
TU WASAFIRI HAPA DUNIANI.
1Mambo ya Nyakati 29:15 “Kwani sisi tu wageni mbele zako, NA WASAFIRI, KAMA WALIVYOKUWA BABA ZETU WOTE; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana”.
Mtu yeyote anayejiita ni mkristo ni wazi kuwa yupo safarini, Na kama yupo safarini ni lazima afahamu malengo yake ni nini, kwamba anatoka wapi, na anakwenda wapi? Na Sababu ya yeye kumfanya atoke pale alipo aende huko aendako ni ipi?, Kadhalika ni lazima ajue ni njia gani atakayoipita, na chombo kipi atakachokitumia kusafiria pamoja na gharama zake..! Lakini ukiwa ni msafiri halafu hujui hayo yote, ni dhahiri kuwa utaitwa MTORO, kama vile Kaini alivyoambiwa na Bwana Mungu kwamba atakuwa“mtoro na mtu asiye na kikao duniani (Mwanzo 4:12)”.
Na huo uzao wa Kaini unatenda kazi miongoni mwa kundi kubwa linalojiita la wakristo, hawana vikao, hawajulikani ni watu wa ulimwengu huu, au ni wasafiri wa kwenda mbinguni, Kumbuka Kaini na Habili wote walikuwa ni ndugu, isipokuwa mmoja hakuonekana kuwa mkamilifu mbele za Mungu.
Mtu aliye makini katika safari yake, siku zote anaona mwisho wa safari yake utakuwa ni upi hata kabla hajaianza hiyo safari, na atatambua ya kuwa wakati akiwa njiani atakutana na mambo mengi tofuati tofauti, na majira mengi tofauti tofauti, hivyo atakuwa makini akijua kuwa yupo safarini kwahiyo hatayatilia maanani mambo yanayopita ya njiani, hata akifika kituoni labda kwa muda mchache tu atashuka kuchuka chakula na kurudi kwenye chombo chake cha usafiri na kuendelea na safari yake, hatashikamana au kuambatana na shughuli zinazoendelea katika hicho kituo alichofika kwa muda tu, huwezi kuona anakwenda kuzunguka tena mijini, labda kwenye viwanja vya michezo, na majukwaa ya sinema, na kutangatanga huku na huko ni kwasababu gani? Kwasababu anajua akifanya hivyo muda wake hautamtosha hivyo ataachwa na kile chombo alichokuwa anasafiria, na hapo pia si sehemu yake aliyotarajia kufika, Kwahiyo yeye mahali popote anapopita atatafahamu ni mpitaji tu,
kadhalika na katika ukristo wa kweli sisi ni wasifiriji tu, ulimwenguni sio kwetu,..Mkristo ni lazima afahamu yeye anatoka wapi, na anakwenda wapi, na kitu gani kinachompeleka huko aendako,,.Safari yetu sisi ni kutoka katika ulimwengu mmoja na kwenda katika ulimwengu mwingine, tunatoka katika ulimwengu huu uliopo sasa unaoharibika na kwenda katika ulimwengu mpya wa milele usioharibika, na ili kuufikia huo ulimwengu mpya ipo njia ya kuipitia, hebu tuone hiyo njia..
Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, NJIA YA UTAKATIFU; WASIO SAFI HAWATAPITA JUU YAKE; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO”.
Unaona hapo sio kila njia tu tunajichagulia kupita, hapana!. Tunapita katika NJIA KUU, Hii imeitwa Njia kuu kwasababu wanaopita juu yake ni wachache, na ni WATAKATIFU tu WALIOSAFARINI ndio watakaopita juu yake, Hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kupita katika hiyo njia isipokuwa amekidhi hivyo vigezo.

Ndugu kama huna UTAKATIFU haupo katika hiyo njia, hata kama utatoa zaka kiasi gani, kama wewe haujajiweka kama mtu anayesafiri, basi jua haupo katika njia hiyo. Biblia ipo wazi kabisa inasema.
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”;
Unaona hapo?, wewe unayesema ni mkristo na unasema upo safarini, umefika katikati ya safari yako umekutana na anasa na burudani za ulimwengu huu, unasahau kuwa wewe ni mkristo unayesafiri unaanza na wewe kushikamana na hivyo vitu vya ulimwengu huu vinavyopita, unaanza na wewe kuhudhuria karama za ulafi, unaanza kujishughulisha na rushwa, unaanza kujichanganya na watu waovu wa ulimwengu huu, ulikuwa ni mwombaji mzuri hapo mwanzo lakini sasa biashara na udanganyifu wa mali vinakusonga, wewe kila wakati ni mali tu, unasahau maisha yako ya rohoni, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria (Neema) hakiwezi kikakusubiria muda wote huo,
Ulikuwa unavaa vizuri na kujisitiri hapo mwanzo, lakini ukafika kituo ukakutana na fashion za ulimwengu huu, ukasahau kuwa upo safarini ukauacha utakatifu uliokuwa nao hapo mwanzo na wewe ukaanza kuvaa suruali na kaptura, ukaanza kuvaa nguo fupi, ukaanza kuvaa nguo zinazochora maumbile yako, ukaanza kupaka ma-lipstick, na wanja, na hereni na ma-wigi kama wanawake wa ulimwengu huu, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria kimeshaanza kukuacha.
Mwanzoni mwa safari yako mawazo yako yalikuwa yameelekea mbinguni tu, ulikuwa unatamani ufikie kilele cha safari yako mapema, ulikuwa unafikiria kila siku habari za mbingu mpya na nchi mpya lakini umefika mahali umegota safarini, umeiacha NJIA KUU YA UTAKATIFU, umeanza kutazama pornography, umeanza kusengenya, umeanza kutukana, umeacha upole wako na ukarimu wako, ndugu ukiendelea hivyo hivyo hautauingia ule mji Yerusalemu ya Bwana, usijidanganye na Dini yako ukadhani inatosha kukufikisha mbinguni, kwasababu biblia ilishasema..”
Mithali 14: 12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”..Kumbuka kama ilivyosema..Pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu.
Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, NJIA YA UTAKATIFU; WASIO SAFI HAWATAPITA JUU YAKE; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.
Umeona biblia inasema watakaopita katika njia hiyo, ulimwengu utawaona ni wajinga, wataonekana kama watu wasiostahili kuwa katikati yao, wanawake waliokataa mitindo ya ulimwengu huu wataonekana washamba na wajinga, wanaume wasiokuwa walevi, wala waasherati, watu wanaoishi maisha matakatifu watadharauliwa, lakini hao ndio Mungu aliowachagua wapite katika njia ile KUU, Biblia inasema wajapokuwa ni wajinga machoni pa ulimwengu lakini hawatapotea katika njia hiyo.
Kumbuka ndugu, biblia imetuonya tufanane na wasafiri wenzetu wa Imani waliotutangulia, ambao walijikana kweli kweli, watu ambao mawazo yao yote yalikuwa ni mbinguni tu, kama tunavyowasoma katika
Waebrania 11: 36 “wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;
38 (WATU AMBAO ULIMWENGU HAUKUSTAHILI KUWA NAO), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.
39 Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;
40 kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi…”
Waebrania 11: 13 Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, NA KUKIRI KWAMBA WALIKUWA WAGENI, NA WASAFIRI JUU YA NCHI.14 MAANA HAO WASEMAO MANENO KAMA HAYO WAONYESHA WAZI KWAMBA WANATAFUTA NCHI YAO WENYEWE.
15 Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.
16 Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji”.
Ndugu hawa watu walijikana nafsi zao kwasababu waliuona uzuri uliopo mbele yao, waliona furaha isiyokuwa na kifani kuingia katika ule mji, waliona ni heri maisha yao ya miaka 80 yasiwe ni kitu kulinganisha na miaka ya umilele inayokuja huko mbeleni.
Na ndio maana tunasoma Ibrahimu licha ya kupewa utajiri wote ule wa kimwilini, bado aliendelea kuishi katika nchi ile ambayo ni kweli ilikuwa ni haki yake kustarehe na kujifurahisha lakini biblia inatuambia aliishi mule kama vile siyo nchi yake, aliishi katika milki yake kama vile sio milki yake, kama vile mgeni nyumbani kwake mwenyewe..aliisha na mke wake Sara kwenye mahema, fikiria Ibrahimu alikuwa ni mtu tajiri sana mwenye mali nyingi alizopewa na Mungu lakini hakuishi kwenye makasri,..hiyo inafunua nini?..Inaonyesha ni jinsi alivyoishi kama mpitaji hapa duniani?.
Unadhani alikuwa hajipendi?. Hapana..Biblia inatuambia ni kwasababu alikuwa anautazama mji ulio bora, alikuwa anautazamia mji wenye misingi, sio ule wa Kaanani aliopewa ambao Mungu kweli alimpa kuwa milki yake, lakini huo ingempasa aweke misingi yeye iliyodhaifu, ingempasa aubuni yeye..Lakini badala yake Ibrahimu hakufanya hivyo bali aliutazamia mji wenye misingi ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu mwenyewe.. Na mji huo si mwingine zaidi ya YERUSALEMU MPYA ya mbinguni HALELUYA!!.
Waebrani 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”.
Jambo hilo ndilo lililomfanya Mungu apendezwe na Ibrahimu na kumfanya awe kielelezo cha kuigwa kwa watu wote, ikiwemo mimi na wewe.
Ndugu kosa kila kitu lakini usikose mbingu. Biblia inasema wenye haki watang’aa kama jua, Mambo ambayo Mungu amewaandalia wampendao ni mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia,
hakutakuwa na uchungu tena, wala kudharauliwa, watapewa miili ya utukufu wa ajabu, watatawala na Kristo Yesu kama wafalme na makuhani, milele na milele, tujitahidi tusikose huko.
Utajisikiaje unyakuo umepita na wewe umeachwa? Wenzako wamekwenda katika karamu ya mwanakondoo mbinguni na wewe umebaki?hapa duniani ukisubiria ziwa la moto?
Utajisikiaje??..Ifuate hiyo NJIA KUU LEO, kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako kama hujafanya hivyo angali muda upo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji tele na kwa Jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38) na kisha utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kitakachokuwezesha kuwa mtakatifu ili uweze kuiendea hiyo NJIA KUU YA UTAKATIFU ili siku ile Uingie katika ile Yerusalemu mpya ya Bwana aliyowaandalia watakatifu wake.
1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.