Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako;
Isaya 37:28 “Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; NA GHADHABU YAKO ULIYONIGHADHIBIKIA.”
Watu wengi huwa wanadhani wanapofanya maovu na huku hamna hatua yoyote inayochukuliwa na Mungu dhidi yao, wanafikiri au wanadhani labda Mungu hajui kinachoendelea juu ya maisha yao.
Hivyo wanaendelea kufanya dhambi na kufurahia mapato ya dhambi wasijue kuwa dhambi ina mshahara wake na mshahara wake ni mauti(Warumi 6:23), na Mungu anaendelea kuwavumilia ili wafikilie toba kwa maana yeye anasema hafurahi kufa kwake mtu mwovu… Ezekieli 18:23,
Ndugu/Dada, Fahamu kuwa Mungu anakujua vizuri, anajua mahali unapoketi sasa, anajua kutoka kwako, na kuingia kwako pia, anajua dhambi zako zote hata zile unazozifanya sirini,
Anajua biashara haramu unayofanya, anajua machukizo unayomchukiza, kila neno unalolitamka analijua, yeye ni shahidi juu mambo yako yote hata yale unayoyakosea bila kujua zaidi hayo unayoyajua!
Unapoenda kufanya uzinzi, uasherati, na kujichua anakuangalia tu na kukuhusunikia, wakati unafurahia rushwa na kusema uongo anakushudia tu, anasema yeye ni shahidi mwepesi juu ya wazinzi, wachawi, na juu ya waapao kwa uongo.
Malaki 3:5 “Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake.”
Dada/Kaka Usifurahie tu unapoendelea kukaa katika dhambi ukadhani Mungu hakuoni, au ukajifariji kuwa Mungu ni wa rehema na wa upendo hivyo hachukizwi na wewe,
Leo ondoa hayo mawazo kabisa, fahamu kuwa Mungu hapendezwi kabisa na hayo machukizo unayomchukiza, apendezwi na hizo tabia zako chafu, huo usengenyaji na uchonganishi unaofanya.. Mungu hapendezwi nao.
Unapoona leo Bwana anakaa kimya pale unapoiba, unapozini na hakuna lolote baya linalokupata, nataka nikuambie ni huruma zake tu na wema wake ndio maana hupatwi na mabaya, ila fahamu kuwa Mungu anakuvumilia ili utubu, kwa maana ukifa kwanye hali hiyo ni huzuni kwakwe.
Hivyo ndugu usiendelee kudharau huo wema wa Mungu na uvumulivu wake anapokuvumilia katika maisha yako ya udunia ili utubu, dhamiria kutubu na kumpa Bwana maisha yako. Fahamu kuwa unapoendelea kuishi katika dhambi na kufanya moyo wako kuwa mgumu unazidi kujiwekea akiba ya hasira kwa ile siku ya hasira.
Warumi 2:4 Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumulivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?
5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,
6 atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;
Unapoendelea kufurahia raha za ulimwengu, na kufanya vile utakavyo, na kutumia mwili wako vile utakavyo, kuweka kila aina ya uchafu, na kutembeza uchi, fahamu kuwa Mungu anajua hiyo ghadhabu unayomghadhibikia, usidhani kwamba we ni mjanja sana na wengine waliokana nafsi zao na kuachana na ulimwengu usifikiri wao ni wajinga, Bwana anakuvumilia tu ndio maana leo upo hai, pengine usingefika leo kwa jinsi unavyomgadhibikia Mungu, yamkini ungeshuka siku nyingi shimoni(kuzimu), ila Bwana bado anakupa muda utubu kabla siku zilizo mbaya hazijakufikia.
Isaya 37:23 Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuingia macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.
28 Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako uliyonighadhibikia.
29 Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu, nitatia kulabu yangu katika pua yako, na hatamu yangu midomoni mwako,..
Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Kumbuka..
Kwa Yesu lipo tumaini la uzima wa milele, Kwa Yesu Unapata utulivu wa nafasi na faraja. Alisema.
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.
Kwa Yesu zipo Baraka.
Na kwa Yesu upo msahama wa kweli:
Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.
Kwa hiyo unapokuja kwake leo hii kwa kumaanisha, ujue kuwa hiyo mizigo ya dhambi uliyonayo haijalishi ni mingi kiasi gani ataitua mara moja, haijalishi uliuwa watu wengi namna gani, haijalishi ulizini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, haijalishi ulikwenda kwa waganga mara nyingi namna gani..Ikiwa tu upo tayari leo kumkaribisha Yesu moyoni mwako basi ataitua, na kukusamehe kabisa kana kwamba hakuna chochote ulichowahi kumkosea..Na atakupa amani.
Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..
Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..
Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.
Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Hongera kwa kuokoka.
Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namna zilizopo hapo chini.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.