
TOKA KATIKA GEREZA LA DHAMBI
Siku zote mtu anayeishi katika dhambi (ambaye hajaokoka), yupo katika kifungo cha uovu.
Matendo ya Mitume 8:23 “Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu”.
Na kama tunavyojua wafungwa wanafungwa gerezani ili watumikie vifungo vyao. Na kila mtu ana kifungo chake kulingana kosa lake.
Na halikadhalika katika roho kuna watu wapo vifungoni, wamefungwa katika magereza ya dhambi.
Isaya 42:22 “Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, WAMEFICHWA KATIKA MAGEREZA; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha”.
Kumbuka mtu anapokuwa katika dhambi anakuwa ni mtumwa wa dhambi, kama vile mtu ambaye yupo kifungoni akiitumikia kifungo chake.
Yohana 8:34 Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
Lakini kwa neema ya Mungu Kristo alikuja kututangazia uhuru wetu kutoka katika UTUMWA WA DHAMBI kama vile raisi anavyotoa msamaha kwa wafungwa na kuwatangazia uhuru wao.
Luka 4:18-19″ Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma KUWATANGAZIA WAFUNGWA KUFUNGULIWA KWAO, Na vipofu kupata kuona tena, KUWAACHA HURU WALIOSETWA,Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa
Kwahiyo injili ililetwa kwetu mahususi kwa kutuweka HURU mbali na dhambi.
Lakini cha kustaajabisha na kuhuzunisha ni kwamba pamoja na Kristo kututangazia uhuru bure, kuna watu waliokataa uhuru wao kwa makusudi angali wakijua kabisa wapo kwenye utumwa na wangepaswa wawe huru, lakini wakapenda kumtumikia bwana wao shetani katika dhambi zao kuliko kumtumikia Mungu.
Yohana 3:19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.
Hebu jiulize leo hii umeshaisikia injili mara ngapi, umehubiriwa uache uzinzi mara ngapi ewe kijana ewe binti? Na hutaki kusikia, usijue kuwa hiyo ni habari njema kwa wafungwa wote.
Umehubiriwa utubu dhambi zako mara ngapi? lakini umekuwa wa kwanza kufanya mizaha? umehubiriwa uache ulevi mara ngapi? unavuta sigara, unaangalia pornoghaphy, unafanya mustarbation, binti unasagana, umekuwa shoga kijana, unaenda kwa waganga, unajifurahisha katika anasa na miziki ya kidunia,
Mwanamke unavaa suruali, vimini, unapaka rangi kucha, kijana unanyoa mitindo isiyofaa na kusuka nywele ,na tatoo kwenye mwili wako, wanawake usengenyaji na umbea, mtukanaji, unajichanganya na watu waovu kwa jinsi isivyopasa, unachati nao mambo maovu, huku ukijua kabisa watu wanaoyafanya hayo wataishia katika jehanum ya moto, Lakini hutaki kutoka katika hilo GEREZA.
Fahamu leo kuwa ule mwaka wa maachikio, kipindi cha neema kitafungwa muda wowote na hakuna mtu atakayeweza kuokolewa tena, na hata ukifa leo katika hilo gereza utashuka huko kuzimu katika yale magereza ya milele, huko hakuna kuachiliwa tena.
Ni heri leo ukatii huu wito unaokuita kila siku utoke katika gereza la dhambi, na unatii kwa kuamua kutubu dhambi zako na kumaanisha kabisa kuziacha na kumfuata Bwana Yesu.
Kumbuka muda wa kuamua kuokoka ni leo na sio kesho au baadaye, sio mpaka umalize shule au upate ajira, na sio mpaka uwashirikishe ndugu au marafiki, jiokoe nafsi yako mwenyewe toka katika gereza la dhambi.
2Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
Hukumu ipo karibu na unyakuo umekaribia mno.
Maran atha
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.