
TEMBEA KATIKA WAKATI WA MUNGU.
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maneno ya uzima.
Neno la Mungu linasema..
“Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.(Mhubiri 3:1)
Kila kitu Mungu ameiweka katika wakati wake, hivyo ni vizuri kufahamu wakati wa Mungu katika maisha yako ili usijilazimishe kutembea katika wakati wa wanadamu.
Wakati wa wanadamu ni wakati ambao wanadamu wamejipangia maisha yao wenyewe kwa kuzifuata desturi na taratibu zao.
Lakini upo wakati wa Mungu pia kwa watoto wake, hivyo ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu ni vizuri kutembea katika wakati wa Mungu na sio kuangalia desturi za wanadamu.
Fahamu kuwa maisha yako yamefungwa katika wakati wa Mungu, kinachohitajika ni kuwa na subira tu. Kwasababu Mungu anakujua vyema na ameshaipangilia maisha yako tangu ulipozaliwa.
Kwa mfano wewe ni kijana au binti, na hujaoa/hujaolewa kwa muda mrefu kidogo, na ukiangalia vijana wa rika lako wanaokuzunguka au unaowafahamu wameoa/wameolewa..umebaki wewe mwenyewe tu, usianze kufikiri labda wewe una shida, au una mikosi.. fahamu kuwa wakati wako unakuja ambao Mungu aliye Baba yako ameiweka.. hivyo usijilazimishe kutembea katika wakati wa wanadamu. (Kuwa na uvumilivu huku ukizidi kuishi maisha ya utakatifu).
Vivyo hivyo na mambo mengine kama kazi/ajira, watoto n.k tembea katika wakati wa Mungu. Usiangalie maisha ya watu wa dunia hii ambao mwisho wao ni uharibifu.
Na halikadhalika kama ni mtumishi wa kweli uliyeitwa kuhubiri injili ya kweli (injili ya utakatifu), usiangalie watumishi wengine walioinuliwa kihuduma, ukadhani wewe una bahati mbaya au Mungu hayupo na wewe, fahamu kuwa wao nao walikuwa kama wewe, wakavumilia na kuwa waaminifu mpaka wakati wa Mungu ulipowadia wakajikuta wapo hapo walipo. (Nazungumzia watumishi wa kweli).
Hivyo ni suala la muda tu, kikubwa ni kuwa mwaminifu katika kile kidogo ulichopewa sasa, endelea kufanya kazi ya Mungu kwa bidii bila kuangalia hali yako kiuchumi, au kielimu. Upo wakati wa Mungu katika huduma yako.
Na mambo mengine yote ni vivyo hivyo, amani ya Kristo iamue ndani yako katika kile unachokifanya sasa, ikiwa una amani fanya kwa bidii maana ndio wakati wa Mungu katika jambo hilo, kama upo shuleni soma sana kwa bidii huo ndio wakati wako, haujui kesho utakuwa wapi.
Mhubiri 3:1-8Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
[2]Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa;
[3]Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
[4]Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;
[5]Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
[6]Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;
[7]Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;
[8]Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.
11 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho”.
Lakini kama hujaokoka na kufanyika mtoto wa Mungu, fahamu kuwa upo wakati wa kuokoka pia, na sio wanadamu wameiweka..bali ni Mungu mwenyewe. Hakuna mtu anayejiamuria tu kuwa ataokoka kwa wakati wake au atakapotaka, kama vile asivyoweza kujiamuria afe kwa wakati Fulani. Ndivyo ilivyo kwa habari ya wokovu, biblia inasema..
2 Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
Umeona, kuna wakati wa kukubalika na wakati usiokubalika, sio kila wakati unaweza kuokoka kwa kujiamuria tu. Wakati wa kuokoka ni sasa hivi unaposoma ujumbe huu na kusikia sauti ya Mungu ndani yako. Usiipuuzie na kusema nitaokoka tu, nitaokoka tu. Wakati uliokubalika ni sasa, amua kuokoka leo..kifo ni wakati wowote usioijua na unyakuo pia ni muda wowote.
Bwana Yesu anarudi.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.