JE! UNAO UZIMA WA MILELE?

Uncategorized No Comments

JE! UNAO UZIMA WA MILELE?

Siyo dhambi kuwa na nyumba nzuri, gari nzuri, biashara kubwa, elimu kubwa, mke/mume mzuri, watoto wazuri, na mafanikio yote ya hapa duniani, kwani biblia pia inakubaliana na mafanikio hayo..

3Yohana 1:2,9 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa, na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”.

Na pia wapo watu wa Mungu waliofanikiwa katika biblia kama wakina Sulemani, na hata sasa wapo watu wa Mungu wenye mafanikio mengi tu. Kwahiyo siyo dhambi kuwa nayo na kutafuta.

Lakini swali ni kwamba pamoja na mafanikio hayo yote uliyonayo au unayoyatafuta, je! unao uzima wa milele?

~Je! una uhakika Yesu akirudi leo utaondokanaye?

~Je! una uhakika kwamba ukifa leo utakuwa salama huko uendako?

Kama hauna huo uhakika.. fahamu kuwa hayo mafanikio unayoyatafuta/uliyonayo ni bure tu.

Itakufaidia nini ukipata hayo yote na kisha ukapata hasara ya nafsi yako!!

Marko 8:36 “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

Ndugu, tafuta kwanza uzima wa milele kisha hayo mengine yawe ya ziada.

Luka 12:29 “Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi,

[30]kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.

[31]Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.

Sasa uzima wa milele tunaupataje?

Marko 10:17 Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, NIFANYE NINI NIPATE KUURITHI UZIMA WA MILELE?

[18]Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.

[19]Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.

[20]Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.

[21]Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. ENENDA, UKAUZE ULIVYO NAVYO VYOTE, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; KISHA NJOO UNIFUATE.

[22]Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; KWA SABABU ALIKUWA NA MALI NYINGI.

Umeona jinsi ya kupata uzima wa milele. Sio kushika amri kumi tu, au kujiunga na kanisa Fulani, au kutoa sadaka nyingi..kanuni ni KUUZA VYOTE na kumfuata Yesu.

Uzima wa milele unapatikana kwa YESU KRISTO yule wa Nazarethi TU. Na sio vinginevyo.

Yohana 17:3 Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na YESU KRISTO uliyemtuma.

Kuuza vyote ambayo Bwana alimaanisha ni kuondoa vitu vyote moyoni.. ikiwemo mali, na kumbeba yeye pekee yake. Na ikiwa mtu atashindwa kutoa hivyo vitu itambidi akauze kabisa ili moyo wake usishikwe na kitu kingine.

Huyu ndugu, alitaka kupata uzima wa milele.. lakini asingeweza kupata mpaka atoe moyo wake kwa Bwana Yesu. Na kwasababu Bwana alimfahamu, alijua tatizo lipo katika vitu alivyo navyo, hawezi kutoa moyo wake..njia ya kumsaidia ni kumwambia akauze vyote alivyovishikilia, Lakini kwasababu alikuwa na mali nyingi hakuweza kufanya hivyo.

Huwezi kumfuata Bwana Yesu au kupata uzima wa milele ukiwa umebeba mali moyoni mwako au fedha, au biashara, au elimu, au mchumba, n.k sharti uuze vyote kisha umfuate Bwana.

Unapokuwa na vitu hivyo moyoni mwako, huwezi kumtumikia Bwana.. kwasababu unakuwa na mabwana wawili jambo ambalo ni ngumu kuwatumikia kwa wakati mmoja, vitu kama mali, fedha vinahesabika kuwa mungu/bwana mwingine. Hivyo ili upate uzima wa milele huna budi kuondoa vyote katika moyo wako, na ikiwa huwezi kuondoa basi kauze vyote, au wape masikini ili uweze kumtumikia Mungu/Bwana mmoja tu.

Mathayo 6:24 Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. HAMWEZI KUMTUMIKIA MUNGU NA MALI.

Na halikadhalika nenda kauze umaarufu wako ili upate uzima wa milele, kauze fashion ulizonazo, uza kiburi ulichonacho, uza marafiki wabaya, ikiwa ni simu inakukosesha kauze, ikiwa ni kazi acha, uza na mambo yote mabaya.

Ikiwa ni ulevi kauze..waachie walevi, ikiwa ni uasherati ni vivyo hivyo, ikiwa ni udunia agana nao. Uza vyote kisha mfuate Bwana Yesu ili upate uzima wa milele.

Swali ni lile lile je! unao uzima wa milele? 

Huwenda unayo dini nzuri, dhehebu kubwa au dogo, na huwenda umezishika amri kumi zote tangu utotoni, lakini moyoni mwako umeweka sanamu watu, umeweka mali kiasi kwamba unaweza ukazimia ukiibiwa, basi fahamu leo kuwa umebeba miungu na hivyo huwezi kupata uzima wa milele kwa Bwana Yesu..huna budi kuuza vyote kama huwezi kuondoa moyo wako huko.

Kwahiyo, leo umefahamu haya kwasababu Bwana anakupenda na hataki upotee..anataka apate uzima wa milele.

Yohana 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Amua leo kumfuata Bwana Yesu kweli kweli ili upate uzima wa milele. Usikubali kitu chochote kikuzuilie uzima wa milele iwe ni utajiri au umasikini usikubali; usikubali kitu chochote kichukue nafasi ya Mungu kwenye moyo wako iwe ni mtu Fulani au fedha usikubali.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho..Bwana Yesu yupo karibu kurudi na kuwachukua wateule wake kupisha hukumu kwa waovu.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *