..
Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
Unaacha vyote na kumfuata Yesu kama ulivyo.. Bwana Yesu anawapenda watu wanyenyekevu, ambao wameamua kabisa kuanza moja katika Maisha yao, ambao wamejikana nafsi, ambao wamedhamiria kabisa kuzaliwa upya.. Leo Bwana anakuita, anataka akutumie kama chombo kipya, hivyo kubali leo ushauri huu wa busara ambayo Bwana anakushauri, (huu ni ushauri wa bure kabisa wenye faida tele), hivyo acha kiburi, vua ujuzi wako leo, vua kiburi chako, acha dhambi zako, na mambo yote yanayokusonga na mfuate naye atakupenda!, na kukupa zawadi ya Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia katika kushinda dhambi, na kukufanya kuwa mtumishi wake..
Usijione kuwa ni Tajiri, na huna haja ya kitu!.. (usiojione kuwa humhitaji Yesu kwa sasa) bado unamuhitaji sana, bado unaihitaji ile Dhahabu.. nenda kainunue kwa Bwana, kwasababu inapatikana kwa bei ya chini.. na ukiinunua na kwenda kuifanyia biashara, yaani kuwafundisha wengine Habari za ufalme wa mbinguni, utakuwa Tajiri sana katika ufalme wa mbinguni.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.