UFAHAMU UMUHIMU KWA KWENDA KANISANI/IBADANI?

Biblia kwa kina No Comments

Waebrania 10:25“wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. 

Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Umewahi kujiuliza vyema na kutafakari kwa kina swali hili..” kwa nini ninakwenda kanisani kila siku jumapili, Jumatano, ijumaa nk”

Umewahi kutafakari ni kwa nini? Au unaenda kama desturi yako au sehemu tu ya jambo unalolifanya katika maisha yako?

Wakristo wengi ukiwauliza swali hili hawajui namna ya kulijibu. Na hiyo yote ni kwa sababu hawatambui kwa nini wanakwenda. Hili ni jambo ambalo si zuri katika maisha ya mwamini.

Wengi watakwambia. “Naenda kumwambudu Mungu” au “ Naenda kumtumikia Mungu” au “Naenda kumuomba Mungu” nk ni majibu ambayo ni sahihi kabisa lakini sio katika usahihi wote.kwa Mkristo anaetambua umuhimu huo.

Na ndio maana watu wengi wanakwenda kanisani kila jumapili, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa wakati mwingine jumamosi lakini hakuna mabadiliko yoyote katika maisha yao bado ni wale wale wakitoka humo kila kitu walichokisikia kinabakia kwenye siti zao makanisani.

Kila siku tunasikiliza maneno ya Mungu lakini je?

Ni kipi unachokisikia maana kila mtu anasikia lakini utofauti uko katika kile tunachokisikia na unachokisikia kina uzito gani kwako au kina maana gani kwako?”

Umewahi fikiria juu ya mambo haya? Ni Muhimu sana kwa Mkristo unaetaka kukua kiroho siku baada ya siku. Bwana Yesu anasema..

Marko 4:24“Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.

Sasa tuangalie nini maana ya kanisa?

Kama tunavyofahamu Kanisa ni kusanyiko la waamini waliomwamini Yesu Kristo na kusamehewa makosa yao. Au kwa maana nyingine ni walioitwa. Kanisa si jengo bali ni mwili wa Kristo unaokutanika.

MAMBO MAKUU MANNE(4) YA KUFAHAMU KWA NINI UNAKWENDA KANISANI.

Mambo haya yaweke kwenye akili yako daima kila unapokwenda kukusanyika katika makusanyiko yote ukienda na fahamu ya mambo makuu haya manne yatakusaidia katika kupiga hatua zaidi ya ukuwaji wa Kiroho. 

1.KUJENGWA.

Tambua unapokwenda kanisani unakwenda kujengwa. Mahali ambapo ulikuwa bado hujajengeka unakwenda kujengwa. Mahali ambapo hujasimama na kupafahamu juu ya Kristo Yesu basi tarajia unakwenda kukutana na kitu kipya. Weka kwenye fahamu zako siku zote hili jambo litakusaidia sana. Na unajengwa kwa kupitia fundisho la kweli la Kristo.

Jua na Amini neno la Mungu siku zote ni hai wala si sanamu kwamba ukilisoma leo ndio lile lile kila siku neno la Mungu ni jipya na linafunuliwa kwetu kwa namna ya tofauti na kipekee kwa kila mmoja mmoja wetu.

Waebrania 4:12“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

2.KUTENGENEZWA.

Fahamu kila siku unapokwenda katika kusanyiko unakwenda kutengenezwa. Siku zote ili kitu kitengenezwe ni lazima kiwe kimeharibika mahali fulani. Hivyo fahamu wewe na mimi kama wanadamu tunahitaji kila siku matengenezo kuna maeneo mengi ambayo hatujaimalika au kusimama vizuri. Huenda tumekuwa wabaya katika maeneo tofauti tofauti. Wakati mwingine kuna tabia zimeanza kuota ndani yetu ambazo si nzuri.

Hivyo tunapokwenda katika ibada/kanisani tunakwenda kutengenezwa kila mmoja katika eneo fulani alipo na udhaifu ili tuimarike tupige hatua mbele zaidi.

Hivyo siku zote nenda na ufahamu huu kila siku utaona kuna mahali fulani Mungu anataka upalekebishe ili tuendelee kupiga mbio zaidi kwa sababri.

Ziko dhambi zituzingazo kwa upesi na hizi zinahitaji neema ya Bwana kila siku ili kuepukana nazo.

Waebrania 12:1“Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,

Kila siku tamani kutengenezwa mahali palipo bomoka. 

3.KUTIWA MOYO.

Katika maeneo ambayo umekata tamaa na umechoka kabisa weka kwenye akili yako hili jambo kwamba unakwenda kutiwa moyo na utaendelea mbele zaidi.

Amini kupitia ibada hiyo Mungu atasema na wewe na kukutia nguvu tena. Mungu siku zote hasemi uongo wala si mwanadamu mwenye kubadilika badilika ameahidi na amesema..

Isaya 40:31“bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Lakini leo hii Wakristo wengi wanakwenda katika makusanyiko/kanisani wanatoka na kurudi majumbani wakiwa bado wamevunjika moyo,Hawana tumaini, wamekata tamaa nk hii yote ni kwa sababu hawajafahamu vyema wanakwenda katika kusanyiko kufanya nini..?

4.KUKUMBUSHWA.

jambo la Mwisho kabisa ni kukumbushwa. Fahamu hili jambo utakutana nalo ibadani usilichukulie kawaida maana itakugharimu. Sisi kama wanadamu tunatabia ya kusahau na hivyo tunahitaji kukumbushwa. Na ndio maana Leo hii mwanafuzi yoyote ni lazima awe na mahali pa kuandika ili asije sahau ili baadae ajikumbushe yale yote aliyofundishwa.

Kusahau ni udhaifu alioumbwa nao Mwanadamu yoyote yule lakini jiulize je unapokumbushwa unasimama na kutenda? Lengo la kukumbushwa sio kutikisa kichwa au kusema “nilisahau kumbe…” halafu baada ya hapo hufanyii kazi si hivyo.

Unaposoma maandiko Roho Mtakatifu atafanya kazi ya kukumbusha maana ni jukumu lake kufanya hivyo.

Yohana 14:26“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

Amini na kuwa na ufahamu huu siku zote akilini mwako kuwa ni lazima Roho Mtakatifu atakukumbusha kupitia kinywa cha Mchungaji,Mzee wa kanisani, mpendwa mwenzako,kupitia maandiko unaposoma,au atasema na wewe ndani yako haya yote lazima yafanyike moja wapo.

Hivyo ukiwa makini unapokwenda katika kusanyiko jua na ni hakika utakutana nayo ni wewe kuyafanyia kazi tu. Sote tujenge nyumba juu ya mwamba na si juu ya mchanga.

Maana kujenga juu ya mwamba ni kusikia na kufanyia kazi. Kujenga juu ya mchanga ni kusikia na kutokufanyia kazi.

Ubarikiwe sana.    

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *