KILA MMOJA WETU ANAWAJIBU WA KUMTUMIKIA MUNGU. 

Biblia kwa kina No Comments

KILA MMOJA WETU ANAWAJIBU WA KUMTUMIKIA MUNGU. 

Watu wengi wanadhani kumtumikia Mungu ni kazi ya watu Fulani, labda walioitwa mahususi kwa ajili hiyo.

Na wengine wanafikiri hawawezi kumtumikia Mungu kutokana na sababu mbali mbali, mfano kutokuwa na elimu ya kutosha, kutokuwa na fedha, au kwasababu ya udhaifu waliyonayo. Lakini leo natumai utapata kitu katika somo hili na kama ulikuwa na mawazo hayo, basi ufahamu wako utabadilika.

Ukweli ni kwamba kila mtu aliyezaliwa mara ya pili (aliyeokoka) anawajibu wa kumtumikia Mungu bila kujalisha udhaifu wake au mazingira Fulani.

Utauliza inamaana hata mtu mwenye matatizo ya kuona, au kusikia au kuzungumza n.k anaweza kumtumikia Mungu?

Jibu ni ndiyo kabisa, vipofu, viziwi, viwete wanawajibu wa kufanya kazi ya Mungu bila kujalisha udhaifu wao. Maana yake udhaifu aliyonayo mtu sio kigezo cha kutomtumikia Mungu.

Hebu tujifunze kwa mifano ya viumbe vilivyoumbwa na Mungu na jinsi wanavyofanya kazi yao na kufanikisha bila shida pamoja na kuwa ni dhaifu katika baadhi ya sehemu.

Ndege :Ndege ni viumbe visivyo na mikono lakini wanatengeneza viota vyao (nyumba) kwa ustadi mkubwa sana kuzidi hata mwanadamu mwenye mikono miwili. Tazama picha hapo chini

 

Mchwa: Hawa ni wadudu wa ajabu sana, mchwa hawana macho lakini wanaweza kutengeneza mlima mkubwa sana, na wanabidii sana katika kazi yao.

Konokono: Huyu ni mdudu ambaye hana meno lakini anaweza kutafuna mifupa migumu..jambo ambalo mnyama kama ng’ombe pamoja na meno yake makubwa hawezi kufanya hivyo..

Hizi ni baadhi ya mifano tu halisi lakini ipo mifano mingi, Na Bwana Yesu alisema tuwaangalie ndege na viumbe vingine ili tujifunze uweza wa Mungu jinsi ulivyo mkuu. Hii ikiwa na maana kuwa na kiungo Fulani katika mwili au kutokuwa nayo sio sababu ya kumtumikia au kutomtumikia Mungu. Nyoka hana miguu lakini anakimbia zaidi kuliko jongoo mwenye miguu mingi lakini hawezi kukimbia.

Ni kweli ukiwa na viungo vyote au kipato kizuri, au maarifa mengi itakurahisishia kufanya kazi ya Mungu lakini pia hata yule ambaye hajapewa hivyo naye anaweza kumtumikia Mungu kwa kadri ya neema aliyopewa..na kitakachotofautisha dhawabu kule kwa mtu na mtu ni kiwango cha neema mtu aliyopewa na jinsi alivyotumia na wala sio upako aliokuwa nayo au umaarufu wake au sababu nyingine yoyote.

Kwahiyo kumbe kasoro zetu hazihusiani na sisi kukidhi vigezo vya kuhubiri Neno la Mungu!, au kumtumikia Mungu kwa namna yoyote ile..maana yake ni kwamba uwe mrefu, uwe mfupi, uwe unajua kuongea au hujui kuongea vizuri, uwe na kigugumizi, uwe mzungu, uwe mwafrika, uwe albino, uwe kiziwi, uwe kipofu, uwe huna miguu, uwe huna mikono, uwe maskini, uwe tajiri, uwe hujui kusoma, uwe mtu mdogo kabisa katika jamii, uwe mtu mkubwa.. uwe yoyote yule uwazaye kuwa, maadamu unaitwa MWANADAMU!. Basi umeshafuzu kuwa na uwezo wa kulibeba Neno la Mungu na kuwapelekea wengine kwa karama uliyopewa.

Kwahiyo usikubali kusikiliza uongo wa shetani ambao unakukatisha tamaa kwenda kuhubiri injili..Kama husikii vizuri, wewe hubiri hivyo hivyo, yule unayemhubiria akikuuliza swali sogea karibu msikilize tena na tena, ukiona bado humsikiI, wewe endelea mbele..usianze kuutafakari udhaifu wako…kwasababu hata yeye wakati huo atakuwa hautafakari udhaifu wako!… na pia hatakuchukia ila lile Neno utakalomwambia hata kama ni moja tayari ni Nguvu ya Mungu..na ni mbegu..

Hivyo usitafute sana ujuzi wala utaalamu katika kwenda kulitangaza Neno la Mungu…au asianze kusema mimi sijui kuongea vizuri nina kigugumizi, sioni vizuri, sina elimu, sina vifaa vya kuhubiria, sina hiki na hiki. Wewe Tafuta Roho Mtakatifu. Kisha itumie karama yako Mungu aliyokupa.

Mwanamke mmoja mashuhuri anayeitwa Fanny Crosby alizaliwa akiwa mzima lakini baada ya wiki mbili akawa kipofu, aliishi duniani katika hali hiyo hiyo ya upofu kwa muda wa miaka 95, lakini hakuacha kutafuta mahali ambapo angemtumikia Mungu licha ya kuwa alikuwa kipofu, alifanikiwa kuandika nyimbo zaidi ya 8,000, katika kipindi hicho cha karne ya 19, akajulikana kwa jina la malkia wa nyimbo za injili, na mwimbaji kipofu, moja ya tenzi mbili muhimu ambazo mpaka leo hii unazijua na kuziimba “Usinipite Mwokozi” na “Ndio dhamana Yesu wangu” pengine ulikuwa hujui ziliimbwa na huyu mama kipofu, na kwa kupitia uimbaji wake, na kuwahubiria wengine alifanikiwa kuwavuta watu wengi kwa Kristo.

Samsoni alitobolewa macho yake lakini baadaye alimuomba Mungu na Mungu akamtia nguvu tena..akawaua maadui zake wengi zaidi hata ya wale waliowaua wakati ana macho.

Waamuzi 16:28 ”Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.

[29]Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto.

[30]Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. BASI WALE WATU ALIOWAUA WAKATI WA KUFA KWAKE WALIKUWA WENGI KULIKO WALE ALIOWAUA WAKATI WA UHAI WAKE.

Naye Yonathani ilifika kipindi taifa lake la Israeli limezungukwa na maadui, na taifa nzima halikuwa na silaha lakini yeye pamoja na mtumishi wake waliwaendea maadui zao kwa siri na Bwana akafanya wokovu mkuu kupitia watu wawili tu wasio kuwa na nguvu kwasababu BWANA haokoi kwa wingi au uchache.

1Samweli 14:6, “Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.

[11]Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania watoka katika mashimo walimojificha!

[13]Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake.

Haitoshi kuleta habari za Daudi na Goliathi, lakini pia kwa shujaa Yaeli aliyemua jemedari wa vita adui wao kwa pigo moja tu la nyundo kichwani soma Waamuzi 4:21, pia muangalie shujaa Shamgari aliyewaua Wafilisti 600 maadui wa Israeli kwa fimbo ya kuswagia ng’ombe tu (Waamuzi 3:31). Na mashujaa wote wa imani..hawakuangalia udhaifu au mazingira kufanya kazi ya Mungu.

Je! Unaitumiaje neema uliyopewa? Biblia inasema “Mwenye kitu atapewa na kuongezewa tele, lakini asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa”. (Mathayo25:29)

Hivyo kila mmoja wetu anapaswa kumtumikia Mungu na kile Mungu alichokiweka ndani yake kuhakikisha injili inawafikia wengi.

Bwana akubariki.

Fuatilia ushuhuda huu utakuongezea nguvu katika kumtumikia Mungu bila kuangalia udhaifu wako.

Mwinjilisti mmoja wa kimarekani Ajulikanaye kama Rick Jonyer alikuwa akiomba kwa muda wa miaka 26 Mungu amnyakue mpaka mbingu ya tatu kama Bwana alivyofanya kwa mtume Paulo. Na siku moja ilipofika Mungu kusikia maombi yake alimchukua katika maono mbinguni kama tunavyosoma katika kitabu chake alichokiandika kijulikanacho kama THE FINAL QUEST, Kilichopata umaarufu mkubwa sana duniani kote. akieleza humo jinsi alivyoonyeshwa mambo mengi yahusuo hali za wakristo wa sasa kwa ujumla, Lakini hasa kwa wakati huu ningependa tujifunze kipengele kifupi cha maono hayo aliyoonyeshwa naamini lipo jambo kubwa sana la kujifunza .

Rick anasema alipofika wakati wa kupitishwa na Bwana mbele ya viti vya enzi vilivyopo mbinguni, aliona kiti kimoja kilichokuwa na utofauti kidogo, malaika wamekipamba na kukizunguka pande zote, na juu yake aliketi mfalme mkuu sana, na malaika walisimama pembeni yake wakisubiri maagizo kutoka kwake ya kufanya. Rick anasema alipokitazama kile kiti kwa ukaribu aliona sura ya mtu ambaye alishawahi kumwona mahali, ndipo alipomwomba Bwana amsogelee aongee naye, naye alipofika alimwambia: naona kama sura yako si ngeni machoni pangu, kama nilishawahi kukuona mahali ila sikumbuki ni wapi.

Lakini yule mtu ambaye jina lake ni Angelo akamwambia ulishawahi kuniona katika maono wakati fulani zamani. Ndipo Rick haraka akajaribu kukumbuka ni wapi ndipo kumbukumbu zake zikamjua kuhusu tukio hilo akasema: siku moja alivyokuwa kijana alitoka ndani na kwenda kukaa nje ya nyuma mbali kidogo na anapoishi sehemu ya utulivu akimsubiria Bwana azungumze naye huku akiwa anasoma biblia yake, anasema maono yalimjia saa ile ile na katika maono hayo aliona mtu mmoja mkristo mwenye bidii sana katika kumtumikia Mungu, alikuwa anashuhudia watu sehemu nyingi na kufundisha biblia mara kwa mara na kwenda kuwaombea wagonjwa kila mahali. Na muda huo huo akamwona na mtu mwingine tena aliyekuwa wa mtaani asiyekuwa na makazi ya kuishi anazurura tu huku na huko, ni mtu ambaye alikuwa hata akipita njia na kukutana na kitu chochote hata kitoto cha paka alikipiga kwa teke kitoke mbele yake.

Na ndipo Bwana akamuuliza , je kati ya hawa wawili ni yupi anayenipendeza zaidi?

Ni yule wa kwanza!: Rick akajibu kwa ujasiri wote.

Hapana! Ni wa pili. Ndipo Bwana akaanza kumweleza Rick habari zao wote wawili na maisha yao jinsi yalivyokuwa.

Yule wa kwanza alililewa katika familia nzuri, inayomjua sana Mungu na kumcha Mungu daima alililewa katika kanisa nzuri na hata alipata nafasi ya kwenda kujifunza masomo ya biblia katika vyuo. Alipewa asilimia 100 ya neema yangu lakini yeye aliweza kutumia asilimia 75 tu ya neema hiyo.

Lakini yule wa pili alizaliwa kiziwi, alikuwa ni mtu wa kunyanyapaliwa na hivyo alitelekezwa kwenye nyumba za kale sehemu za baridi mpaka siku alipokuja kukutwa na serikali ya nchi yao na kupelekwa katika vituo vya watu wasiojiweza, alihamishwa kituo kimoja hadi kingine, kutokana na kunyanyapaliwa na watu, lakini haikusaidia mpaka alipojikuta tena yupo mitaani alipokuwepo mwanzo. Hivyo Mungu akamuhurumia na kumpa sehemu tatu za neema yake, lakini alizishinda zote aliacha kuwapiga mapaka barabarani.. 

Pindi Bwana alipokuwa akisema nami niligeuka kumtazama tena huyo mfalme mkuu jinsi alivyoketi kwenye enzi kuu namna ile, mwenye utukufu mwingi kushinda hata wa Sulemani, malaika wamemzunguka kila mahali wakisubiria maagizo kutoka kwake. Ndipo nilipomgeukia tena Bwana na kumsihi BWANA azidi kunielezea juu ya habari ya huyu mtu.

Bwana akasema Angelo alikuwa mwaminifu kwa kila neema niliyompa, Nilimwongezea sehemu nyingine tatu za neema yangu na zote akazitenda kiuaminifu. Akaacha kuiba, hata wakati alipopitia katika mazingira magumu nusu ya kufa kwa njaa lakini hakutaka kuiba mali ambayo haikuwa ya kwake kwa ajili ya kwenda kujishibisha. Alijinunulia chakula chake kwa pesa yake mwenyewe aliyoipata katika kukusanya makopo barabarani aliyoyauza. Na mara chache akipata kazi za kusafisha uani katika majimba ya watu.

Angelo alikuwa ni kiziwi lakini alijifunza kusoma. Hivyo nilimpelekea nakala za vipeperushi cha Injili. Na Alipovisoma Roho wangu alimfungua macho yake na ndipo akayakabidhi maisha yake kwangu. Nikamwongozea tena sehemu ya neema yangu, na zote hizo alizitumia kuaminifu. Alitamani sana kushuhudia habari zangu kwa watu wengine lakini hakuweza kuongea, lakini japo kuwa alikuwa katika hali ile hakutana habari zangu zisiwafikie wengine. Alianza kutumia zaidi ya nusu ya alichokipata kusambaza kipeperushi vya injili mabarabarani.

Ndipo nikamuuliza Bwana, Ni watu wangapi aliowavuta kwako?, ni wazi itakuwa maelfu ya watu, mpaka ifikie hatua ya kuketi katika viti vya wafalme ni lazima atakuwa amewavuta wengi.

Lakini Bwana akamwambia: Alifanikiwa kumvuta mtu mmoja tu kwangu. Nilifanya hivyo Ili kumtia moyo alimvuta mlevi mmoja aliyekuwa anakaribia kufa barabarani. Na hiyo ilimtia moyo sana kiasi cha kumfanya aweze kuendelea kukaa miaka mingi zaidi barabarani kujaribu kumvuta mtu mwingine kwangu. Lakini mbingu nzima ilikuwa inamfurahia kutaka aje huku juu, nami pia nilitamani aje apokee ujira wake. Huyo ni Angelo.

Lakini ni kitu gani kilimfanya Angelo aweze kuwa mfalme hapa? Niliuliza.

Alikuwa mwaminifu kwa vyote alivyopewa aliyashinda yote mpaka alipokuwa kama mimi, yaani KUFA KWA AJILI YA IMANI.

Lakini je! yeye naye alishindaje shindaje, na alikufaje kufaje kwa ajili ya Imani? Niliuliza tena.

Aliushinda ulimwengu kwa UPENDO wangu. Wachache sana wanaweza kushinda wakiwa na vichache. Watu wangu wengi wanaishi katika mazingira mazuri zaidi hata ya wafalme walioishi karne moja iliyopita lakini bado hawana shukrani kwa hayo.Lakini Angelo yeye hakuwa hivyo, yeye aliweza hata kushukuru kwa boksi aliloliokota barabarani na kuligeuza hilo kuwa hata sehemu yake ya kufanyia ibada. Alianza kupenda kila kitu alichokiona na kila mtu,aliweza kupenda hata tunda la tofaa zaidi hata ya watu wanavyoweza kufurahia sherehe kubwa wazifanyapo. Alikuwa mwaminifu kwa kila nilichompa japokuwa nilichompa hakikuwa kikubwa kulinganisha na wengine lakini yeye alikuwa mwaminifu katika hivyo.

Nilikuonyesha maono juu yake wakati ule, kwasababu ulishampita mara nyingi barabarani.

Ndipo nilipotaka kufahamu nilifanya nini nilipomuona.

Bwana akasema ulimnyooshea kidole chako na kumwambia rafiki yako, kuwa watu kama hao wanaosimama kwenye vituo vya mabasi ni watu waliotumwa na shetani kuuvuruga ukristo, watu waliopoteza mweleko wa imani.

Niliposikia hivyo nilijisikia mnyonge na mwenye aibu nyingi, ndipo nikamwomba Bwana anisamehe akasema umeshasamehewa.

Bwana akaendelea kusema, alikuwa na mengi ya kuwapa watu wangu lakini hawakupenda kumsogelea. Alikuwa mwaminifu kwa alichokipata alinunua biblia yake, na baadhi ya vitabu kusoma lakini alipojaribu kwenda katika makanisa hakuna mtu aliyempokea. Kama wangempokea basi wangekuwa wamenipokea mimi. 

Ndipo nilipozidi kutaka kufahamu Angelo alikufaje kufaje?

Bwana akasema: Aliganda katika baridi kujaribu kumwokoa mlevi mmoja barabarani.

Ndipo nipomuliza Bwana najua anastahili kuwepo hapa lakini je! si ni wale watu wanaokufa kwa ajili ya injili yako ndio wanaohesabika kuwa ni mashahidi wako waaminifu. Inakuwaje kwa huyu?

Angelo alikuwa anakufa kwa ajili yangu kila siku, aliweza kuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya mtu mwenye uhitaji. Kama Mtume Paulo alivyosema, hata nikiutoa mwili wangu wote uungue na moto kama sina upendo mimi si kitu, lakini kama utautao uhai wako katika upendo hiyo inahesabika sana mbele za Mungu. Angelo alikuwa anakufa kila siku kwasababu alikuwa haishi kwa ajili yake, bali kwa ajili ya wengine. Japokuwa alikuwa anajiona mwenyewe kuwa ni mdogo katikati ya watakatifu lakini kiuhalisia alikuwa ni mkubwa sana. Wale watu wanaojiona kuwa ni wakubwa na kusifiwa na watu wengi wao wanaishia kuwa wadogo huku.

Mwisho wa nukuu.

*******

Bwana Yesu alisema..Luka 16:10 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.”

Ujumbe huu ukutie nguvu..aumke na kuanza kumtumikia Mungu kwa bidii zote bila kujalisha jinsi ulivyo au mahali ulipo. Kumbuka dhawabu utapewa kulingana na uaminifu wako.. kama leo haufanyi lolote kwa Mungu, unahudhuria tu kanisani tegemea kuambiwa siku ile haya maneno..

… Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

[27]basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

[28]Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

[29]Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa”. (Mathayo25:26-29)

Wakati wenzako waliokuwa wanajuhudi katika kumtumikia Mungu pamoja na udhaifu wao wakipongezwa na kupewa mataji, wewe utakuwa katika majuto ukisema ningejua ningetumika na mimi hata katika kile kidogo nilichokuwanacho.

Lakini kama hujaokoka yaani hujatubu dhambi zako na kupokea Roho Mtakatifu, basi habari ya kumtumikia Mungu na kwenda mbinguni haitakuhusu kabisa..bali sehemu yako itakuwa ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti (Ufunuo 21:8), hivyo ni heri uamue leo kuokoka kweli kweli ili uanze kumtumikia Mungu.. kumbuka muda tuliobakiwa nao ni mfupi sana.. hizi ni siku za mwisho na YESU KRISTO yupo mlangoni.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *