BASI, JIANGALIENI MIOYO YENU ISIJE IKALEMEWA
Luka 21:36 Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
Shalom, Jina kuu la mwokozi wetu Yesu libarikiwe daima.
Je! Umewahi kuitafakari kwa utulivu hii kauli ya Bwana aliposema ”jiangalieni mioyo yenu isije ikalemewa”, yapo maneno aliyoyasema Bwana ambayo ukiisoma kwa haraka haraka unaweza ukadhani ni maneno ya kawaida tu kama mengine ya siku zote.
Kwamfano Bwana aliposema ”viuno vyenu viwe vimefungwa na taa zenu ziwe zinawaka” kwa haraka haraka bila kutafakari ni rahisi kuona hiyo kauli ni ya kawaida tu kama hii ambayo Bwana alisema pia “Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwani;
Tofauti ya kauli hizo, ni kwamba moja ni ya tahadhari na nyingine ni ya ushauri, sasa ushauri unaweza usiwe na uzito sana kuliko ile ya tahadhari japokuwa zote ni muhimu kutii. kwanini?
Ni kwasababu ushauri, mtu anaweza akakubaliana nayo na akafanyia kazi ikamletea faida, lakini pia anaweza asiifuate huo ushauri na asipate adhabu kwa yule aliyemshauri japokuwa kuna kitu atakosa.
Lakini tukija kwenye swala la tahadhari, mlengwa ni lazima atii na achukue hiyo tahadhari vinginevyo atapata shida.
Sasa tukirudi kwenye ile kauli ya Bwana, aliposema”jiangalieni mioyo yenu isije ikalemewa” maana yake wote ambao ni walengwa (wanafunzi wake) wanapaswa wachukue hiyo tahadhari, kwani wakijisahau tu na mioyo yao ikalemewa basi, watapata hadhara kubawa sana (Kumbuka sio miili ni MIOYO).
Na hadhara yenyewe ni kwamba ILE SIKU itawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
Sasa swali ni siku gani hiyo ambayo Bwana alinena kuwa itawajilia watu ghafula kama mtego unasavyo?
Ili tuelewe vizuri hebu tusome tena maneno ya Bwana sehemu nyingine, Bwana alisema..
Mathayo 24:36 Walakini habari ya SIKU ILE na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.
[37]Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
[38]Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
[39]wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
[40]Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
[41]wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
[42]Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
[43]Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
[44] KWA SABABU HIYO NINYI NANYI JIWEKENI TAYARI; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Umeona hapo, ipo siku moja isiyokuwa na jina ambayo inakuja mbeleni, Nabii Zekaria aliona hiyo siku kabla hata Bwana Yesu hajanena.
Zekaria 14:6 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
[7]lakini itakuwa SIKU MOJA, iliyojulikana na BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.”
Siku hiyo itaitwa tarehe Fulani ya Mwezi Fulani na mwaka Fulani.
Siku hiyo upande mmoja wa dunia utakuwa ni mchana na mwingine usiku, siku hiyo watu watakuwa wanapika, wengine wanafanya biashara, wengine wanajenga, wengine wapo katikati ya harusi, wengine watakuwa safarini, wengine watakuwa misibani, wengine mashuleni, Wengine watakuwa wamelala, wengine wapo kanisani, wengine watakuwa mahospitalini, wengine mahakamani, wengine wanacheza mpira, wengine wapo disko. Wengine bungeni, wengine magerezani,wengine wanapanga mipango na mikakati ya namna ya kuimarisha vipato vyao na kazi zao n.k…Siku hiyo ndio itakuwa mwisho wa utendaji kazi wa Roho Mtakatifu duniani kwa watu wa mataifa…siku hiyo utapita kitu kinachoitwa UNYAKUO.
Wakati watu wengi watakuwa hawaelewi chochote, kufumba na kufumbua baadhi ya watu watatoweka, wachache sana…Tetesi tetesi chache zitasikika huko na huko kwamba kuna baadhi ya watu wamepotea katika mazingira ya kutatanisha, lakini kutokana na kwamba dunia imelewa na kulemewa na mambo mengi, wengi watasema ni habari za kuzusha, kwani imezoeleka kusikika unyakuo umepita na unakuta hakuna lolote lililotokea. Watasema mwaka 2000 ilikuwa hivyo hivyo, walitabiri na hakuna kilichotokea…mwaka 2002 ikawa hivyo hivyo, wakasema unyao umepita na hakuna lolote, kadhalika mwaka 2012…Na leo tena uzushi mpya umezuka.
Wakati mamia na maelfu ya watu wanapuuzia habari hizo na kuona ni habari za uzushi, upande wa pili kutakuwa na uchungu na vilio kwa wale waliowashuhudia wenzao wakinyakuliwa mbele ya macho yao, wale waliokuwa wanalima pamoja ghafla jirani anatoweka mbele yake, wale ambao walikuwa wamelala na wenzao katika chumba kimoja ambacho kilifungwa na makomeo kwa ndani, na walipoamka kwa ghafla wakakuta hawapo, huku milango bado imefungwa vile vile kwa ndani, wale ambao walikuwa wapo ibadani pamoja kanisani na ghafla wenzao wamepotea, wale ambao wamemwona mtu Fulani kaketi mahali Fulani na kufumba na kufumbua katoweka. Hao ndio watakaoelewa uchungu wa kuachwa. Watalia sana na kuomboleza lakini haitasaidia.
Siku hiyo utakapoona mwanao hayupo, dada yako aliyekuwa ameokoka hayupo, mchungaji wako hayupo, na wewe umeachwa! Itakuwa ni uchungu kiasi gani?. Ukitazama ni masaa machache tu nyuma umetoka kupokea rushwa, ukitazama ni masaa machache tu nyuma umesikia mahubiri ya kukuonya na ulimwengu ukakataa. Ukitazama ni wiki chache tu nyuma uliota ndoto inayokuonya kwamba hizi ni siku za mwisho ukapuuzia. Masaa machache tu ulisikia mahali panazungumziwa habari za unyakuo.
Ukitazama ni siku chache tu nyuma ndio ulianza kupoa, utajisikiaje? Ukitafakari sasa wenzako wanafutwa machozi mbinguni na wewe umebaki ukingojea dhiki kuu na chapa ya mnyama na ziwa la moto milele?, ukitafakari ni disko ndio iliyokuponza, mke au mume unayeishi naye ndio aliyekuponza, binti/kijana unayetembea naye ndiye aliyekuponza, utafutaji mali uliopindukia ndio iliyokuponza, miziki ya kidunia, na tamaa ndivyo vilivyokuponza kuikosa mbingu, utakuwa katika huzuni kubwa kiasi gani.
Ndugu hiyo siku inafika, labda ni leo, au kesho au kesho kutwa hakuna aijuaye! Lakini ipo karibuni sana biblia inasema hivyo…
Bwana Yesu alisema..
Mathayo 24:36 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.
37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
38 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
39 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu
43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.”
Sasa, tukijua hayo, basi sisi kama wanafunzi wake, hatuna budi kujiweka tayari kwa kwa ajili ya siku hiyo, hatuna budi kujiangalia mioyo yetu isije ikalemewa na ULAFI, NA ULEVI NA MASUMBUFU YA MAISHA HAYA.
Kumbuka ulafi na ulevi unaozungumziwa hapo sio ule wa kula sana na kunywa pombe maana watakatifu hawawezi kuwa katika hali hiyo, bali ulevi unaozungumziwa hapo ni ule wa kulewa na mafundisho potofu na ibada ya sanamu (Ulevi wa rohoni).
Wewe kama mtakatifu ambaye unatarajia kwenda kwenye karamu ya Bwana iliyo karibu, katika siku hizi chache tuliobakiwa nazo, hatuna budi kujiangalia mioyo yetu, hatuna budi tuwe na tahadhari na mambo ya dunia,..
Kama mkristo uliyeokoka kweli kweli, huna budi kukaa mbali na anasa na tamasha za kidunia, ni lazima ujitenge na vitu vya kidunia, ni lazima uchuje vitu vinavyoingia kwenye moyo wako, angalia jinsi usikiavyo na unavyoenenda.
Je! moyo wako upo kwa Bwana asilimia mia kweli? Je! Ni aina gani ya mafundisho unayapenda?
Tunaishi ukingoni mwa nyakati, siku ya unyakuo imekaribia mno, wewe ambaye upo nje ya wokovu, sijui unasubiri nini mpaka sasa na kila siku unasikia injili? Au labda ni kiburi ndiyo kinakufanya usimpokee Yesu kweli kweli na kuachana na maisha ya dhambi na ya kuupenda ulimwengu. sikia basi, Neno la Mungu.
Malaki 4:1 Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; NA WATU WOTE WENYE KIBURI, NAO WOTE WATENDAO UOVU, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.