Kuwa Mtu Chunguza-chunguza na tafuta-tafuta.

Biblia kwa kina No Comments

Kuwa Mtu Chunguza-chunguza na tafuta-tafuta.

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Mtu wa kuchunguza-chunguza ni anatafsirika kwa namna gani?

Mtu anayechunguza na kutafuta kuhusu mambo ya rohoni mara nyingi ni mtu anayehisi kiu ya kiroho au anayetafuta maana ya maisha, uelewa wa kiroho, na uhusiano wa kina na Mungu au ulimwengu wa kiroho

Kama Mkristo uliemwamini Yesu Kristo ni muhimu sana ukawa na tabia hii ndani yako ambayo walikuwa nayo manabii.

 1 Petro 1: 10  Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.

11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.

Ukweli ni kwamba manabii walitabiri/kutoa habari za Kristo kwa sehemu kubwa sana Roho alipokuwa akishuka walitabiri mambo makuu mno kuhusu Kristo.  Lakini ajabu ni kwamba ijapokuwa walikuwa wanatabiri na kuonyeshwa wakati mwingine lakini HAWAKUWA WANAELEWA.

Manabii wote walimtabiri Kristo anazaliwa lakini hawakuwa wanafahamu ni kwa namna gani? Wakati gani? Atakuwa mtu wa namna gani?, watu watapataje ukombozi,tutahesabiwa haki kwa imani,kuondolewa kabisa dhambi zetu(si kufunikwa kama ilivyokuwa kwao)nk haya yote hawakuwa wanafahamu kabisa japokuwa walitabiri.

Sasa walifanikiwa kujua kwa sehemu ndogo sana japo walitamani kujua zaidi lakini haukuwa mpango wa Mungu wafahamu kila kitu bali aliruhusu wafahamu kwa sehemu na sehemu nyingine ambayo ni utimilifu wote uje ufunuliwe kwetu kwa jinsi ya mwili kupitia Kristo Yesu.

Sasa kitu kilichofanya wakafahamu kwa sehemu ni kwa sababu ya tabia waliyokuwa nayo.. maandiko yamesema hapo.  Walikuwa na tabia ya KUTAFUTA – TAFUTA na KUCHUNGUZA-CHUNGUZA. walikuwa ni watu wenye kiu na shauku kubwa sana ya kufahamu juu ya wokovu na neema tuliyoipata katika Kristo Yesu.

Na ndio maana wakafanikiwa kwa sehemu kidogo kufahamu.  Maana yake kama wasingelikuwa na tabia hii ndani yao basi wasingelifahamu chochote kabisa. Wangeliishia tu kukaliwa na Roho na kutabiri na wasielewe chochote.

Maana neema ilikuwa haijafunuliwa dhahiri kabisa katika kipindi chao.

Ikiwa sisi ambao neema hii imetufikilia IMETUPASAJE? sisi kila kitu kiko wazi tunae Roho Mtakatifu anaetufunulia kweli yote maana yake inatupasa kuwa zaidi ya wao walivyokuwa.

Lakini matokeo yake Wakristo wengi wanasema wameokoka lakini hawajui hasa ukombozi au neema tuliyoipokea. Wapo tu wamekaa na wameridhika na hali yao miaka nenda rudi(huenda na wewe ni mmoja wao). Wakristo wengi hawamfahamu kabisa Kristo, hawajui haki tuliyonayo katika Kristo,Mamlaka tuliyonayo katika Kristo,nguvu tulizonazo katika yeye nk.

Na ndio maana Leo hii Wakristo wengi wanasumbuliwa na nguvu za giza! Wanakimbilia mafuta ya upako,maji ya upako nk.

Wakati fulani niliwahi kuongea na mtu mmoja ambae ameokoka lakini akaniambia “ Mtumishi nasumbuliwa na nguvu za giza napambana nazo na ninaomba tushirikiane katika hili kufukuza mapepo/wachawi ndani ya nyumba yake..”

Ukweli nilitafakari kwa sehemu nikafahamu ni Elimu ndogo sana hajaipata nayo ni kufahamu yeye ni nani?.

Usipokuwa ni mtu wa kutafuta tafuta/kuchunguza-chunguza ni madhara gani yatakupata. Na nini ufanye?

1.Kuangamia.

Maandiko yanasema..

Hosea 4:6“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.”

Kuokoka haitoshi peke yake ili uweze kuwa salama lazima uwe na maarifa mengi kuhusu Mungu.  Ni sawa na kujua kusoma haitoshi kusema umeelimika bali unapokuwa na maarifa mengi nje na kujua kusoma ni muhimu sana.

Leo hii wewe ni MKristo unaeshinda tik tok,Instagram, snapchat, ukiangalia umbea tu.. uko busy na matamthilia yenye maudhui ya kizinzi zinzi tu. Kusoma biblia ni jumapili kwa jumapili,kusikiliza mhubiri ni mpaka jumpili unategemea vipi hapo kuwa na maarifa?

Fahamu “kuwa na maarifa sio bahati au maarifa hayaji tu yanahitaji ujifunze kuwa na maarifa ni mchakato endelevu wa kujifunza.”  

Wakati mwingine utakaa unaomba Mungu kila siku akupe maarifa ndugu yangu kama husomi vitabu hilo sahau.

Wekeza muda wako mwingi katika kujifunza. “Maarifa hayaji kwa bahati mbaya ni Mchakato “

Kuwa ni mtu wa kujifunza kila siku nakuhakikishia utaanza kuona maarifa mengi na hekima vitaanza ndani yako..

2.kuendelea kuwa mtoto mchanga. 

Usipokuwa ni mtu wa kuchunguza-chunguza na kuutafuta-tafuta ndugu katika roho utaendelea kuwa ni mtoto mchanga sio mkomavu mwisho wa siku unachukuliwa na upepo wa mafundisho ya kila namna ya uongo.

 

Waefeso 4:14“ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”

Ni rahisi sana kwenda katika njia ya udanganyifu kwa sababu unakuwa huna tofauti na mtoto mchanga kila kitu utapokea kwa sababu huwezi kupambanua.

Kuwa kama Danieli alikuwa ni mtu wa kusoma sana vitabu na kuchunguza-chunguza sana akafanikiwa kujua muda wa wao uliosalia wa kutoka utumwani.  Danieli asingelikuwa ni mtu wa kujifunza asingelifahamu muda uliokuwa umebaki wa wao kuendelea kukaa utumwani.

Danieli 9:2″katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.”

Usiwe ni Mkristo wa jumapili kwa jumapili kanisani kuwa ni Mkristo amabe una faida katika ufalme wa Mungu. Usiwe msindikizaji.

Kuwa siriazi na wokovu wako tuko katika nyakati za Mwisho hizi. Fanya imara zaidi uteule wako.. ikiwa manabii walifunuliwa kwa sehemu wewe unae utimilifu wote.

1 Petro 1:12 “Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.”

 

Unaona hapo?, Walifanikiwa hata kufahamu kuwa hata wokovu haukuwa kwa taifa moja tu bali kwa wote.

Ndugu usipochukua hatua ya kujifunza zaidi nahakika hutaweza kukua wala kupona na hila za adui

Anza leo kuwa mtu wa kutafuta tafuta na kuchunguza-chunguza.

Ubarikiwe sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *