UNABII ULIO MBIONI KUTIMIA HIVI KARIBUNI!!.

Siku za Mwisho No Comments

UNABII ULIO MBIONI KUTIMIA HIVI KARIBUNI!!

Ezekieli 38:14 “Basi, mwanadamu, tabiri, umwambie Gogu, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile watu wangu, Israeli, watakapokaa salama, hutapata habari?

[15]Nawe utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini, wewe, na watu wa kabila nyingi pamoja nawe, wote wamepanda farasi, kusanyiko kubwa, na jeshi kuu;

[16]nawe utapanda juu uwajilie watu wangu, Israeli, kama wingu kuifunika nchi; itakuwa katika siku za mwisho, nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue, nitakapotakaswa kwako, Ewe Gogu, mbele ya macho yao”.

Vita vya Gogu na Magogu ipo mbioni kutokea.

Vita vya Gogu na Magogu vitahusisha mataifa ya kiarabu kama Iran, Lebanoni, Iraq, Sirya, Saudi Arabia, na mengineo wakiungana na taifa la Urusi (Gogu) kama mkuu wao kuvamia taifa la Israeli.

Kumbuka Magogu sio wingi wa Gogu… bali ni jina la mtu mmoja, ambalo tunalipata katika kitabu cha Mwanzo 10:2.

Mwanzo 10: 1 “Hivi ndivyo vizazi vya wana wa Nuhu, Shemu, na Hamu, na Yafethi. Na kwao walizaliwa wana wa kiume baada ya gharika.

2 Wana wa Yafethi ni Gomeri, na MAGOGU, na Madai, na Yavani, na Tubali, na Mesheki, na Tirasi.

Magogu kama tunavyosoma alikuwa ni Mjukuu wa Nuhu, alikuwa ni Mtu. Sasa mtu huyu biblia haijaeleza alikuwa ni mtu mwenye sifa gani, lakini kutokana na uwepo wake katika sehemu nyingine za biblia, inaonekana wazao wake walikuja kuwa watu Hodari kipindi hicho, na mwenye uwezo mkubwa sana wa kijeshi, na kiuchumi, mfano wa Nimrodi aliyeujenga Babeli.

Na Magogu naye ni hivyo hivyo, uzao wake ulikuja kuwa Hodari..na kuwa Taifa lenye nguvu kijeshi, na watu hao wote kwa ujumla wakaitwa Magogu kufuatia jina la baba yao huyo.

Kama vile mji wa Moabu ulivyoitwa kufuatia jina la baba yao aliyeitwa Moabu. (Mwanzo 19:37 “Yule mkubwa akazaa mwana, akamwita jina lake Moabu; huyo ndiye baba wa Wamoabi, hata leo”)

Na Magogu ni hivyo hivyo, Uzao wake ulikuja kuitwa kwa jina hilo la Magogu, na nchi yao ikaitwa nchi ya Magogu, kufuatia jina la baba yao huyo aliyeitwa Magogu.

Tunalisoma hilo vizuri katika Ezekieli..

Ezekieli 38:1 “Neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, kaza uso wako, umwelekee GOGU, wa NCHI YA MAGOGU, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali, ukatabiri juu yake.

Na nchi hiyo ilikuwa upande wa kaskazini mwa Asia na Ulaya, ambayo sasahivi ni Maeneo ya nchi ya Urusi. Hatima ya hilo Taifa la Magogu, biblia haijaieleza, lakini ni wazi kuwa lilikuja kupotea kama yalivyopotea mataifa mengine yaliyokuwa hodari kama Babeli.

Lakini huyu Gogu ni nani? Kama tulivyotangulia kusema Magogu sio wingi wa Gogu. Bali Gogu ni kiongozi wa Taifa la Magogu. Yaani mfalme wa taifa la Magogu. Kwahiyo tunaposoma, neno Gogu na Magogu, Ni sawa na kusema Farao na Misri, au Sulemani na Israeli.

Ndio maana tunasoma hapo katika Ezekieli 38:3… “useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe GOGU, mkuu wa Roshi, na Mesheki, na Tubali;”

Umeona hapo mstari wa 2, unasema Gogu mkuu wa…. Neno “mkuu wa” linaashiria ni kiongozi, hivyo Gogu ni jina la kiongozi kama vile Farao, au Sultani. Na Magogu ni Taifa hilo lenye nguvu ambalo linatawala mataifa mengine madogo madogo (Tubali, Mesheki na Roshi)

Sasa kama tulivyotangulia kusema huo mji wa Magogu haupo tena wala mkuu wake Gogu hayupo…Lilikuwepo enzi hizo, lakini sasa halipo tena, lakini huo unabii wa Ezekieli 38 bado haujatimia na ndio upo mbioni kutimia.. Ambapo ukisoma hiyo Ezekieli 38 yote, utaona inazungumzia Habari za vita vitakavyopiganwa Israeli, ambapo Mataifa mengi katika nchi ya mashariki ya kati (kwasasa ni mataifa ya kiarabu), yataungana pamoja na Gogu na Magogu wa sasa kuja kuivamia Israeli, lakini biblia inasema Gogu atashindwa vibaya sana Pamoja na mataifa hayo aliyoshirikiana naye.

Sasa huyu Gogu na Magogu, ni nani kwa sasa, kama mji huo ulishapotea kitambo?..

Gogu atakayeasisi vita hivyo vya Ezekieli 38, Uthibitisho wote unaonyesha kuwa si mwingine Zaidi ya Mkuu wa Taifa la URUSI .

Kwanini ni Taifa la Urusi, ndio linalofananishwa na Magogu na si Taifa lingine?.

Kwasababu ndio taifa lililopo kaskazini mwa Asia na ulaya, eneo lile lile Magogu walipokuwepo, pili ndio taifa lenye nguvu kijeshi kaskazini mwa Ulaya, mfano wa magogu wa mwanzo.

Hivyo Urusi ndiyo itakayotimiza unabii huu wa Gogu na Magogu, katika vita hii ambayo ipo mbioni kuanza.

Kumbuka Israeli hawakuwa taifa huru kwa takribani miaka 2500 tangu walipopelekwa Babeli miaka mia tano kabla ya Kristo, na hiyo ni kutokana na makosa yao. Lakini mwaka 1948 walirudi katika nchi yao na kuwa taifa huru linalojitegemea ili kutimiza unabii wa Isaya 11:11-12 na..

Ezekieli 39:21 “Nami nitauweka utukufu wangu kati ya mataifa, na mataifa wote wataiona hukumu yangu niliyoitekeleza, na mkono wangu niliouweka juu yao.

[22]Basi, nyumba ya Israeli watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, tangu siku hiyo na baadaye.

[23]Nao mataifa watajua ya kuwa nyumba ya Israeli walihamishwa, na kwenda kifungoni, kwa sababu ya uovu wao; kwa sababu waliniasi, nami nikawaficha uso wangu; basi nikawatia katika mikono ya adui zao, nao wakaanguka kwa upanga, wote pia.

[24]Kwa kadiri ya uchafu wao, kwa kadiri ya makosa yao, ndivyo nilivyowatenda, nami nikawaficha uso wangu.

[25]Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Sasa nitawarejeza watu wa Yakobo waliohamishwa, nitawahurumia nyumba yote ya Israeli; nami nitalionea wivu jina langu takatifu.

[26]Nao watachukua aibu yao, na makosa yao yote waliyoniasi, watakapokaa salama katika nchi yao wenyewe, wala hapana mtu atakayewatia hofu;

[27]nitakapokuwa nimewaleta tena kutoka kabila za watu, na kuwakusanya kwa kuwatoa katika nchi za adui zao, na kutakaswa kati yao mbele ya macho ya mataifa mengi.

[28]Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, kwa kuwa naliwahamisha, waende utumwani kati ya mataifa, na mimi nikawakusanya, na kuwaingiza katika nchi yao wenyewe; wala sitawaacha tena huko kamwe, hata mmojawapo;

[29]wala sitawaficha uso wangu tena; kwa maana nimemwaga roho yangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.”

Lakini unabii ulitabiri baada ya Israeli kurejeshwa, kutakuwepo na vita vikuu viwili ambavyo vitahitimisha mwisho wa dunia hii. Na moja ya vita ambayo ipo mbioni na maandalizi yako tayari ni vita hii ya Gogu na Magogu, na nyingine itakayomaliza kabisa historia ya dunia ni ile ya Harmagedoni (Ufunuo 16:16) ambayo itahusisha mataifa yote ya dunia kuungana na kwenda kupigana na Israeli, wakati huo unyakuo umeshapita siku nyingi.

Hii ni kuonyesha ni kwa jinsi gani mwisho ulivyokaribia sana!!, Bwana YESU alisema kwa mtini jifunzeni.

Mathayo 24:32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;

[33]nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.

[34]Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.

[35]Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Mtini umechipuka mwaka 1948. Na Bwana alisema “Amin, nawaambieni kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie” (kizazi kilichoshuhudia mtini kuchipuka yaani Israeli kuwa taifa huru).

Kumbuka mtini kibiblia unawakilisha taifa la Israeli (Soma Yeremia 24), na kizazi ni miaka 80-100.

Israeli ndio kalenda yetu, vita vinavyoendelea katika nchi ya Israeli ni ishara ya siku za mwisho. Ni maandalizi ya vita vya Gogu na Harmegodon kutukia.

Unyakuo unaweza kutokea kabla, au wakati au baada ya vita vya Gogu na Magogu.

Swali ni je! umejiweka tayari kumlaki Bwana Yesu mawinguni??

Kama bado unasubiri nini mpaka sasa? Hujui muda umekwisha na parapanda ipo karibu sana kulia, na watakatifu kunyakuliwa!!!

>Hebu tubu leo Mgeukie Bwana Yesu akuoshe dhambi zako ili uwe miongoni mwa watakaonyakuliwa moja ya hizi siku.

>Amua kuacha maisha ya dhambi na uvugu uvugu, acha udunia, acha huo usherati wa boyfriend na girl friend, acha huo usengenyaji, acha kujipodoa na kujipamba kama Yezebeli ni machukizo kwa Mungu, mwanamke acha kuvaa suruali, vimini, nguo za kubana, na mavazi mengine ya kikahaba, kijana acha kujichua/punyeto, acha kusikiliza miziki ya kidunia, acha kushabikia mipira na kucheza magemu na kubeti, acha uhuni, acha mambo yote mabaya.

YESU KRISTO ANARUDI MUDA WOWOTE!!

Tubu kiukweli ukweli na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la BWANA YESU KRISTO (Matendo 2:38).

Maran atha (Na uje Bwana Yesu).

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Vile vile ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *