Ni nini tunajifunza kwa Shamgari?
Shamgari alikuwa ni shujaa wa Israeli aliyetokea kipindi cha Waamuzi na kuwaokoa Israeli mikononi mwa Wafilisti kwa kuwapiga watu mia sita (600) kwa mkono wake mwenyewe akitumia tu fimbo ya kuswagia ng’ombe.
Tusome habari yenyewe..
Waamuzi 3:31 “Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng’ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.
Konzo la ng’ombe ni fimbo ya kuchungia ng’ombe, hebu tafakari mtu mmoja awapige watu 600 tena kwa fimbo, ni muujiza mkubwa mno!!
Je! sisi kama wakristo nini tunajifunza tunaposoma habari kama hizi?
Katika Agano letu (Agano jipya) hatupigani na wanadamu wenzetu, vita vyetu si ya damu na nyama.. yaani hatutumii silaha za mwilini kama mapanga, marungu, fimbo, n.k, bali biblia imetuelekeza kuwa kushindana kwetu ni juu ya falme na mamlaka, juu ya ya wakuu wa giza hili, juu ya mapepo wabaya katika ulimwengu wa roho. (Waefeso 6:12)
2Wakorintho 10:3 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)”
Hapo Neno la Mungu linasema silaha za vita vyetu si za mwili, bali ZINA UWEZO KATIKA MUNGU HATA KUANGUSHA NGOME.
Na silaha zetu ni zile zilizotajwa katika Waefeso 6:10-18, ambayo ni pamoja na kweli kiunoni, dirii ya haki kifuani, utayari wa kuhubiri Injili, ngao ya imani, chepeo ya wokovu, upanga wa roho ambao ni neno la Mungu, maombi.
Ukiwa na hizo silaha zote unaonekana kama mwanajeshi aliyekamilika kwa ajili ya vita, na kama mkristo ni lazima tuwe na silaha zote.. tuwe tayari kwa vita muda wowote. Kumbuka silaha hizi zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.
Sasa tukirudi katika habari hiyo ya Shamgari, huyo shujaa wa Israeli aliyewaokoa Israeli kwa mkono wake mwenyewe kwa kuwapiga maadui zake jeshi lote la Wafilisti watu mia sita kwa fimbo ya ng’ombe..
Nini tunajifunza kwa habari hiyo? Je! na sisi tunaweza kuwa mashujaa kama yeye? tunaweza tukawapiga maadui zetu (shetani na maajenti wake) bila kutegemea kuwa na silaha kubwa, au kutegemea misaada..
Wakati mwingine tunapaswa tufike mahali tuweze kusimama wenyewe na kupigana na adui zetu Ibilisi pasipo kutegemea viongozi wetu, pasipo kutegemea visaidizi, ndiyo kuna mahali utahitaji kushirikisha waumini wenzako ili muongeze nguvu, au viongozi wako wa kiroho ila sio kila mara utafanya hivyo, kuna wakati inakubidi usimame mwenyewe pasipo kujalisha kiasi cha imani uliyonayo kwa wakati huo, Kuna wakati Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake maneno haya…
Mathayo 17:19 Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?
20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
Inahuzunisha unapomkuta mkristo anahangaika kila kukicha huku na huku kutafuta msaada wa maombezi, anashindwa kutumia ile silaha aliyonayo (ngao ya imani) kumshinda adui kwa kujiombea, na kuombea familia yake, ndugu zake, kanisa na watu wote kwa ujumla, kisa tu atakuambia yeye hana imani kama aliyonayo mtu mwingine..atakuambia yeye hajakomaa, bado anahitaji kufika katika kiwango fulani labda aweze kusimama mwenyewe, anahitaji afikie kiwango fulani cha imani ili aweze kuhubiri Injili, au kwenda kuwaombea wagojwa, na kuwafungua waliofungwa na nguvu za giza.
Kama mwamini tumia imani uliyonayo hata kama ni ndogo kiasi cha punje ya haradali hiyo ndiyo fimbo yako kwa sasa usisubiri mpaka uwe na mabomu ya nyukilia, au silaha kubwa za kisasa, tumia tu fimbo utaona utakavyoangusha adui zako kwa namna ya ajabu, kumbuka silaha zetu zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.
Hiyo hiyo Imani uliyonayo anza kufanya kazi ya Mungu, anza kujiombea kwa imani, anza kuwaombea wagojwa, utaona Bwana atakavyokushangaza, huo mlima utashangaa umehama kwenda kule kwa hiyo imani yako tu ndogo! huo ugojwa sugu hautasimama mbele yako maadam utatumia tu imani yako na kadri unavyotumia ndivyo unazidi kuimarika na ile imani ambayo ilikuwa kama punje ya haradali itafika mahali itakuwa mti mkubwa,
Zekaria 4:6 Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi.
7 Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta liwe jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.
Tumia nguvu uliyonayo, imani uliyonayo kuangusha ngome za adui, achana na tabia ya kutafuta tu kuombewa-ombewa, simama mwenyewe na Bwana atakuwa pamoja nawe, wakati fulani Yonathani alipoona maadui zao wanakuja kuwavamia na wao hawana silaha isipokuwa yeye tu na baba yake (Sauli), alinyanyuka kwa ujasiri bila hata kumtarifu mtu yoyote wakaenda yeye na mtumwa wake wakawapiga maelfu ya jeshi lote la Wafilisti na Bwana akaleta wokovu mkuu kwa Israeli kwa mkono wa watu wawili tu kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwa wachache. (1Samweli 14:1-16)
Naamini leo utaanza kusimama wewe kama wewe na Bwana akusaidie.
Je! umeokoka?? Je! unahabari kuwa tunaishi katika muda wa nyongeza na Kristo yupo mlangoni kurudi!
Fahamu kuwa huwezi kumshinda adui ukiwa nje ya wokovu! mwamini Bwana Yesu na kisha mruhusu aingie ndani yako ili akubadilishe na akupe nguvu ya kumshinda adui, unachopaswa kufanya baada ya kumwamini ni kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi zote na kwenda kubatizwa kwa maji mengi na Kwa Jina lake sawa sawa na Matendo 2:38 na utapokea muhuri wa Roho Mtakatifu ambaye atakusaidia kushinda dhambi na kuishi maisha ya utakatifu.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.