
ENYI WAPUMBAVU, LINI MTAKAPOPATA AKILI?
Zaburi 94:7 “Nao husema, BWANA haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.
[8]Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?
Mpumbavu ni nani kibiblia?
Mpumbavu ni mtu asiye na akili, na hapa hatuzungumzii akili ya darasani au kuwa na maarifa ya kidunia, hapana, unaweza ukawa na degree zote au ukawa namba moja darasani lakini kwa Mungu ukawa hauna akili.
Kwa maana hiyo, akili tunayozungumzia ni akili ya kumjua Mungu na kumcha, mtu yoyote asiyekuwa na akili hiyo, haijalishi anajua kufanya biashara vizuri, au anafaulu vizuri katika maisha yake, huyo kwa Mungu hana akili ni mpumbavu.
Zifuatazo ni tabia za mtu asiye na akili kibiblia/mpumbavu.
Mithali 10:8 “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka”.
Mithali 9:13 “Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu”.
Mithali 10:14 “Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu”.
Mithali 10:23 “Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima”.
Mithali 12:15 “Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri”.
Mithali 14:16 “Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai”.
Mithali 20:3 “Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana
Zaburi 14:1 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema”.
Hivi ni baadhi ya vifungu tu, lakini unaweza kuona mpumbavu ni mtu anayetajwa kuwa ana dharau, asiye na heshima, anayeropoka ropoka, asiyemcha Mungu, asiyeamini hata kama kuna Mungu, asiyetaka kurekebishwa, anayependa ugomvi, anayesambaza habari za uzushi n.k.
Hivyo tafsiri hasaa ya Neno mpumbavu, ni mtu ambaye hajazaliwa mara pili (ambaye hajaokoka).
Kwahiyo ikiwa wewe upo nje ya Kristo, haijalishi utakuwa msomi kiasi gani, au utakuwa tajiri kiasi gani, au utakuwa na ushawishi mwingi kiasi gani, wewe ni mpumbavu kibiblia, kwasababu hutakosa tabia mojawapo ya wapumbavu zinayozungumziwa katika biblia.
Hivyo ni heri leo ukampa Yesu maisha yako ili upate akili uondokane na upumbavu.
Ni Yesu pekee ndio mwenye uwezo wa kumgeuza mtu moyo wake na kumfanya kuwa mtu mwingine kabisa. Yeye mwenyewe alisema.. Wote wanaompokea anawapa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu. (Yohana 1:12). Hii ikiwa na maana ukimkaribisha Yesu katika maisha yako, ni uhakika kuwa UWEZO huo utakuja ndani yako, wa kuweza kuzishinda tabia zote za wapumbavu, yaani kushinda ulevi, kushinda uzinzi, kushinda anasa, kushinda usengenyaji n.k..
Ikiwa upo tayari leo kuokoka, basi fungua hapa kwa ajli ya kuongozwa sala ya Toba na kupata maelekezo mengine ya kiroho >>>>> SALA YA TOBA
Bwana akubariki sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618