UMCHUKUE MWANAO, MWANA WAKO WA PEKEE, UMPENDAYE.

Biblia kwa kina No Comments

UMCHUKUE MWANAO, MWANA WAKO WA PEKEE, UMPENDAYE.

Shalom jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe daima.

Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Siku ya leo tutajifunza umuhimu wa kumtolea Mungu wetu vile vinavyotugharimu.

Wengi wetu tunafahamu ile habari ya Ibrahimu baba yetu wa Imani..kumtoa Isaka mwanaye pekee kuwa sadaka ya kuteketezwa, Mungu alimwambia Ibrahimu..

Mwanzo 22:2 “Akasema, UMCHUKUE MWANAO, MWANA WAKO WA PEKEE, UMPENDAYE, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

Sasa tukisoma hiyo habari..huwa tunadhani ni jambo jepesi..ila hebu leo hii ujiweke kwenye hiyo nafasi ya Ibrahimu.

Mungu akuambie mtoe mwanao, mwana wako wa pekee, tena umpendaye halafu umtolee yeye awe sadaka ya kuteketezwa (yaani ukamkate kate vipande na kisha umchome moto kabisa) bila shaka utasema Mungu ni katili, hana upendo.

Tena ukizingatia ni huyo tu ndiye tumaini lako na ulimpata kwa shida..halafu leo hii umteketeze kabisa, ukweli ni kwamba sio jambo jepesi…linahitaji Neema kubwa, na moyo wa kumpenda Mungu sana na kumwamini kwa asilimia yote… Ibrahimu kwa vile alivyomwamini Mungu na kwa jinsi alivyompenda..hakuona shaka kumtoa mwanae wa pekee kuwa sadaka kwa Mungu..aliamini uweza wa Mungu kwamba Mungu aweza kumfufua hata kutoka kwa wafu (Waebrania 11:17-18).

Na sisi tulioitwa katika Imani..tunapaswa tuwe vivyo hivyo kama baba yetu Ibrahimu, tuige ule moyo wa Ibrahimu wa kumpenda Mungu na hiyo imani ya kumwamini Mungu namna hiyo…hadi kufikia kiwango cha kumtoa mwanaye wa pekee kuwa sadaka ya kuteketezwa.

Lakini kutokana na upendo wa wengi kupoa katika siku hizi, hiyo imani na huo moyo wa kumtolea Mungu ni nadra sana.

Leo hii Mungu anaweza asikuambie umtoe mwanao, mwana wa wako wa pekee, umpendaye iwe sadaka ya kuteketezwa, lakini Bwana amekupa mali, amekupa viwanja, n.k ila hebu jiweke sawa na Ibrahimu, Mungu anataka umchukue mwanao, mwana wa wako wa pekee umpendaye, ambaye yaweza kuwa ni kiwanja chako au mali yako umtolee Bwana kwa ajili ya kuendeleza kazi yake..je! upo tayari? au utasema hiyo imani tuachie wakina Ibrahimu.

Ukiona hivyo ujue bado hujaingia katika imani ya kumwamini kwanza Kristo, au upendo wako na Mungu umepungua kabisa au haipo.

Hebu leo anza tena upya, anza kumpenda Mungu hata kwa vile vidogo ulivyo navyo..sio lazima uwe bilionea.

Mwana wako wa pekee ni kile cha thamani ambacho unakichikilia katika maisha yako, hebu jifunze kumtolea Mungu maana ni kwa faida yako..kuna faida sana katika kumtolea Mungu vitu vya thamani, mbona unaweza ukajitoa tu kwenye vitu vingine vya kidunia kwanini usimtolee pia Mungu…mchango wa harusi unatoa laki moja, lakini ukisikia mchango wa kupeleka injili..unatoa elfu kumi? Halafu unategemea Mungu akubariki zaidi… nataka nikuambie umpandacho ndicho utakachovuna.

Ukiingia  gharama kubwa kumpa Kristo kitu Fulani  jambo ambalo mtu wa kawaida hawezi kufanya, ..mbinguni unahesabika ni kama umemwaga damu yako kwa ajili yake kama wale mashujaa wa Daudi ambao walihatarisha maisha yao kumletea Daudi maji ya thamani sana mpaka daudi akayageuza hayo maji kuwa thabihu ya Bwana kama vile damu ya wanyama ilivyokuwa ikitolewa kuwa dhabihu. (2Samweli 23:13-17)

Leo hii ukimtolea Mungu kwa moyo wa upendo…Haijalishi hicho kitu ni kidogo kiasi gani, kinachojalisha ni gharama uliyoingia. Je ni kubwa kiasi gani..mbele za Mungu, Yule mwanamke aliyekuwa mjane, aliingia gharama kubwa kutoa kila alichonacho ingawa kwa nje ilikuwa ni senti mbili tu.

Tujifunze pia kwa yule mwanamke aliyevunja kibweta chake cha Pafyumu ambacho thamani yake ilikuwa ni kubwa sana sawa na pesa za kitanzania milioni 6.

Yule mwanamke hakujali hiyo thamani alikivunja kabisa hicho kibweta/kijagi na kumimina kichwani pa Bwana. Mpaka wengine wasiompenda Bwana wakamlalamikia kwanini unaharibu pesa nyingi namna hii. (Marko 4:3-8).

Hata sasa, kila mmoja wetu anachokibweta chake, ni suala tu la muda.. Utajiuliza, unamtazama msanii Fulani kwenye tv, anamwaga pesa, na kuwapa makahaba, au ananunua gari la kifahari, halafu wewe unaanza kulalamika na kusema upotevu wote huo wa nini, si ni heri angewasaidia maskini, kuliko kutumia kwa anasa.. Usimlaumu kibweta chake ndio amekivunjia hapo.

Leo hii, utaona, mtu kumtolea Mungu, au kusapoti huduma ambazo zinamsaidia kiroho ni ngumu, hata halifikirii.. Lakini mwanawe akitaka kwenda shule, atahangaika kila mahali kumtafutia ada, au akiumwa, anahitaji kwenda kutibiwa India, atauza, gari mpaka shamba, kusudi kwamba aokoe maisha ya mwanawe..Hicho ni kibweta chake amekivunja.

Tujiulize, vipi kuhusu Mungu wetu..Yesu wetu aliyetuokoa, twaweza kudhubutu kuwa kama huyu mwanamke? Ambaye alikivunjia kwa Bwana?..Hakujua kwa kufanya vile, injili yake itahubiriwa kizazi baada ya kizazi.. Na Yesu ni yeye Yule jana na leo na hata milele.. Kama alimfanyia huyu, anaweza pia akakufanyia na wewe, kwa namna yako..Lakini ni lazima ukivunje kibweta chako kwake..Unafurahi vipi, Bwana akuhudumie, halafu wewe umuhudumii?

Tafakari!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Je umempokea Yesu?

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *